Wiki iliyopita, makala hii iliishia pale Marcus Aurelius anaandika: “Kwa sababu jambo linaonekana ni gumu kwako, usifikiri kwa wengine haliwezekani.” Huwezi ukashinda kama huchezi.
Neno ‘Haliwezekani’ tulitumie kwa uangalifu mkubwa. Padri Dk. Faustin Kamugisha anaandika: “Kama kila mtu angejitahidi kufanya lolote zuri, dunia ingekuwa mahali pazuri pa kukalika.”
“Ushindwe wakati umejaribu.” Ni methali ya Tanzania. Methali ya Sierra Leone inasema: “Usipojaribu hautafanikiwa. Kutojaribu au kutofanya lolote ni zaidi ya kosa, ni dhambi. Kujaribu na kushindwa si uvivu.”
Usikubali kuishi duniani bila kufahamu mwelekeo wa maisha yako. F. Buscagalia (1924-1998) anasema: “Mtu ambaye hajiweki katika hali ya hatari, hafanyi lolote, hana lolote na si chochote na atakuwa si chochote. Aanaweza kukwepa huzuni na mateso lakini hawezi kujifunza na kuhisi na kubadilika na kukua na kupenda na kuishi.”
Binadamu ni kiumbe aliyepewa upendeleo wa aina yake katika uumbaji. Kiumbe huyu ana uwezo wa kujenga au kubomoa, ana uwezo wa kufikiri, kutenda na kuamua, ana uwezo wa kubadili kile anachokiona na ana uwezo wa kutawala viumbe wengine – kutaja machache.
Sifa nyingine ya binadamu ni Kubadilika. Binadamu si kama gogo ambalo linaweza kukaa miaka mingi kwenye maji lakini lisibadilike hata siku moja na kuwa mamba. Binadamu anabadilika na anabadili. Na yote katika yote ni kwamba mwanadamu amepewa upendeleo wa aina yake, wa kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni zawadi. Mfumo wa dunia umebadilika. Dunia inawahitaji watu wenye fikra pevu na pana. Katika maisha mtu akifanya jambo lilelile kila siku, tena kwa njia ileile, na kutarajia kupata matokeo tofauti au mapya, hii inakuwa ishara mojawapo ya upungufu wa akili, uendawazimu au udumavu wa fikra.
Tukubali kubadilika. Kuna methali ya Hausa isemayo: “Muziki ukibadilika na dansi inabadilika.” Katika maisha mabadiliko yanapotokea, huibuka makundi matatu ya watu. Wapo wale wanaokubali mabadiliko, ‘mabadiliko huwatunza’.
Wapo wanaoyakataa, lakini wanataka wabaki kwenye mfumo, ‘Mabadiliko huwaondoa’. Wapo ambao hawajui nini kinaendelea, ‘Mabadiliko huwashangaa’. Tukubali kubadilika penye sababu ya kubadilika. Ningependa kuwahamasisha Watanzania wote kuuchukia umaskini. Umaskini unafedhehesha.
Umaskini unadhalilisha. Deepa Narayan, alimnukuu maskini mmoja katika utafiti wake alioufanya katika nchi 50 duniani na kuuchapisha katika kitabu chake kiitwacho: ‘Voices of the poor: Can anyone hear Us?”
Anasema: “Kwa mtu maskini kila kitu kwake ni balaa. Maskini ni kama takataka ambayo kila mtu anaikimbia, maskini huambulia kudhalilishwa, kutukanwa na kubaguliwa pale anapohitaji msaada.”
Lisilowezekana linawezekana. Bilionea wa Afrika, Aliko Dangote anasema: “Mtu asiye na malengo hana sababu ya kuishi.” Thomas Carlyle anaandika: “Mtu asiye na lengo ni kama meli bila usukani -mtu aliyepotea, mtu kabwela, mtu bure.”
Jambo baya kuliko yote si kifo, lakini ni kuishi maisha yasiyo na malengo. Katika maisha ni lazima uwe na uwezo wa kumwona sungura na kobe kwa wakati mmoja. Usione kwa sababu una macho ya kukuwezesha kuona. Lione jambo moja katika taswira au sura tofauti tofauti.
Steve Jobs anasema: “Kuna wakati maisha yanakupiga kichwani kwa tofali: Usipoteze matumaini.” Mwanafalsafa wa Denmark, Soren Kierkegaard (1813 – 1855) anasema: “Maisha si tatizo ambalo linahitaji kutatuliwa, bali ni uhalisia unaopitia.”
Francois-Marie Arouet, mwanafalsafa wa Ufaransa anasema: ‘Mwenyezi Mungu alitupatia zawadi ya maisha, hivyo ni juu yetu kujipatia zawadi ya kuishi maisha mema.”
Jeffrey Gitomer alipata kuandika hivi: “Vipingamizi haviwezi kukusimamisha. Matatizo hayawezi kukusimamisha. Watu walio wengi hawawezi kukusimamisha. Ni wewe peke yako unaweza kujisimamisha.” Uwe na tafakuri njema.