Mara zote Watanzania wamejitambulisha kama wakomavu wa siasa, ukomavu usioeleweka namna ulivyo kama nitakavyoonesha hapa chini. Ikumbukwe kwamba mara baada ya Tanganyika (Tanzania Bara) kujitawala kabla ya kuungana na Visiwa vya Zanzibar, iliamriwa kwamba ni bora nchi ikafuata udikteta wa chama kimoja cha siasa, na hivyo huo kuwa mwisho wa mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa. Tanganyika ikabakia na chama kimoja cha siasa – Tanganyika African National Union (TANU).
Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar kule nako demokrasia ikafutika, ukabaki uimla wa chama kimoja cha Afro-Shirazi Party (ASP). Yeyote aliyetaka kwenda kinyume cha uimla huo yaliyompata yamebaki kwenye historia, kila mfuatiliaji analijua hilo.
Kwa hiyo, kwenye Muungano wa Tanzania vikawa vyama viwili tu vya siasa – TANU na ASP – ambavyo lakini vilikuwa havivuki bahari, kama ilivyo reli, ili kwenda sambamba na neno muungano wa nchi mbili. TANU ikabaki Bara tu wakati Visiwani kikitamba chama cha ASP peke yake.
Wakomavu wa kisiasa wa Tanzania wakauzoea uimla huo wakiuchukulia kama mfumo sahihi wa kuendesha maisha ya nchi! Ni mfumo uliokuwa wa aina yake duniani kote, mfumo ambao haukumpatia mwananchi uamuzi mwingine nje ya matakwa ya vyama hivyo viwili, lakini Watanzania wakijiona wao ni wakomavu wa siasa! Maajabu.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990 ndipo lilipokuja shinikizo kubwa la kimataifa kutoka kwa nchi wahisani, baada ya nchi hizo kuchoshwa na utoaji wa misaada kwa nchi zisizokuwa na mifumo ya kidemokrasia, ambapo misaada iliyokuwa ikitolewa kwa nchi husika ili kuzinufaisha nchi hizo na watu wake haikutakiwa kuhojiwa na waliopaswa kunufaika nayo yaani wananchi.
Kwa hiyo, watoa misaada wakaona kwamba ili misaada hiyo ihojiwe ni lazima pawepo na demokrasia ambayo isingewezekana ndani ya uimla wa chama kimoja cha kisiasa.
Ikaitishwa kura ya maoni kwa imani kwamba wananchi walio wengi wangesema wanahitaji vyama vingi vya siasa. Kilichosahaulika ni kwamba watu waliodumu kwenye giza kwa muda mrefu wakiuona mwanga macho yanauma, na hivyo kutamani kuendelea kuishi kwenye giza.
Kura ya maoni ilionesha kwamba asilimia 80 ya Watanzania wanatamani kuendelea na chama kimoja cha siasa, wakati asilimia 20 ya Watanzania ndiyo waliokuwa wakiutamani mwanga wa vyama vingi vya siasa.
Tanzania ikalazimika kuingia tena kwenye mfumo wa demokraisa ya vyama vingi vya siasa wakati wananchi walio wengi walikuwa hawavitaki! Hilo ni shinikizo ambalo halikuweza kukwepeka.
Sababu kama wachache ndio wanaoogopwa kupuuzwa, walio wengi tunawezaje kuamini kwamba hapo hakuna shinikizo? Tunawezaje kudai kwamba kilichoamuriwa kinatokana na matakwa yetu wakati walio wengi tumekikataa? Lakini bado tunaamini kwamba sisi ni wakomavu wa siasa! Maajabu.
Baada ya kuyaangalia maajabu hayo sasa tuyageukie maajabu mengine ndani ya ukomavu huu wa siasa wa Watanzania.
