HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA MAZUNGUMZO NA WASHIRIKI WA MKUTANO WA JUKWAA LA UONGOZI AFRIKA, IKULU, DAR ES SALAAM,  TAREHE 30 AGOSTI 2019

 

Ni heshima kubwa kwangu kupata fursa hii adhimu ya kuzungumza kwenye Mkutano huu muhimu kwa mustakabali wa Bara letu la Afrika. Natambua kuwa huu ni Mkutano wa sita tangu kuanzishwa kwa Jukwaa la Uongozi la Afrika mwaka 2014 na mmekuwa mkifanya Mikutano kama hii katika nchi mbalimbali lakini, mwaka huu, mmeamua, kwa mara nyingine tena, kufanyia Tanzania. Hivyo, nitumie fursa hii kuwashukuru sana kwa heshima hii kubwa kwa Taifa letu. Napenda pia nitumie fursa hii kuwakaribisheni nyote hapa Ikulu. Nitumie fursa hii pia kuwakaribisha nchini wageni kutoka nchi mbalimbali mkiongozwa na Marais Wastaafu wa Nigeria, Tanzania, Afrika Kusini, Jamhuri ya Somalia na Madagascar.

Aidha, naipongeza sana Ofisi ya Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, pamoja na Taasisi yetu ya Uongozi, kwa kuanzisha Jukwaa la Uongozi Afrika ili kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikabili Bara letu. Ni ukweli usiopingika kwamba changamoto za Afrika zitatatuliwa na Waafrika wenyewe. Hakuna wajomba watakaokuja kutusaidia. We must face our own realities, no imported solutions can resolve Africa’s challenges sustainably. Sisi Waafrika tunafahamu changamoto zetu vizuri zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.

Hivyo basi, nawapongeza waheshimiwa Marais Wastaafu kwa kuendelea kutoa mchango wenu kwenye uongozi wa nchi zenu na Afrika kwa ujumla. Uzoefu wenu unatusaidia sana sisi ambao tumepokea dhamana hizi kubwa za kuyaongoza Mataifa yetu. Na katika hili, naomba mniruhusu niwashukuru watangulizi wangu mliopo hapa; Mheshimiwa Mzee Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Mheshimiwa Mzee Kikwete, ingawa yeye anaonekana bado kijana mbichi kabisa. Nawashukuru kwa ushauri mbalimbali ambao mmekuwa mkiutoa katika kuongoza nchi yetu lakini zaidi kwa kuniwezesha mimi kuchaguliwa kuwa Rais. 

Mzee Mwinyi ndiye aliyesimamia mchakato wa kwanza kabisa uliopelekea mimi, kwa mara ya kwanza, kuwa Mbunge. Akiwa Mwenyekiti wa CCM, angeweza kunikata tu jina na huenda nisingekuwa Mbunge. Mzee Mkapa aliniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na baadaye Waziri kamili. Vilevile, Mzee Kikwete aliniteua kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Waziri wa Ardhi na Waziri wa Ujenzi. Lakini huyu Mzee Kikwete ndiye aliyesimamia pia mchakato uliniwezesha kuwa Rais. Kwa kweli, mchango wenu hautasahaulika katika historia ya Taifa letu. Nawashukuruni sana Wazee wangu.

Waheshimiwa Marais Wastaafu;

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Washiriki:

Ni dhahiri kuwa msingi mkubwa wa maendeleo ya kweli ya taifa lolote ni rasilimali zake na watu wake. Lakini uwepo wa rasilimali na watu pekee havitoshi kuleta maendeleo, endapo itakosekana mifumo thabiti ya kusimamia rasilimali na kuwaendeleza watu ili wanufaike na rasilimali zilizopo.

