Wapendwa Taifa la Mungu,
Hii ni aya ambayo inahitimisha sura ya tano ya waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho.
Katika sura hii, Mtume Paulo ametoa maelezo mbalimbali kumhusu Kristo na mwishoni anahitimisha na kumsihi kila mmoja ajitahidi kupatanishwa na Mungu.
Mwaliko huu ni kiashirio kwamba maisha ya Mkristo lazima yaambatane na jitihada ya kutaka kupatanishwa na Baba wa mbinguni kwa sababu baada ya maisha haya tutarudi kwake (taz. 2Kor 5:10).
Mafundisho yote yanayohusu upatanisho ni kipengele muhimu katika mpango wa Mungu wa wokovu. Upatanisho ni neno ambalo binadamu hukutana nalo mara nyingi asomapo Maandiko Matakatifu na ndani ya jamii anamoishi.
Upatanisho ni sehemu ya wokovu wetu; unakuza uhusiano wetu na Mungu na pia kati yetu.
Pindi tuwapo duniani tunakumbwa na changamoto zinazosababisha tukae mbali na Mungu (2Kor 5:6) kwa kupendelea dunia na kasumba ya kujijali na kujiabudu sisi wenyewe.
Tunatumbukia katika hatari ya kuabudu mawazo mabovu ya binadamu wenzetu, kazi zetu, michezo, siasa na ushabiki na hata kuabudu familia na marafiki zetu. Kipaumbele kinakuwa kimewekwa kwa malimwengu zaidi kuliko kwa Mungu.
Hivi dhambi daima huharibu uhusiano wetu na Mungu na jirani, tunahitaji njia ya kurekebisha uharibifu huo na kurejesha uhusiano huo. Tunahitaji upatanisho. Upatanisho wa Kibiblia, basi, ni kuondolewa kwa dhambi ili kurejesha uhusiano kati yetu sisi wenyewe na Mungu.
Kwa sababu hii, Ujumbe wa mwaka huu unatuhimiza kujitahidi kupatanishwa na kumpendeza Bwana (taz. 2Kor 5:9).
Tufanye jitihada za kujiepusha na kuridhika na sifa za binadamu (taz. 2Kor 5:12) na badala yake tusifie maendeleo ya kiroho kwa kuwa tukiwa ndani ya Kristo, tunakuwa viumbe vipya (taz. 2Kor 5:17). 2
Sura ya Kwanza: Upatanisho katika maandiko matakatifu na mafundisho ya Kanisa; Agano la Kale
1. Katika Agano la Kale Mungu alitoa nafasi kwa binadamu kujipatanisha naye kwa njia ya kutolea dhabihu mnyama ili kuondoa uharibifu wa dhambi kutoka kwa watu wa Mungu.
Mungu mwenyewe katika Kitabu cha Mambo ya Walawi alieleza kwa nini ilikuwa hivyo: “Maana uhai wa kiumbe ulioko ndani ya damu; nami nimekupa wewe kufanya upatanisho kwa ajili yenu juu ya madhabahu; ni damu inayofanya upatanisho kwa maisha ya mtu.” (taz. Law 17:11).
2. Tunajua kutoka Maandiko Matakatifu kwamba mshahara wa dhambi ni mauti. Dhambi ya Asili ilileta mfarakano na kifo duniani kote (taz. Mwa 3). Mungu alipoweka utaratibu wa kutolea dhabihu ya mnyama, damu ya mnyama iliyomwagika ilitumika kama ondoleo la dhambi za binadamu.
Utaratibu huu ulifanyika kwa njia ya ibada ya kila mwaka iliyojulikana kama Siku ya Upatanisho. Kama sehemu ya ibada hii, Kuhani Mkuu alichagua mbuzi wawili kutoka miongoni mwa jamii.
Mmoja wa mbuzi hawa alichinjwa na kutolewa kama dhabihu ili kufanya upatanisho kwa dhambi za watu. “Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam! Dhambi zao zote, naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari.
“Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu; naye atamwacha mbuzi jangwani.” (taz. Law 16:20-22).
3. Wazazi wetu wa mwanzo walionja hasara na maumivu ya kumwasi Mungu. Farao, mfalme wa Wamisri ni mmoja wa viongozi walioanzisha utengano na Mwenyezi Mungu. Moyo wake ulikuwa mgumu na kushindwa kuona ukuu wa Bwana Mungu wa Waisraeli. Alidiriki kutuma jeshi lake liangamize taifa la Mungu, kinyume chake Mungu alipigana kulilinda taifa lake na kuliangamiza jeshi la Farao ndani ya Bahari ya Shamu (taz. Kut 14:26-31).
Uadui huu alioufanya Farao si kitu cha kuiga. Kupatana na Mungu na kupatana kati yetu ni moja ya zawadi kubwa tulizopewa na Mungu mwenyewe.
