Watembelea Kiwanda cha Mtanzania Aliyewekeza Nchini Thailand
Bangkok
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo mwishoni mwa wiki aliongoza Ujumbe wa Tanzania nchini Thailand kutembelea Kiwanda Earth Supply Co. Ltd kinachotengeneza Mashine zinazotumika katika shughuli za kukata, kutoboa na kunga’risha madini ya Vito.
Ziara katika kiwanda hicho ililenga kujifunza kuhusu teknolojia mbalimbali za kisasa zinazotumika katika shughuli hizo ikikumbukwa kwamba, Thailand ni miongoni mwa nchi zilizoendelea katika shughuli za uongezaji thamani madini ya vito zikihusisha utengenezaji wa bidhaa za mapambo ya vito na usonara ya thamani kubwa.
Katika ziara hiyo ilielezwa kwamba, nchi walaji wa mashine zinazotengenezwa na kiwanda hicho ni pamoja na Colombia, Uswis, Madagascar na Thailand yenyewe ambapo shughuli hizo zimeshamiri kwa kiasi kikubwa.
Aidha, ziara hiyo kiwandani hapo ni mwendelezo wa dhamira na jitihada zinazofanywa na Serikali kusimamia shughuli za uongezaji thamani madini ya vito na usonara ikiwemo kujenga na kuimarisha miundombinu ili Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kiweze kutoa mafunzo ya uongezaji thamani madini kwa ufanisi.
Vilevile, kupitia ziara hiyo wasimamizi wa kituo cha TGC na watendaji kutoka Wizarani walipata uelewa na kufahamu ujuzi unaohitajika katika uendeshaji wa viwanda vya kuchakata madini ya vito, utengenezaji na usimamizi wa tasnia ya uongezaji thamani madini kutokana na nchi ya Thailand kubobea katika eneo hilo.
Kadhalika, kwa Tanzania ziara hiyo inalenga kuongeza uelewa na ujuzi wa namna ya kuendesha viwanda hivyo ili kuwezesha utengenezaji wa bidhaa zenye ubora unaokubalika kimataifa kupitia kituo cha TGC ikiwemo usimamizi wa tasnia hiyo.
Wizara inaichukua ziara hiyo kwa uzito mkubwa kutokana na namna ilivyobarikiwa aina mbalimbali ya madini ya vito vya thamani kubwa. Inaelezwa, Tanzania ina zaidi ya aina 100 za madini ya vito yakiwemo ya thamani kubwa huku aina zinazovunwa zikiwa si zaidi ya 25 za madini hayo.
Kupitia ziara hiyo, wataalam wanapata uelewa wa namna bora ya kusimamia na kuendeleza shughuli hizo ili kuongeza tija katika sekta hiyo ikiwemo ajira kwa watanzania na kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini.
Katika hatua nyingine, ikiwa ni katika kuunga mkono juhudi za kuwaendeleza kiuchumi watanzania hususan kwa kuchangamkia fursa mbalimbali nje ya nchi, Februari 26, 2024, Naibu Katibu Mkuu Mbibo na ujumbe wake walimtembelea Mtanzania Suleiman Kilonda anayemiliki kiwanda cha kuzalisha nguo nchini humo na kujionea namna kiwanda chake kinavyofanya shughuli zake. Uwekezaji wa Malonda nchini Thailand ni mwendelezo wa Sera ya mambo ya nje katika diplomasia na uchumi.
Akizungumza kiwandani hapo baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji, Mbibo alimpongeza kwa ujasiri na uthubutu wa kufanya shughuli zake za kiuchumi nje ya Tanzania bila kujali ni jamii gani anayoihudumia.
Alitumia nafasi hiyo kumpa moyo na kumtaka kushirikiana na kuvuta watanzania wengine ili waweze kujifunza na kupata ujuzi wa kile anachokifanya.
Aidha, Mbibo alimtaka kuhakikisha anafanya shughuli zake kwa kuzingatia sheria na kuhakikisha anafuata taratibu zote za kiwekezaji nchini Thailand ili kulinda jina zuri la Tanzania, hivyo kuwafungulia milango watanzania wengine.
‘’ Nipende kukupongeza sana bwana Kilonda kwa uthubutu wako uliouonesha. basi nikutake uendelee kuzingatia na kufuata taratibu zote za usajili na usikate tamaa ili kuhakikisha ndoto zako zinakuwa kweli.’’ Lakini nipende kuchukua fursa hii kuwaasa vijana kutojifungia na kubaki sehemu moja,’’ alisema Mbibo.
Awali, Kilonda alimweleza Mbibo kuhusu mipango yake ya kuanzisha kiwanda cha nguo nchini Tanzania na kuhusu hatua mbalimbali ambazo tayari amekwishazifanya ili kufikia lengo lake.
Kilonda alitumia nafasi hiyo kuzishukuru mamlaka mbalimbali ambazo zimemwezesha kuelekea hatua ya kupata hati ya eneo ambalo amepanga kujenga kiwanda hicho eneo la Mlandizi, Mkoani Pwani.
Aidha, alimwomba Naibu Katibu Mkuu afikishe ombi lake la kuiomba Serikali kumsikiliza ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuanzisha kiwanda hicho nchini.
‘’ Nashukuru masuala ya ardhi yanakwenda vizuri natarajia mwezi huu nitapata hati ya eneo ninalotarajia kujenga kiwanda. Ombi langu naomba Serikali inisikilize. Inawezekana kuna viwanda ambavyo havijaendelezwa basi tupewe, lakini bado kuna changamoto ya kupata fedha za mtaji kwa wawekezaji wa kitanzania hayo ni miongoni mwa masuala ambayo natamani kuona yanatatuliwa ,’’ alisema Seleman
Seleman alimwonesha michoro ya kiwanda ambacho amepanga kukijenga nchini Tanzania ikihusisha kiwanda, eneo la makazi, hospitali na miundombinu mingine muhimu.