*Kisa? Kumzuia mumewe asikipige kichanga cha miezi miwili
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mara
Katika tukio lisilokuwa la kawaida, mkazi wa Buchegera, Serengeti mkoani hapa, Nyaikongoro Ntumbo (28), anatuhumiwa kumpiga mkewe mdogo na kumlazimisha kula kinyesi.
Akizungumza na JAMHURI, mwathirika wa tukio hilo, Eliza Nchagwa (20) amesema limetokea Novemba 21, mwaka jana.
“Mume wangu alinipiga sana hadi nikajisaidia haja kubwa. Akachukua panga, akaniamuru nile kinyesi na nisipofanya hivyo ataniua.
“Sikuwa na cha kufanya kwa kweli, nililazimika kula hadi kumaliza. Kipigo kiliniacha na maumivu makali ya tumbo na mwili,” anasema Eliza kwa sauti ya simanzi.
Anasema usiku huo mumewe alionyesha wazi dhamira ya kumuua, kwa kuwa hakukuwapo sababu ya kumpiga kiasi kile.
“Yeye alitarajia kuwa ningekataa kula kinyesi ili anikate na panga na kutekeleza nia yake. Nikalazimika kula huku amenisimamia.
“Asubuhi akaniambia sitakiwi kutoka nyumbani kwenda kijijini kwetu au kupata tiba na msaada kwa watu wengine,” anasema Eliza.
Siku iliyofuata, Eliza alimweleza mama mkwe wake ukatili aliofanyiwa na mumewe, taarifa iliyomuacha mdomo wazi akisema hajawahi kushuhudia wala kusikia ukatili wa namna hiyo.
Anasema mama mkwe alimwita mwanaye na kumkanya asirudie tena kitendo hicho, ikizingatiwa kwamba ilikuwa ni miezi miwili tu tangu Eliza atoke kujifungua.
“Kitendo cha kugombezwa na mama yake kilimuudhi sana mume wangu, usiku huo alinipiga tena na kutishia kuniua. Kwa kweli kipigo cha siku mbili mfululizo kilinikosesha usingizi.
“Sikulala. Tumbo likawa linaniuma sana nadhani kwa sababu ya kula kinyesi. Asubuhi wakati anakwenda kuchunga (mifugo), akanikataza tena kutoka nyumbani,” anasema.
Anadai aliamua kutoroka na mwanaye kwenda kijijini kwao, Masebe, Kata ya Mbalibali.
Alipofika kwao, mama yake, baada ya kuona hali aliyokuwa nayo Eliza, alimchukua hadi kwa Mwenyekiti wa Kitongoji.
Baadaye wakapelekwa Ofisi ya Kijiji ambako viongozi walimwita mumewe aliyekiri kufanya ukatili huo na kusema kwamba hamtaki tena.
Uongozi wa kijiji uliwapa barua kwenda hospitalini kupitia Kituo cha Polisi, ambako walifungua jalada la shambulio namba 3171/2023.
Eliza amepata matibabu katika hospitali ya wilaya alikopigwa X-ray na kupasuliwa uvimbe kichwani uliosababishwa na damu kuvilia ndani.
JAMHURI limezungumza na muuguzi mmoja hospitalini hapo aliyethibitisha Eliza kupata matibabu.
“Alipewa dawa za tumbo na maumivu mengine. Hata hivyo bado hali yake haijatengemaa, hasa tumbo na maumivu,” anasema.
Kutotengemaa haraka kwa hali ya Eliza kunadaiwa kutokana na familia kutokuwa na fedha za kugharamia matibabu ya ziada.
Kwa nini kipigo hicho?
Eliza anasema chanzo cha kupigwa ni kitendo cha kumzuia mumewe kumpiga mtoto wao mchanga mwenye umri wa miezi miwili.
“Alipofika nyumbani, mtoto akawa analia. Yeye (Nyaikongoro) akaanza kumpiga makofi na kumfinya eti asimpigie kelele.
“Nikamuuliza anawezaje kumnyamazisha mtoto mchanga kwa kipigo na kumfinya? Ndipo akachachamaa, akadai najifanya mtoto ni wangu peke yangu, kwamba yeye hana sauti juu yake. Akaanza kunishambulia,” anasema.
Eliza ni mke wa pili wa Nyaikongoro na anasema amekuwa na wakati mgumu kutokana na tabia ya ulevi na ukorofi wa mume wake.
Anasema amekuwa akipigwa mara kwa mara na kusuluhishwa, lakini kipigo cha mwisho kimemwonyesha kuwa kuna uwezekano wa kuuawa.
Mama, baba wazungumza
Rebeca Nyantori, mama yake Eliza, ameliambia JAMHURI kuwa hali ya mwanaye ilikuwa mbaya sana.
“Aliponieleza alichotendewa, nililia sana. Nikamjulisha baba yake, akatupa pesa nikampeleka hospitali yeye na mjukuu wangu. Lakini hadi leo hali yake haijatengemaa, hasa tumboni,” anasema Rebecca.
