Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tunaweza kujifanya hatuoni wala hatusikii. Tunaweza kujifanya yanayotokea na kuwapata Watanzania wenzetu ni yao wao, si yetu!

Tunaweza, kwa upofu na utamu wa madaraka, tukadhani kuwa sisi ni chama tawala, na kwamba tutakuwa kwenye hizi nafasi kwa miaka yote.

Hupaswi kuwa mfuasi wa chama cha upinzani ndipo utambue kuwa kinachofanywa na vyombo va dola dhidi ya wafuasi wa vyama vya upinzani, hasa CHADEMA ni uonevu ambao mwisho wake si mwema. Hiki kinachoendelea ni mbegu; na kwa kawaida si mbegu zote ambazo huchipua haraka! Tena basi, wana CCM wa kweli na mapenzi mema, wenye kutambua kuwa kwao Tanzania ni nambari wani na CCM ni ya pili, wanaumia mioyoni kuona damu za Watanzania wasiokuwa japo na manati zikimwagika na wengine kutiwa vilema vya maisha kwa uonevu tu.

Bahati mbaya kuna dhana mbovu ya kuwaona wanaojitokeza kuyasema haya kuwa ni ‘wapinzani’, au wanataka kumkwamisha rais, au wana chuki, na mambo mengine yasiyo na maana kama hayo.  

Sikutarajia kwa nchi yetu kuona leo polisi – vijana wa Tanzania waliozaliwa na kusomeshwa kwa fedha za makabwela wa nchi hii wakishiriki kuwakamata na kuwatia vilema Watanzania wenzao eti kwa kosa la kwenda kusikiliza kesi ya kiongozi wao! Kupiga raia katika nchi hii imekuwa fasheni ya vyombo vya dola. Watu wazima wenye akili hawawezi kufurahia haya kwa kigezo kuwa wanaopigwa ni wapinzani, au wakaidi.

Matumizi ya watu, mbwa, farasi, magari, na mitambo kukabiliana na watu ambao mikononi hawana hata chupa ya maji ni matumizi mabaya ya rasilimali za nchi. Fedha zinazotumika kuandaa na kuutekeleza uchuro wa ‘vurugu’ ni nyingi na zinapotea bure. Huu ni uchuro kwa sababu sijawahi kuona, wala hakuna historia ya Watanzania kukusanyika mahali na kufanya vurugu za kisiasa.

Mgeni yeyote aliyezuru Tanzania akapita Kisutu juzi, au aliyetazama televisheni akaona mavazi na hekaheka za polisi asingekubali kuwa hii ndiyo ile Tanzania iliyojengwa na watu makini – waliokuwa na kiu ya kuona Watanzania na Waafrika wakiishi kwa uhuru, upendo, mshikamano na kwa misingi ya haki.

Ndani ya CCM, ndani ya serikali na katika jamii, wapo wengi wasiofurahishwa na maguvu yanayotumiwa na polisi kuwatia vilema vya kudumu Watanzania wenzetu. Haya yote wanayaona, yanawaumiza, lakini wameamua wakae kimya ili wasitibue ‘maisha yao’. Tumeamua kuwa taifa la ma-opportunists bila kujali au kuwa na huruma kwa wanaoumizwa na kwa nchi yetu. Leo televisheni kubwa duniani zinatangaza mabaya ya Tanzania.

Tumeamua kujifanyia ‘censorships’ sisi wenyewe kwa kujiaminisha kuwa kwa kukosoa tutamuudhi rais na watawala wengine. Wengine, hasa mwaka huu wa uchaguzi tunaogopa kusema kwa kuhofu tutachukiwa au kuondolewa kwenye orodha. Hii ni dhana mbaya, hasa tukizingatia kuwa Katibu Mkuu wa CCM Dk. Nchimbi, juzi amewapiga kufuri wana CCM wanaoimba nyimbo mbaya dhidi ya Watanzania wenzao wanaotofautiana kiitikadi. Dk. Nchimbi kwake Tanzania ni muhimu sana kuliko ushabiki wa vyama! Huu ndio uongozi unaotakiwa.    

Dhambi hii ya unafiki wa kukaa kimya ilisemwa na Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1962 kwenye kijitabu chake cha TUJISAHIHISHE: “Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana.” Haya ni maneno ya Mwalimu. Naam! Tunaogopa kumweleza Rais ukweli wa huku mitaani ili tusichukiwe – tukakosa nafasi! Hapa ile ahadi ya “Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko”, kivitendo imeshafutwa na wanachama.

