Ukraine imeripotiwa kurusha kwenye maeneo ya ndani ya Urusi makombora ya masafa marefu aina ya Storm Shadow yaliyotengenezwa na Uingereza. Hii ni licha ya Urusi kuendelea kuonya dhidi ya hatua ya aina hiyo.

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema ofisi yake haiwezi kuzungumzia ripoti hizo au masuala ya kiutendaji. Uingereza imekuwa ikiipa Ukraine makombora ya masafa marefu ya Storm Shadow tangu mwaka jana lakini ilikuwa imeruhusu yatumike katika maeneo yanayokaliwa ya Ukraine pekee.

Sasa, baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuondoa vikwazo kwenye matumizi ya Ukraine ya makombora ya Kimarekani aina ya ATACMS kwenye maeneo yaliyoko ndani kabisa ya Urusi, inaonekana kama Uingereza imefuata mkondo huo.

Makombora ya Storm Shadow, na yale ya Ufaransa ya SCALP – yanaweza kuruka umbali wa zaidi ya kilomita 250. Mwezi Septemba, Kyiv iliyatumia makombora ya Storm Shadow kuyapiga makao makuu ya manowari za Urusi katika Bahari Nyeusi ya Sevastopol huko Crimea.

Rais wa Urusi Vladmir Putin anaonya kuwa matumizi ya makombora yaliyotengenezwa Marekani na Uingereza kwenye ardhi yake itakuwa sawa na NATO kuingia moja kwa moja katika vita na Urusi.