Deodatus Balile

Deodatus Balile

Pole Sioi Sumary. Hongera Joshua Nassari. Nyota ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inachanua. CCM waanze kujifunza kuwa kambi rasmi ya upinzani mwaka 2015. Haya ni maneno ya utangulizi niliyolazimika kuanza nayo katika safu hii ya Sitanii. Ikiwa mazingira hayatabadilika, nitakachokitabiri hapa ndicho kitakachotokea mwaka 2015.

Mwaka 1929 kilipoanzishwa chama cha Tanzania African Association (TAA), lengo lao ambalo lilikuja kuchukuliwa na Tanganyika African Union (TANU) mwaka 1957, lilikuwa ni jinsi ya kuondokana na unyanyasaji wa mkoloni. Unyanyasaji unaozungumzwa hapa ni pamoja na yaliyokuwa yanaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hii.

Haya yalikuwa ni pamoja na watu weusi kulipishwa kodi ya kichwa (poll tax), kufanywa vijakazi (serfs) katika ardhi ya mama zao, Wazungu kupewa hati za ardhi na majengo wakatambulika kisheria (title deeds/collateral) – zilizowawezesha kukopesheka benki – maghorofa ya Upanga waliishi Wazungu wachache na Wahindi.

Wakazi ya Upanga, Oysterbay, Masaki, Msasani walikuwa wakijengewa lami, huku Manzese, Buruguni na kwingineko wakiambulia vumbi. Hali si tofauti na mikoani. Taifa lilitengwa katika maeneo ya Uzunguni na Uswahilini. Uzunguni maji yalikuwa yakitoka kwenye mabomba saa 24, huku Uswahili wakihemea maji kama digidigi usiku wa manane.

Nafasi za uongozi zilikuwa za Wazungu na Wahindi au watoto wa machifu waliokuwa wakijipendekeza kwa Wazungu. Mwafrika alipaswa kusujudu mbele ya Mzungu, bila kujali umri, rika au haiba. Kuhusu elimu walikuwa na shule zao, akina siye kajamba nani tulikuwa na shule zetu za kutuandaa kuwa makarani kwa utaratibu wa 3Rs; reading, writing and arithmetic (kusoma, kuandika na kuhesabu). Shule za aina ‘Kayumba’.

Hospitalini matibabu zilikuwapo za Wazungu kama Agha Khan, huku akina siye tukienda kwa ‘Babu Loliondo kupata kikombe’. Mahakama zilikuwapo za wazawa (Native Courts), ambazo hata Mzungu angekuchapa kibao hazikuwa na mamlaka ya kumshitaki, lakini wao walikuwa wakishitakiwa katika Mahakama za Wilaya na wanachagua sheria wanayotaka itumike.

Leo matajiri wamechukua nafasi ya Mzungu. Wakifika mahakamani wana haki zaidi ya akina siye pangu pakavu.  Waafrika walikuwa watumwa ndani ya nchi yako na Wazungu walikuwa wakiwamiliki kama bidhaa.

Inawezekana hujui mpendwa msomaji, mababu zetu wakati wameshikwa utumwa, ilikuwa ni halali kwa mmiliki wa mtumwa kumpiga risasi akamuua mtumwa, na hakukuwapo mahala pa kumshitaki. Polisi alikuwa na mamlaka ya kukukamata muda wowote bila kutoa sababu na ukawekwa ndani kwa kipindi chochote bila kujua hatima yako.

Ilitarajiwa kuwa Serikali ya wazawa ikiingia madarakani, basi walau angalau Waafrika wangenukia waridi. Hali haikuwa hivyo. Mwalimu Julius Nyerere alijitahidi. Alianzisha mashirika ya umma, akataifisha mali zilizokuwa mikononi mwa ‘wezi wa mali ya umma’, na akajitahidi kusambaza umeme mijini na vijijini ili angalau watu waone matunda ya Uhuru.

Sitanii, yote aliyoyatenda Mwalimu Nyerere yalianza kufumuliwa ndani ya Awamu ya Pili. Tulianza na kubinafsisha mashirika ya umma mwaka 1987, bila kukumbuka chimbuko la kuyataifisha mwaka 1967. Tukaruhusu biashara huria, lakini kwa mtindo wa holela. Siasa zikaondoka kuwa za kuwatumikia wananchi, ikabaki wanachama kusuguana ndani ya chama kutamani nani awe Rais, lakini hawaelezi wakishinda wataifanyia nini nchi yetu.

Chama tawala kimefika mahala kimeacha kabisa kutekeleza majukumu ya msingi kiliyoomba na kuahidi kwa wananchi. Katika kampeni za Oktoba 2010 tuliahidiwa reli mpya yenye ‘geji’ ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Tabora na hatimaye Ngara, Rwanda na Burundi.

Ziwa Victoria tuliahidiwa meli mpya, Ziwa Tanganyika na Nyasa nako tukaahidiwa meli mpya pia. Tuliahidiwa barabara za madaraja ya juu (flyovers) kwa Dar es Salaam. Barabara alizopanua William Lukuvi kwa sasa zimefungwa.

Huduma ya maji ndiyo tuliyoambiwa tatizo hili litakuwa historia. Mwaka 2000 mzee Benjamin Mkapa aliahidi kuwa kila Mtanzania atapata maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka nyumbani kwake, hadi leo haijatekelezeka.

