Ukraine imerusha zaidi ya droni 24 kuulenga mkoa wa Urusi wa Kursk ikiwa ni sehemu ya kampeni yake ya kijeshi iliyoanza siku ya Jumamosi usiku ambayo imefanikiwa kuharibu bohari ya mafuta.
Hayo yamesemwa na kaimu gavana wa mkoa huo unaopakana na Ukaine, Andrei Smirnov. Kulingana na afisa huyo, droni 13 za Ukraine zilidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi ikiwa ni siku moja tu tangu droni nyingine 19 kuharibiwa zikiwa njiani kuulenga mkoa huo.
Andrei amesema mashambulizi hayo yalisababisha uharibifu mdogo kwenye majengo ya maakazi lakini hakutoa ufafanuzi zaidi kuhusu athari zilizotokea.
Katika miezi ya karibuni Ukraine imekuwa ikiilenga miundombinu ya nishati na kijeshi ya Urusi kwa dhamira ya kuvuruga uchumi wa nchi hiyo na uwezo wake wa kuendelea na vita vilivyoanza kwa uvamizi wa jeshi la Urusi mnamo Februari 2022.