Mwana falsafa Machiavelli katika kitabu chake maarufu cha ‘The Prince’ anasema kwamba: “Lazima kiongozi awe tayari kutumia udhalimu ili kudumisha utawala wake na ili kuhakikisha amani na usalama wa taifa.” Kuna dalili zote kuwa polisi wetu wanaamini nadharia hii ya maguvu na kutesa watu kama njia ya kuufanya utawala uendelee kuwa madarakani! Wanaojua hawataki kumkumbusha Rais Samia maneno yake kuwa hataki kuongoza nchi inayotiririka machozi!

Mwanafalsafa Jean-Jacques Rousseau, anapingana na Machiavelli hasa kupitia mtazamo wake kuhusu mkataba wa kijamii katika kitabu chake maarufu ‘The Social Contract’ (1762).

Rousseau anaeleza kwamba utawala wa haki na usawa ndio unaopaswa kuwa msingi wa mamlaka ya kisiasa, na anakataa kabisa wazo la kutumia udhalimu kama njia ya kudumisha utawala.

Aliona kwamba mamlaka halali ya serikali inatokana na makubaliano ya kijamii ambako wananchi wanakubali kujiunga na kujitolea kwa pamoja kwa manufaa ya wote, kwa kuzingatia haki na usawa. Rousseau anasisitiza kwamba kiongozi au serikali inapaswa kutenda kwa niaba ya watu, na hiyo inahitaji utawala unaohusisha demokrasia na haki za kiraia.

Jeshi la Polisi linajidanganya kudhani kuwa nadharia ya Machiavelli inaweza kuwa hirizi ya kuifanya serikali wanayoipenda kwa zama hizi iendelee kuwa madarakani milele. Kinyume chake, wanachofanya ni kuongeza hasira na visasi kwa wananchi wa sasa na hao wanaozaliwa kila leo. Fikiria mtoto ambaye anakua akiona baba yake hatembei kwa sababu alivunjwa nyonga kwa ‘kosa’ la kwenda kusikiliza kesi ya mwenyekiti wake!

Ingawa tumeshuhudia mifano mingi ya utawala wa mabavu duniani, hakuna utawala uliodumu milele. Haupo. Utawala wa mabavu unaweza kudumu kwa miongo mingi, lakini huwa na mwisho wake, kwa sababu ya mabadiliko ya kijamii, kisiasa, au namna nyingine. Mabadiliko ya kijamii hayaji yenyewe, bali huwa yanaandaliwa – na kwa bahati nzuri au mbaya Tanzania mabadiliko haya yanaandaliwa na watawala wenyewe kwa msaada wa vyombo vya dola.

Upepo wa mabadiliko, nguvu za raia, au shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa mara nyingi husababisha mwisho wa utawala unaolindwa na mapolisi kwa maguvu na kwa ukosefu wa huruma.

Kila nikirejea kupigwa kwa wale wananchi Kisutu, na nje kabisa ya Kisutu, nashindwa kuelewa kitu gani au upepo gani unaikumba Tanzania! Tukio hilo limewafanya baadhi ya wana historia waibue picha za video za kesi ya uhaini ya miaka ya 1970. Picha zile zinawaonyesha mamia kwa maelfu ya wananchi wakiwa mahakamani kusikiliza kesi nzito ya watu waliotaka, si tu kupindua, bali kumuua Rais. Mbona haki hii iliheshimiwa miaka hiyo, leo kwa nini izuiwe? Hata kama ni kuzuia, kulikuwa na sababu gani kutumia mbwa kuwang’ata watu ambao wana mapenzi ya kuona kiongozi wao anavyoshitakiwa? Hii ndiyo ile dhana ya kwamba anayepigwa, anapigwa, na ananyimwa hata haki ya kulia!

Mambo mengine yanayoendelea unaweza kujiuliza, wote walioshika nafasi mbalimbali wanamtakia mema Rais Samia? Huku mitaani wengi wanadhani kuna ajenda ya kumfitinisha Rais na wananchi wake kutokana na dhuluma hizi wanazofanyiwa wafuasi wa vyama vingine vya siasa.

Lakini hao hao wanakwenda mbali zaidi na kuhoji, kama Rais hapandezwi na haya yanayoendelea, mbona yeye mwenyewe yuko kimya? Ameridhika kuona raia wake wakivunjwa mikono, miguu na nyonga bila hatia? Kwa nini basi, asimwagize hata waziri wake mmoja akemee hii piga-piga iliyohalalishwa?