Umeme tangu mwaka 2006 tunazungumza Richmond na Dowans, lakini hadi sasa kampuni hizo hazipo, ila na umeme nao haupo. Hatutangaziwi mgawo rasmi, ila maumivu tunayapata. Tuliahidiwa zahanati na kituo cha afya kila kata, leo kiko wapi?

Leo imegeuka sera ya CCM kubatizana majina kama wanasiasa. Walianza kuitana mafisadi, mara wakabadili msimamo wakaitana magamba. Mafisadi na magamba hayo hayo, ndiyo wanayoyasimamisha majukwaani kukombeana kura CCM. Mara wakabadili msimamo kidogo na kusema CCM si chama cha mafisadi, bali kuna watu wachache. Wananchi walikwishashika kauli ya mwanzo, kwamba CCM ni Chama Cha Mafisadi. Harakati zozote za kubadili hilo zinahitaji kuthibitisha vinginevyo.

Sitanii, taarifa nimezipata. Huko Arumeru Mashariki yapo mambo ya msingi yaliyoipa ushindi Chadema. Tangu mwanzo nilizungumza kuwa si vyema vyama vya siasa kwenda kwenye kampeni kujadili watu. Amekwenda Mzee Mkapa akaanza kujadili familia ya Nyerere badala ya kuwaeleza wananchi kwa nini mashamba aliyobatilisha akiwa Rais wa nchi hii mwaka 1999 hadi leo hayajawafikia wananchi?

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, yeye badala ya kuhubiri CCM wakishinda watawafanyia nini wananchi, amekwenda Arumeru Mashariki kuwamwagia upupu akina Dr. Wilbrod Slaa na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema.

Shida ya wana-Arumeru si matusi, ni ardhi na maji. Wala wana-Arumeru hawakuwa na haja na midundo ya ngoma za Komba, bali kuelezwa maji yamekosekanaje na mpango wa kuyaleta ni upi. Suala la ubunge kuwa cheo cha kifalme nalo lilijadiliwa!

Sitanii, leo karata hizi mbili – ardhi na maji – zilizotumika kuikaanga CCM huko Arumeru Mashariki, hakika zitaikaanga zaidi mwaka 2015. Wahindi na Wazungu wanaoishi Masaki, Oysterbay na Msasani – wote wamepewa hati za kumiliki ardhi na majengo yaliyopo juu yake. Viongozi na watoto wa viongozi wengi wanazo hati za nyumba, hivyo wanakopesheka benki. Sisi tunaambiwa mikakati inaendelea!

Akina siye, ambao tumeokoteza na kujenga vibanda vyetu kwa njia ya kupika maandazi na vitumbua, hatutambuliki. Katika hili najiuliza, hivi ni uzembe wa aina gani kwamba tangu mwaka 2004, Serikali imechora ramani na ikatangaza kubatilisha matumizi ya ardhi kwa eneo kama Kitunda, Dar es Salaam, lakini hadi leo tunadaiwa kuishi kwenye kiwanja cha mtu?

Waliobahatika wamepewa hati za makazi, lakini wengine ndiyo tumesuswa. Hivi akija mtu akasema atahakikisha tunapata hati za viwanja na majengo yetu hata kama ni Mrema unadhani hatutampigia kura?

CCM nyie fikirini Watanzania wanatania, mtakiona cha mtema kuni mwaka 2015. Kwa sasa hatuhitaji longolongo. Hatuhitaji mgombea ubunge, udiwani au urais asiyetueleza bayana akichaguliwa atatufanyia nini kama taifa. Tumezichoka ahadi za nitatekeleza sera ya chama. Mgombea aeleze kama anamaliza tatizo la hati za viwanja, umeme, maji, elimu au huduma za afya. Hii itatupa fursa kumbana asiyeleta umeme kama alituahidi, itatuwezesha kumdai mgombea maji na huduma za afya.

Ukiacha hayo, CCM inalo bomu jingine. Ilituahidi Watanzania tangu miaka ya 1960 kuwa elimu itakuwa bure. Hapa bure yenyewe si bure bali ni kupitia kodi zetu. Walianzisha kitu kinaitwa Skills Development Levy (SDL), lakini bado wakubwa waliosoma bure kwa kodi zetu, wenyewe wanataka watoto wetu vyuo vikuu walipie.

Hoja hapa si majibu rahisi kuwa wanafunzi wamekuwa wengi. Kama wanafunzi wamekuwa wengi ziwepo mbinu za jinsi ya kupata fedha nyingi pia. Watoto wetu kubaguliwa katika vyuo vikuu CCM ijiandae kwa kifo kitakatifu mwaka 2015. Tulipigania Uhuru kumwondoa Mkoloni madarakani, hivyo si matarajio wala utashi wetu kuona Ikulu anakaa mkoloni mweusi anayetupa ahadi hewa.

CCM bado mnayo nafasi ya kutekeleza yale mliyoahidi ili muweze kupata kisemeo. Mkiona ushauri huu hauwafai, endelezeni libeneke lenu la kuvuana magamba. Hakika mnachofanya kama chama mnachekea nyani wachache ndani ya chama chenu, mwisho wa siku mtavuna mabua.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu simamia amani yetu. Hongera Chadema, hongera Nassari. Moto ulioanzia Arumeru Mashariki sitashangaa ukiishia Ikulu mwaka 2015.

[email protected] au 0784404827