Nyote hapa mnafahamu kwamba Bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa maliasili kama vile ardhi yenye madini, gesi, mafuta na inayofaa kwa kilimo; wanyamapori; misitu; maeneo ya uvuvi; nk. Sipendi kutoa takwimu hapa lakini ninyi mnajua, kwa mfano, takriban asilimia 30 ya ardhi yenye kufaa kwa kilimo duniani inapatikana Afrika. Hata hivyo, rasilimali hizi hazijasimamiwa na kutumiwa vizuri ili zilete manufaa stahili kiuchumi.  Kimsingi, tatizo la umasikini Afrika ni la mifumo yetu ya usimamizi na matumizi bora ya rasilimali tulizo nazo. Ni kwa sababu hii ninawapongeza sana kwa kaulimbiu muafaka kabisa ya “Kuimarisha Usimamizi Bora wa Maliasili kwa ajili ya Mageuzi ya Kijamii na Kiuchumi Afrika” yaani “Promoting Good Natural Resource Management for Socio-Economic Transformation in Africa”. Kaulimbiu hii inaonyesha umuhimu wa Afrika kujenga mifumo mipya ya kusimamia na kutumia rasilimali zake kwa manufaa ya watu wake, vinginevyo rasilimali zetu zitasimamiwa na kutumiwa na watu wengine kwa manufaa yao. Na ndicho ambacho kimekuwa kikifanyika katika maeneo mengi ya Bara letu.

Lakini swali kubwa la kujiuliza: ni kwa nini Bara tajiri la Afrika limeshindwa kusimamia na kutumia rasilimali zake ili kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi?  Naona, kwenye kusanyiko hili, kuna wataalam wengi wabobezi wa masuala ya siasa na uchumi, yaani political economy. Mimi siyo political economist, mimi ni mkemia tu. Sasa, katika “ulayman” wangu, nitataja sababu chache. Zingine nitawaachia wataalam.

Kwa maoni yangu, sababu kubwa ni masalia ya fikra za kikoloni au colonial mindset ambazo Waafrika tumeendelea kubaki nazo. Kimsingi hatukuitafsiri vizuri dhana ya uhuru. Dhana ya uhuru haiwezi kutenganishwa na kujitegemea. Kama hujitegemei huwezi kuwa huru, kwani uhuru wako utakuwa mikononi mwa unayemtegemea. Maana hasa ya kupigania uhuru ilikuwa ni kurejesha rasilimali na hasa maliasili zetu lakini pia kuwa na maamuzi kamili kuhusu namna ya kuzisimamia na kuzitumia kwa manufaa yetu ili kuleta ukombozi wa kiuchumi. Na hii ndiyo namna pekee ya kulinda uhuru wa kisiasa.

Kutokana na kutoelewa dhana kamili ya uhuru, tukadhani kwamba watawala wetu wa zamani ndio wenye uwezo kutusaidia kusimamia na kuendeleza rasilimali zetu. Na huu ndio mwanzo wa ugonjwa wa utegemezi, yaani dependency syndrome unaolitesa Bara letu la Afrika. Tusidanganyike watawala wetu wa zamani hawawezi kugeuka overnight na kuwa wajomba zetu au wakombozi wetu kiuchumi. Utegemezi huu ndio umeimarisha mizizi na misingi ya ukoloni mamboleo. Ni lazima tuamke!

Sababu ya pili ninayoiona mimi ya kushindwa kusimamia maliasili zetu na kuzitumia kuleta mageuzi ya kiuchumi ni tafsiri potofu ya msingi wa maendeleo. Mara nyingi tumedanganyika na kudhani kuwa fedha ndiyo msingi wa maendeleo. Hivyo, tumekuwa tukizunguka kwenye mataifa tajiri kuomba misaada na mikopo, na inawezekana kabisa misaada na mikopo hiyo inatokana na maliasili zetu wenyewe. As Africans, we must focus on what is available in our local and immediate context and transform it into money. Fedha ni matokeo ya mwisho kabisa ya matumizi ya maliasili zetu na siyo msingi wa maendeleo. Hata Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Fedha itakuja tu.