Pamoja na ukweli wa kwamba mabadiliko ya kisiasa ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi na watu wake tukiwa tumeziangalia zile nchi tunazozitembezea bakuli, inatubidi tuutumie tunaouita ukomavu wetu kisiasa kulielewa hilo na kulikubali. Mbali na hilo tutazidi kuongelea kwenye dimbwi la maajabu ninayoyasema hapa.
Sababu, mafanikio kama ya Marekani sidhani kama waliyapata kwa vile wana tundu kutoka mbinguni kwa Mungu kuelekea kwenye nchi yao, hapana, yanatokana na uongozi bora wa nchi yao unaotokana na mabadiliko ya kisiasa, basi.
Kwa hiyo, ni wazi kwamba tunapoyagomea mabadiliko ya kisiasa nchini mwetu moja kwa moja tunakuwa tumeyagomea mafanikio katika maendeleo yetu.
Maajabu yanakuwa kwamba wagomaji wakubwa wa mabadiliko ya kisiasa nchini Tanzania ni wananchi wa maeneo yaliyo gizani, kwa maana ya vijijini na maporini. Nimeyaona hayo kutokana na kuyatembelea maeneo ya aina hiyo ambapo kwa sasa niko mkoani Kagera nikiendelea kulitazama tatizo hilo. Nimetembelea Kijiji cha Kamuli, Kata ya Rubale wilayani Bukoba Vijijini, Kagera. Ukiliangalia eneo hilo utaona kwamba liko nyuma kimaendeleo kwa zaidi ya miaka 50 likilinganishwa na maendeleo yaliyoko kwenye maeneo mengine ya nchi.
Lakini jambo la kushangaza ni kwamba wakazi wa eneo hilo hawataki kusikia kitu kingine zaidi ya CCM! Pamoja na ukweli kwamba chama hicho tawala kimewahujumu wananchi hao kwa kiasi hicho, kuwatenga kimaendeleo na kuwafanya wawe nyuma kiasi kikubwa namna hiyo, bado wao wanaona hicho ndicho chama kinachowafaa, maajabu ya dunia!
Katika Tanzania hakuna sehemu iliyo na maendeleo kama yaliyo Jijini Dar es Salaam, mambo yote ya ulimwengu wa kisasa huanzia Dar es salaam kabla ya kuenea katika maeneo mengine hapa nchini, na yapo mambo mengine ambayo sidhani kama yataweza kwenda nje ya jiji hilo. Lakini ni eneo hilo linaloyatamani mabadiliko ya kisiasa kuliko sehemu yote nyingine hapa nchini!
Pamoja na Dar, maeneo yote ya mijini yakiongozwa na miji ya Arusha na Mbeya yanaonekana jinsi yalivyo mstari wa mbele katika kuyataka mabadiliko ya kisiasa, tofauti na yalivyo maeneo ya vijijini ambako ndiko uliko umuhimu zaidi wa maendeleo kwa wakati huu.
Miji kama Bukoba, Tanga, Mtwara na mingineyo inaonekana jinsi ilivyodhamiria bila unafiki wowote kuiona Tanzania inaingia kwenye mabadiliko ya kisiasa na kusonga mbele kimaendeleo kwa kuyatumia mabadiliko hayo.
Ni kwamba mtaji mkubwa wa mahafidhina wasiotaka mabadiliko ya kisiasa umebaki katika maeneo ya vijijini kulikosahaulika kimaendeleo, maeneo ambako taa za barabarani, barabara za lami mpaka kwenye vichochoro, maji yanayotiririka ndani ya majumba, barabara zilizopambwa kwa maua na kadhalika ni vitu vilivyo kama miujiza, huko ndiko wananchi wasikotaka mabadiliko ya kisiasa! Kama hayo siyo maajabu ni kitu gani?
Kwa maana hiyo ukomavu wa kisiasa wanaotamba nao Watanzania unatakiwa kufanyiwa utafiti ili kuona kama ni ukomavu wa kawaida unaofahamika kwa maana halisi, usijekuwa ni udumavu wa kisiasa unaotazamwa kwa namna tofauti!