Tunajifunza kutoka kwa Daudi ambaye baada ya kutenda dhambi aliomba kupatanishwa na Bwana (taz. 1Sam 12:13) na kwa upatanisho huo aliyanusuru maisha yake.
Mstari huu unajikamilisha kwa lugha ya upendo yenye kuhimiza kupokea msamaha usio na malipo. Ni maneno ya upendo yenye ujumbe unaoomba binadamu ajipatanishe na Mungu.
4. Kila binadamu anatamani kuwa huru na kuwa na amani ndani yake. Hatuwezi kupata amani kama tuna ugomvi na Mungu, ndugu zetu na marafiki zetu wa karibu.
Njia sahihi ya kuleta mapatano ni maridhiano, kufanya jitihada kuona ni mambo gani yaliyosababisha ugomvi au chuki baina ya pande mbili.
Mungu ni zaidi ya rafiki, ni Baba na ni Muumba wetu. Mara nyingi tumevunja muunganiko naye kwa njia ya dhambi. Mungu anasema mimi ni Mungu mwenye wivu, hataki tuwe na miungu mingine, lakini kwa ukaidi, binadamu amekiuka na kuanza kuvutwa na malimwengu, na kumwacha Mungu halisi, na hapo ndipo mafarakano huanza.
5. Mapatano ya Mungu na binadamu yanapaswa yastawishwe na mapendo kwa wengine, kwa kuwa haiwezekani kusema unampenda Mungu usiyemwona na kumchukia binadamu unayemwona (taz. 1Yoh 4:20-21).
Mapatano ya binadamu na Mungu ni ishara ya wazi ya kumtangazia shetani kwamba tunavunja ushirika naye na kuungana na Mungu.
Bwana wetu Yesu Kristo alimshinda shetani, nasi tutamshinda kwa kuyakataa yote yatokayo kwake kama choyo, kiburi, ufisadi, kutokutenda haki, tamaa mbaya na mengine mengi yanayofanana na hayo.
6. Kupatana ni kukubali kuanza upya, ni kuzika udhaifu wote wa zamani ambao ulikuwa chanzo cha mifarakano na Mungu na wenzetu kama nabii Isaya anavyoweka wazi chanzo cha mifarakano na Mungu:
“Lakini maovu yenu yamewafarakanisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.” (Isa 59:2).
Tunaalikwa kutembea katika njia iliyokusudiwa na Mungu katika maisha yetu, kamwe tusijaribu kutumia akili na uwezo wetu pekee bila ya kumshirikisha Mungu, kwa kuwa Mungu ndiye mwenye ramani yote ya maisha yetu.
“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” (Yer 29:11).
Katika kuyapokea hayo mema, Mungu aliwaasa taifa lake kupatana naye na kuwa na ushirika naye. Nabii Yeremia anasema: “Ee Bwana, najua kuwa njia ya binadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uweza wa binadamu.” (Yer 10:23).
Kitabu cha Mithali kinaeleza bayana kuwa: “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu lakini mwisho wake ni njia za mauti.” (Mith 16:25).
7. Kwa kurejea vifungu hivi, taifa la Mungu lilihitaji kutokana na upungufu wake, kupatanishwa na Mungu kwa sababu lisingefanikiwa nje ya Mungu. Binadamu hawezi kufanikiwa nje ya Mungu na hata kama akifanikiwa ni mafanikio ya muda mfupi tu yenye uchungu na majuto ndani yake.
Taifa la Mungu lilipojipatanisha na kuomba neema na huruma ya Mungu, Mungu aliahidi kuwa pamoja nao:
“Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; nitakushauri jicho langu likikutazama.” (Zab 32:8).
Nabii Isaya alilikumbusha taifa la Mungu kwamba binadamu asipokuwa na mapatano mazuri na Mungu hawezi kuendelea kustawi katika nyanja yoyote ile, iwe ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii, kwa kuwa Mungu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kwa maisha yote ya binadamu:
“Kumbuka mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu wala hapana mwingine; mimi ni Mungu wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, shauri langu litasimama, nami nitayatenda mapenzi yangu yote.
“Nikiita ndege mkali kutoka mashariki, mtu wa shauri langu toka nchi iliyo mbali; naam! Nimenena, nami nitatekeleza; nimekusudia, nami nitafanya.” (Isa 46:9-11).
8. Binadamu ni wa thamani kubwa mbele za Mungu na thamani hiyo huzidi sana pale anapojipatanisha naye kwa njia ya toba ya kweli. Mungu anawahurumia watu wake kama baba amhurumiavyo mtoto wake.
Taifa la Mungu kwa kuishi katika mapatano na kuhurumiwa na Mungu lilikuwa na nafasi ya kumcha Mungu wao vema: “Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.” (Zab 103:13-14).
Itaendelea.