Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imebaini mapungufu na hasara lukuki ambazo zimekuwa zikisababishwa changamoto za uendeshaji na hivyo kusababisha taasisi au shirika kupata hasara ikiwemo upungufu wa maji wa kati ya asilimi 10 hadi 80 ya mahitaji ya maji katika mamlaka za maji 25.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 6,2023 jijini Dodoma kuhusu taarifa ya ukaguzi kwa kipindi cha mwaka 2021/2022,Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Charles Kichere alisema,pia Mamlaka za maji 23 zilipata hasara ya shilingi bilioni 162.14 kutokana na upotevu wa maji katika mwaka 2021/22.
Vilevile asema pia katika ukaguzi wake alibaini kiwango kisichoridhisha cha ukusanyaji wa madeni katika Mamlaka za Maji 28, ambapo jumla ya madeni yasiyolipwa hadi Juni 30 , 2022 yalikuwa shilingi bilioni 127.07 ambapo Mwaka 2021 madeni yalikuwa ni shilingi bilioni 129.59.
“Aidha kulikuwa na upungufu katika utekelezaji wa miradi ya maji katika Mamlaka za Maji mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 56.27. “amesisitiza
Katika eneo hilo amesema,ukaguzi uliofanywa na ofisi yake ulibaini Mfuko wa Bima ya Afya ulikataa madai ya kiasi cha shilingi bilioni 8.84 kati ya madai yote ya shilingi bilioni 92.44 yaliyotozwa na hospitali za umma.
Kwa mujibu wa Kichere, Mfuko wa Bima ya Afya ulirekodi nakisi kabla ya kodi inayofikia shilingi bilioni 189.65 ambapo kwa 2021 ilikuwa shilingi bilioni 93.68.
Aidha amesema, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ilitoza bei kubwa zaidi kiasi cha shilingi bilioni 1.01 kwa vituo vya afya tofauti na bei zilizoidhinishwa, pia kulikuwa na ongezeko la bidhaa zilizopokelewa zikiwa zimebakiza chini ya 80% ya muda wa kuisha au miaka miwili kabla ya muda kuisha.
“ Katika Bohari Kuu ya Dawa shilingi bilioni 295.76; na utoaji wa huduma za mikopo bila mkataba halali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili shilingi bilioni 16.73.
“Pia, nilibaini mashirika mbalimbali na taasisi zingine za umma zilipitia changamoto mbalimbali katika uendeshaji uliosababisha kutofanya vizuri katika uwekezaji na uendeshaji wa biashara, hivyo kupelekea shirika au taasisi husika kupata hasara.”alisema Kichere na kuongeza kuwa
“Sababu za kupata hasara/nakisi kwa baadhi ya taasisi hizo ni kama ifuatavyo Kampuni ya Ndege ya Tanzania imekuwa ikipata hasara kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo,
“Pamoja na Serikali kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 30.63 kwa mwaka wa fedha 2021/22, kampuni bado iliripoti hasara ya shilingi bilioni 35.23,Serikali isingetoa ruzuku hiyo, kampuni ingepata hasara ya shilingi bilioni 65.86,
“Hii inaonesha changamoto ambazo Kampuni ya Ndege Tanzanaia inakabiliana nazo katika soko kwa sasa. Hivyo, Kampuni ya Ndege Tanzania itathmini upya mbinu na mikakati ya uendeshaji ili kupunguza gharama na kuongeza mapato.”
Kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ,alisema uliripoti hasara ya shilingi bilioni 204.65 kutokana na ongezeko la gharama za mafao ya matibabu na gharama za huduma kwa wanachama ambazo hazikulingana na mapato yaliyoongezeka.