Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema kuwa kutotabirika kwa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kunaweza kusaidia kumaliza vita na Urusi.

Trump, ambaye anatarajiwa kuapishwa rasmi Januari 20, aliahidi kuumaliza mzozo huo wa muda mrefu wa takriban miaka mitatu ndani ya saa 24 baada ya kuingia madarakani.

Hata hivyo, Ukraine ina wasiwasi kuwa itahitaji kuachia maeneo yaliyodhibitiwa na Urusi ili kufikia amani.

Katika mahojiano na televisheni ya Ukraine, Zelensky alisema kwamba Trump ni mtu mwenye nguvu na ambaye hatabiriki, akionyesha matumaini kwamba ushawishi wake utaweza kumaliza mgogoro na Urusi.

Zelensky amejaribu kujenga uhusiano na timu ya Trump tangu uchaguzi wa Novemba, huku hofu ikiwa imetanda kwamba chama cha Republican kinaweza kupunguza msaada muhimu wa kijeshi kutoka Marekani katika juhudi za kumaliza mzozo huo.