Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amekiri hadharani kwa mara ya kwanza kwamba vikosi vya Ukraine viko katika eneo la Belgorod, Urusi.
Katika hotuba yake aliyoitoa Jumatatu, Zelensky alisema, “Tunaendelea kufanya operesheni za kijeshi katika maeneo ya mipakani kwenye ardhi ya adui, na hiyo ni haki kabisa – vita lazima virejee mahali vilipotokea.”
Kauli hii pia ilihusiana na eneo la Kursk, ambapo Ukraine inashikilia sehemu ndogo baada ya shambulizi kubwa mwaka jana, ingawa Moscow imechukua tena udhibiti wa sehemu kubwa ya eneo hilo.
Zelensky alifafanua kuwa lengo kuu la operesheni hizo ni kulinda maeneo ya mipaka ya Sumy na Kharkiv, na kupunguza shinikizo katika maeneo mengine ya mstari wa mbele, hasa katika eneo la mashariki la Donetsk.
Jeshi la Urusi liliripoti mwezi uliopita kwamba Ukraine ilijaribu kuvuka mpaka na kuingia kwenye eneo la Belgorod, lakini walidai kuwa mashambulizi hayo yalizuiwa kwa mafanikio.
Rais Zelensky alithibitisha kuwa operesheni za kijeshi za Ukraine katika maeneo ya Kursk na Belgorod ni sehemu ya juhudi za kulinda nchi yake dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Mnamo tarehe 18 Machi, Zelensky alikiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba vikosi vya Ukraine viko kwenye eneo la Belgorod, akisema “Kuna operesheni inayoendelea huko,” alipoulizwa kuhusu taarifa za Urusi zinazosema kuwa vikosi vya Ukraine vilijaribu kuingia sehemu ya magharibi ya Belgorod bila mafanikio.
Taarifa za hivi karibuni kutoka kwa wanablogu wa kijeshi wa Urusi zinaonyesha kuwa vikosi vya Ukraine vinajiondoa kutoka eneo la Demidovka, likionyesha kuwa operesheni za Ukraine katika eneo hili ni za kiwango kidogo ikilinganishwa na zile za Kursk, ambapo Ukraine ilishinda vijiji vingi, ikiwemo mji wa Sudzha.
Hali hii pia inaweza kumaanisha kuwa Ukraine inatumai kubadilishana maeneo ya Urusi inayoshikilia kwa sehemu za maeneo ya Ukraine yanayoshikiliwa na Moscow katika mazungumzo yoyote ya amani ya baadaye.
Wachambuzi wa vita, hasa kutoka Ukraine na Magharibi, wamehoji ufanisi wa kijeshi wa operesheni hizi za Ukraine kwenye ardhi ya Urusi, wakibaini idadi kubwa ya majeruhi na changamoto za upatikanaji wa silaha.
