SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limewatahadharisha mamilioni ya watu wanaoishi katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kujihadhari na ukame unaoweza kusababisha maafa makubwa ya kibinadamu.
Nchi ambazo zimetajwa katika ripoti hiyo ni pamoja na Lesotho, Malawi, Namibia, Zambia, na Zimbabwe, ambapo mazao mengi yameharibika na mifugo imepotea.
Msemaji wa WFP Kusini mwa Afrika, Tomson Phiri, amethibitisha hali hiyo na kuongeza kuwa Angola na Msumbiji pia ziko hatarini kukumbwa na tatizo la ukame.
Phiri amesisitiza umuhimu wa nchi hizo kujiandaa kuhifadhi chakula, kwani hali hiyo huenda ikazidi kuwa mbaya ifikapo Aprili mwakani.
Taarifa zinasema kuwa ukame huo umeathiri zaidi ya watu milioni 27 katika eneo hilo, huku watoto milioni 21 wakiwa katika hatari ya utapiamlo.
Hata hivyo, WFP inaendelea kusambaza misaada ya chakula licha ya kupokea kiasi kidogo cha fedha, dola milioni 360, kusaidia mataifa yaliyokumbwa na tatizo la ukame.