Wewe ni dereva? Umewahi kuendesha gari lako binafsi au pikipiki kwenye barabara ya mwendokasi? Sasa Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam limeanza kufanya operesheni ya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wote wanaokiuka taratibu.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amesema operesheni hiyo imeanzishwa kutokana na ukiukwaji mkubwa wa matumizi ya barabara hiyo unaofanywa na madereva wasioheshimu wala kuzingatia sheria.
Mapema Rais Magufuli aliagiza kuwa wanaovunja sheria na kupitisha magari kwenye barabara ya mwendokasi wakamatwe na kupelekwa kwenye vituo vya polisi ama kung’oa matairi kwenye magari yao ili liwe fundisho kwao na kwa wengine.
Akieleza utekelezaji wa agizo hilo, Kamanda Mambosasa amesema hadi sasa idadi ya magari yaliyokamatwa yakipita kwenye barabara hiyo ni kubwa.
“Zoezi hili ni endelevu, na tutaendelea kuwakamata, kwa sababu madereva tunaona hawakomi kupita kwenye hiyo njia.
“Hatutaangalia kama hili ni gari la serikali au la mtu binafsi, magari yote tutayakamata na tutawafikisha polisi wahusika na wakakabiliane na kesi,” amesema Mambosasa.
Amesema tabia hiyo ya madereva kupita katika barabara ya mwendokasi inaleta kero na usumbufu kwa magari ya mwendokasi muda mwingine kusababisha ajali.
Ili kuepuka kadhia hiyo, Mambosasa amesema Jeshi la Polisi kupitia askari wake wa usalama barabarani wamejipanga kutekeleza kwa vitendo kauli ya Rais Magufuli.
“Tunazidi kusisitiza kuwa magari ambayo si ya mwendokasi hayaruhusiwi kupita kwenye barabara ya mwendokasi.
“Yawe ya serikali au ya raia, hayaruhusiwi, labda tu magari ya kubeba wagonjwa, nayo likiwa na mgonjwa na kama halina haliruhusiwi,” amesema Mambosasa.
Kwa upande wa magari ya serikali, amesema yataruhusiwa kupita katika barabara hiyo endapo kutakuwa na msafara na lazima njia nyingine ziwe zimefungwa na hakuna uwezekano wa kupita.
“Waliokamatwa tunawaandalia jalada ili tuwapeleke mahakamani, kule kesi zao zitasomwa na kutolewa hukumu,” amesema Mambosasa.
Mkurugenzi wa Usafiri wa mabasi yaendayo haraka (UDART), John Nguya, amesema vitendo vya magari ya watu binafsi kupita kwenye barabara ya mwendokasi vinaharibu taswira ya mradi wa mabasi hayo.
Amesema kwamba magari yanayoitumia barabara hiyo wakati hayaruhusiwi yanaua mategemeo ya nchi.
Ili kudhibiti vitendo hivyo ameshauri serikali itunge sheria itakayolinda barabara ya mwendokasi tofauti na hali ilivyo sasa, ambapo sheria zinazotumika ni zile za barabara za kawaida.
“Itungwe sheria kali ambayo mtu akikamatwa anapita kwenye barabara ya mwendokasi akipewa adhabu hataweza kupita tena.
“Sheria hii ikitungwa ni vema ibainishe ni vyombo gani vinatakiwa kupita kwenye barabara yetu,” amesema Nguya.
Naye Ofisa Usafirishaji wa UDART, Haji Maywaywa, amesema mradi umekua lakini ni mpya kwa watumiaji, hivyo askari wa usalama barabarani wanatakiwa kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji.
“Utakuta watembea kwa miguu wanashindwa kupita sehemu husika wanakwenda kupita sehemu ambayo hairuhusu mtembea kwa miguu,” amesema Maywaywa.
Dereva wa magari hayo, Caroline Ngoda, amesema zipo changamoto kadhaa za barabara ya mwendokasi ikiwemo ya magari ya kawaida kukatisha maeneo ambayo hayaruhusu gari kukata kona.
Kutokana na hali hiyo, amesema hujikuta wakishindwa kufanya kazi kwa ufanisi, hivyo kushindwa kutimiza malengo ya UDART.