Kabla ya kukamatwa ndege
Mwaka 1983 kupitia Kifungu cha 3( 1 ) cha Sheria iliyoitwa Acquisition and Transfer Management Act, 1983 kampuni sita za Mzungu Hermanus Steyn ambazo ni Rift Valley Seed Ltd, Hashman Estate Ltd, Lente Estate Ltd, Loldebbis Ltd, Mayoka Estate Ltd na Tanganyika Air Ltd zilitaifishwa na Serikali ya Tanzania.
Baadaye Steyn alifungua malalamiko kwenye taasisi ya usuluhishi (arbitration) akiomba haki zake zote katika kampuni zote zilizotaifishwa, jambo ambalo alifanikiwa mbele ya Jaji R.V. Makaramba aliyeamua alipwe Dola za Marekani 36,375,672.81 (Dola milioni 36).
Muda ukapita, lakini baadaye Mei 2011 Mzungu huyo akaamua kuisajili hiyo hukumu ya taasisi ya usuluhishi katika Mahakama Kuu ya Biashara ili iwe hukumu ya mahakama, hivyo iweze kutekelezeka.
Julai 2012 wakati akiwa katika mchakato wa kufuatilia utekelezaji, serikali na Mzungu huyo wakaingia makubaliano kuwa aachane na hiyo hukumu ili imlipe Dola za Marekani 30,000,000 ( Dola milioni 30) badala ya zile 36,375,672.81 zilizoamuliwa awali.
Mzungu akakubali na makubaliano yakasainiwa, na makubaliano hayo yakasajiliwa na mahakama, hivyo yakasimama kama hukumu mpya ya mahakama.
Kufikia Machi 2016, serikali ikawa tayari imemlipa Mzungu huyo Dola za Marekani 20,099,155.12 (dola milioni 20).
Mwaka 2018 wakati malipo yanaendelea kidogo kidogo, serikali ikasitisha malipo na kufungua maombi namba 168/2018 Mahakama Kuu ya Biashara Tanzania. Ikawa inaiomba mahakama iifanyie marejeo hukumu ya taasisi ya usuluhishi iliyoamua Mzungu kulipwa Dola za Marekani 36,375,672.81, kwa hoja kuwa ilikuwa na upungufu wa kisheria.
Desemba 2018, Jaji B.K. Philip alitoa uamuzi kwa kukataa maombi ya serikali ya kuifanyia marejeo hukumu hiyo, kwa hoja kuwa hukumu hiyo haipo na ilishakufa baada ya serikali na Mzungu kuamua kuelewana na kuyasajili maelewano hayo mahakamani, hivyo kuyafanya maelewano hayo kuwa hukumu mpya.
Katika maombi hayo serikali iliwakilishwa na Wakili Jacqueline Kinyasi, wakati Steyn aliwakilishwa na Wakili Erick Ng’maryo.
Hoja kuu ya Wakili Erick hapo mahakamani ilikuwa kwamba uamuzi wa taasisi ya usuluhishi (arbitration) ulishakufa na haupo, na kuwa uamuzi huo uliuliwa na makubaliano kati ya mteja wake na serikali, ambapo makubaliano hayo nayo yalisajiliwa yakawa hukumu mpya ya mahakama, hivyo serikali kuiomba mahakama ifanye marejeo ya hukumu hiyo ya awali ni sawa na kuiomba irejee kitu ambacho kilishakufa na hakipo.
Mahakama ilikubali hoja hii ya Wakili Erick na kumpa ushindi kwa hoja hii. Kumbuka huyu Erick ndiye anayetajwa kuongoza mchakato wa kuzuiwa kwa Airbus Afrika Kusini.