Ndugu zangu, tunaweza kujifanya hatuyaoni haya yanayoendelea sasa, lakini tujue ipo siku yataonekana – hata kama si duniani, basi kwa Mungu.

Amani ya nchi ni matokeo ya haki katika nchi. Tunajidanganya na kumdhihaki Mwenyezi Mungu kwa kuhimizana kuombea amani ilhali nje ya sala kuna wababe ambao kazi yao ni kupiga na kuumiza Watanzania wenzao. Haiwezekani watawala wakiwa majukwaani wawe wanahimiza amani, lakini pembeni viongozi wa dola wanaandaa orodha ya nani wapigwe na hata kujeruhiwa. Matumizi ya virungu kulinda dola ni kuishiwa maarifa kwa watawala ambao wanadhani hoja zinazimwa kwa maguvu badala ya hoja.

Tanzania inakuwa nchi ya amani endapo sote – bila kujali itikadi zetu au nafasi zetu katika jamii – tutaamua kuishi kwa haki na usawa. Tuione Tanzania ni nchi yetu sote, na kwamba leo CCM wako madarakani, lakini wakati mwingine wanaweza kuwa wengine – hakuna kisichobadilika, ila mabadiliko tu. Tuwe kwa mfano wa mataifa makubwa ambako unaona safari hii chama fulani kinaongoza, safari nyingine chama kingine kikiingia madarakani. Wanafanya hivyo kwa sababu uwanja wao wa ushindani ni tambarare. Tusiweke mazingira ya kulipizana visasi.

Hata hivyo, hayo yote hayatawezekana kama tutaendelea kuishi kiuadui. Tunao wajibu wa kujenga misingi na uwanja sawa wa kuendesha nchi yetu ili kwamba hata anayetolewa madarakani akiwa mpinzani, asijute. Tusisahau kule Zambia yupo kiongozi aliyejenga mazingira mabovu ya gereza ili amweke mtangulizi wake, lakini baadaye akajikuta naye akiingizwa humo humo.

Katika nchi yetu, haki iwe ni nguzo ya ustawi wa jamii na maendeleo endelevu. Linapokuja suala la kutendewa haki, hakuna mtu anayepaswa kupuuzwa au kudhulumiwa kwa sababu ya imani zake za kisiasa, kidini, au kiitikadi. Hali ya baadhi ya wafuasi wa CHADEMA, na hata raia wengine, kunyanyaswa na vyombo vya dola inapaswa kuwa ni jambo lisilokubalika katika jamii yetu. Hakuna haki ya kisheria inayoweza kutetea vitendo vya vurugu, mateso na dhuluma kwa watu ambao hawana hatia yoyote, ila kuwa na imani tofauti na walio madarakani.

Tanzania ni nchi yetu sote, na kila mmoja wetu anastahili kuhisi kuwa ni sehemu ya taifa hili, akiwa na uhuru wa kuishi, kujieleza, na kushiriki katika masuala ya kijamii na kisiasa bila hofu ya kuonewa. Haki ya kupata usalama, huduma bora, na ulinzi inapaswa kuwa ni haki ya kila Mtanzania, bila kujali itikadi yake au ushabiki wake wa kisiasa. Dola haipaswi kuwa chombo cha kudhulumu raia wake, bali inapaswa kuwa mlinzi wa haki, usawa, na maendeleo kwa kila mmoja.

Katika muktadha huu, tuseme kwa nguvu zote kwamba haki na sheria hazitakiwi kuwa na upendeleo wala ubaguzi. Tanzania ni yetu, na kila mmoja anastahili haki sawa mbele ya sheria. Hakuna mtu anayepaswa kuvunjwa mikono, miguu, au nyonga kwa sababu ya tofauti za kisiasa. Tunapaswa kuwa na Tanzania ambayo inajivunia misingi ya haki, usawa, na amani, ambako kila mmoja anaishi kwa hofu ya Mungu na kwa utu wa binadamu.

Kwa kumalizia, tunapojenga taifa lenye misingi imara ya haki na sheria, tutakuwa na taifa la amani, umoja, na ustawi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Haki itakuwa ndiyo mwanga wa taifa letu, na watu wote wataishi kwa furaha na usalama. Tanzania iwe nyumba ya haki na amani kwa kila raia wake wote. Madaraka yana mwisho, lakini Tanzania ni ya milele. Tusikubali kuivuruga nchi yetu hii nzuri.

Mungu Ibariki Tanzania

0759 488955