Miaka mitatu iliyopita, deni la taifa lilikuwa Sh trilioni tano hivi, lakini mwaka huu wa 2012 deni hilo limepanda hadi kufikia zaidi ya Sh trilioni 20.
Wataalamu wa uchumi wamelizungumza jambo hilo ndani na nje ya Bunge. Kuna hoja kwamba ukubwa wa deni si hoja, hasa kama linalinganishwa na wastani wa pato la taifa na ukuaji uchumi.
Aidha, wananchi wanaaminishwa kwamba deni hilo limepaa kwa kasi hiyo ya kutisha kutokana na mikopo ya fedha za maendeleo ya ujenzi wa miundombinu, kilimo, mawasiliano na kadhalika. Kwa vyovyote itakavyosemwa, ukweli ni kwamba deni hili ni mzigo mkubwa mno kwa Watanzania, hasa masikini.
Tunaungana na wale wanaosema kuwa kukopa si hoja, alimradi fedha zinazokopwa zinakuwa na tija katika miradi iliyokusudiwa. Kinachosikitisha ni kwamba mara kadhaa mikopo mingi imekuwa haina tija ya moja kwa moja kwa wananchi.
Hivi karibuni kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilibainika kuwa Serikali inamiliki magari yenye thamani inayozidi shilingi trilioni tano. Hizi ni fedha nyingi mno kwa sekta moja tu ya magari.
Bado kuna upangaji nyumba kwa viongozi na watumishi mbalimbali wa umma. Itakumbukwa kuwa miongoni mwa makosa makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu, ni ya kuuza nyumba za watumishi wa umma. Viongozi na watumishi wengi waligawana nyumba ambazo sasa wamezibadili na kuwa vitegauchumi.
Nyumba za watumishi wengi, wakiwamo mawaziri, majaji, wakurugenzi na wengine wa kada mbalimbali ziliuzwa. Hatua hiyo imewalazimu baadhi ya majaji, mawaziri na wakurugenzi waishi katika hoteli au nyumba za kupanga kwa gharama kubwa mno.
Hapana shaka kwamba fedha zinazotumika kuwalipia nyumba hizo, zikawa zinachotwa kwenye mfuko mkuu wa fedha za Serikali ambao kimsingi unapaswa kujielekeza zaidi kwenye shughuli za maendeleo.
Haishangazi kuona kuwa fedha zinazotengwa kwenye bajeti kwa shughuli za maendeleo zinakuwa kidogo kuliko zile zinazotengwa kwa matumizi ya kawaida.
Ndiyo maana tunaungana na wale wote wenye shaka juu ya ukuaji wa deni la Taifa kwa sababu mzigo huo utawalemea watoto na wajukuu zetu. Pia tunadhani kuwa utaratibu wa kukopa unapaswa kuwa na mkondo maalumu kwa sababu ilivyo sasa ni kwamba hakuna umakini katika ruhusa ya taasisi kukopa.
Matarajio yetu ni kuona kuwa ukusanyaji kodi, hasa kutoka kwenye kampuni kubwa, unazingatiwa ili kuiwezesha Serikali kuwa na mapato yenye kuiwezesha kujiendesha.
Aidha, ukuaji wa deni la taifa unapaswa kwenda sambamba na uboreshaji miuondombinu, hasa ya reli. Pamoja na juhudi za kujenga barabara za lami nchini kote, hatuamini kama hilo litakuwa na tija hasa kutokana na ukweli kwamba kila inapomalizika kujengwa barabara moja, nyingine iliyokuwa ikitumika inakuwa imeshaharibiwa na shehena nzito za malori. Dawa pekee ni kuimarisha reli.
Kwa yyovyote iwavyo, tunapaswa kuwa waangalifu juu ya ukuaji huu wa kasi wa deni la Taifa.