Anasema tangu Eliza aliporejea nyumbani, mumewe hajakwenda kumjulia hali zaidi ya kutoa Sh 100,000 baada ya kubanwa na uongozi wa kijiji.
Baba yake Eliza, Nchagwa Wambura, anasema hadi sasa amekwisha kutumia zaidi ya Sh 300,000 kwa ajili ya matibabu ya Eliza na mwanaye.
Anasema licha ya mahari ya ng’ombe 10 alizopokea, kwa hali aliyokutana nayo Eliza, hataweza kumruhusu kurudi kwa mumewe.
“Kitakachofuata ni kifo tu. Bora waachane kuliko kuishi katika mazingira hayo. Majirani wanataka haya mambo yaishie nyumbani; kwamba sitakiwi kumfunga mkwe wangu! Siwaelewi kabisa. Angemuua wangesemaje?” anahoji Wambura.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Buchegera, Matiko Mete, anasema Eliza na mumewe wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara na kusuluhishwa.
“Pamoja na kuwasuluhisha, hili la kumlisha kinyesi chake! Limetushinda. Huu ni ukatili wa kiwango cha juu kabisa, lazima sheria ichukue mkondo wake,” anasema.
Anasema baada ya uongozi wa kijiji kumbana na kumtaka mume wa Eliza atoe Sh 100,000, Nyaikongoro alilalamika na kudai kuwa hakustahili kutoa fedha hizo.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Nyamburi Gitano, amelithibitishia JAMHURI kuwa mtuhumiwa alikiri mbele ya viongozi kumpiga Eliza na kumlazimisha kula kinyesi.
“Nilishangaa ujasiri alionao wa kusema bila hofu. Nikaagiza waende polisi kwa hatua zaidi, maana ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,” anasema Gitano.
Mtuhumiwa ajitetea, adai ni pombe
Akizungumza na JAMHURI, Nyaikongoro amekiri kumpiga mkewe hadi kujisaidia haja kubwa.
“Kwa kweli siku ile nilikuwa nimepiga maji sana kule senta (eneo la kijiji lililochangamka).
Nilipofika nyumbani, nikakuta mtoto analia. Nikauliza sababu, mama yake akadai kuwa alikuwa na siku tatu hajajisaidia. Wakati namnyamazisha, yeye akaingilia kati.
“Nilimwacha mtoto nikampiga kofi moja, kisha nikachukua fimbo nikamchapa kichwani na miguuni. Akajisaidia haja kubwa. Nikamuuliza kwa nini amefanya hivyo? Akadai ni kutokana na hofu ya kipigo. Lakini sikumlazimisha kula,” anasema.
Alipoulizwa iwapo mkewe na uongozi wa kijiji wanasema uongo kuwa alikiri mbele yao kumlazimisha mkewe kula kinyesi, alinyamaza, kisha akasema:
“Siwezi kusema kuwa viongozi ni waongo. Inawezekana nilimlazimisha kwa kuwa wakati huo nilikuwa nimelewa sana. Naomba mnisaidie haya mambo yaishe, maana yamenikalia vibaya.”
Anakiri kutokuwapo uhusiano mzuri kati yake na familia ya mkewe, akisema hawezi kwenda kuwajulia hali kwa hofu ya kufanyiwa kitu kibaya.
“Upande wa matibabu, nilichangia Sh 100,000 nikitarajia kuwa zingemtibu hadi kupona kabisa. Sikujua kama tatizo ni kubwa kiasi hiki,” amesema.
Kwa sasa Nyaikongoro anasema anatafuta watu wa kumsaidia kumwombea msamaha ukweni ili mambo yaishe, warudiane.
Mkazi wa Nyamburi ambaye pia ni Msaidizi wa Kisheria wa Shirika la Geitasamo Paralegal Organization (GEPAO), Julius Nyigesa, anasema baada ya kupata taarifa aliwatafuta wahusika wote kwa nyakati tofauti na kubaini mtuhumiwa alitenda kosa hilo; na kwamba aliomba amsaidie kumuunganisha na familia mambo yaishe.
“Ukatili wa kijinsia ni vitendo vya udhalilishaji au ubaguzi ambavyo hufanyiwa mtu kutokana na kuwa wa jinsi au jinsia tofauti. Vinasababisha madhara kimwili, kisaikolojia, kiuchumi au kiroho.
“Mimi sasa nina umri wa zaidi ya miaka 70, sijawahi kusikia mtu anapigwa, anajisaidia haja kubwa, kisha analazimishwa kula kinyesi chake mwenyewe. Nilishauri waende kwenye vyombo vya sheria,” amesema.
Siku chache baada ya JUMHURI kuanza kufuatilia tukio hilo, Polisi Wilaya ya Serengeti imesema tayari mtuhumiwa amekamatwa.
“Yuko mahabusu tangu Desemba 30, 2023 majira ya saa 5 asubuhi wakati taratibu nyingine za kumfikisha mahakamani zikiendelea,” Polisi imeliambia JAMHURI.