Sababu nyingine kubwa ni ukosefu wa ubunifu na teknolojia ya viwanda, yaani lack of innovation and industrial backwardness. Afrika haitaweza kusimamia na kutumia rasilimali zake kiuendelevu bila kuwa na viwanda. Tukiendelea kuuza mazao ghafi ya kilimo, madini, misitu, mifugo, uvuvi, nk.; itakuwa ni vigumu sana kufikia mageuzi ya kijamii na kiuchumi kupitia maliasili zetu. Ni lazima tukuze ubunifu wa vijana wetu pamoja na teknolojia ya viwanda. Na hapa siyo lazima tutumie teknolojia kubwa sana yenye gharama. Tujikite kwenye teknolojia rahisi na kufanya uhawilishaji wa teknolojia ya viwanda ndani ya Bara letu ili tuweze kusindika asilimia kubwa ya mazao yanayotokana na maliasili zetu.

Sababu kubwa ya nne kwa mtazamo wangu ni migogoro na hali tete ya kisiasa Barani Afrika. Maeneo mengi katika Bara letu, hususan yenye maliasili nyingi, yanakumbwa na migogoro. Kwa sehemu kubwa, migogoro au mapigano haya yanasababishwa na mabeberu wanaotaka kuendelea kutumia maliasili za Afrika kwa manufaa yao. Wakati sisi tunapigana, wenyewe wanakula. Na kamwe hawatapenda Mataifa yetu yawe na amani kwani migogoro ndio mtaji wao.

Sababu ya tano ni mikataba na makubaliano tunayoingia na wawekezaji katika kutumia rasilimali zetu. Mara nyingi mikataba hii hunufaisha upande mmoja. The agreements are not founded on a win-win principle. Tatizo hili limesababisha matumizi mabovu ya maliasili za Afrika bila kuleta impact yoyote kwa wakaazi wa Bara hili. Lakini chanzo kikubwa cha mikataba mibovu ni ukosefu wa uzalendo  miongoni mwa watendaji wa Serikali zetu na hujuma zinazofanywa na mabeberu pamoja na vibaraka wao wa ndani ya nchi husika. Endapo watendaji wetu wangekuwa na uzalendo, wasingekubali kuingia mikataba isiyo na manufaa kwa mataifa yao. Na hapa nikiri kwamba nchi yetu imeliwa sana kutokana na mikataba mibovu, hususan kwenye madini. Madini yameanza kuchimbwa miongo mingi iliyopita lakini hatukuona manufaa yake hadi tulipoamua kuipitia upya mikataba na kubadilisha Sheria zetu.

Sababu ya sita, na hii nitaomba iwe ya mwisho, ni uharibifu wa maliasili unaosababishwa na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi. Hii nayo ni changamoto kubwa katika Bara la Afrika na chanzo kikubwa ni ukataji hovyo wa misitu kwa ajili ya nishati ya majumbani. Kutokana na gharama kubwa za umeme na gesi asilia, watu wengi bado wanatumia kuni na mkaa kama nishati za majumbani. Chanzo kingine cha mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa maliasili ni uchafuzi wa mazingira unaofanywa na mataifa makubwa yaliyoendelea kiviwanda lakini Afrika ndiyo inayoathirika zaidi. Ukame, mafuriko na kutotabirika kwa mifumo ya hali ya hewa ni baadhi ya madhara ya mabadiliko ya tabia nchi. Ili kukabiliana na madhara haya, hatuna budi kuchukua hatua za pamoja. Hizi ni baadhi tu ya sababu ambazo binafsi nadhani zimesababisha nchi zetu zishindwe kunufaika na maliasili zake. Lakini, kama nilivyosema awali, Mkutano huu umeshirikisha wataalam wazoefu na wabobezi. Hivyo basi, zitaibuliwa sababu nyingine nyingi na hivyo kusaidia nchi zetu kunufaika na rasilimali zake.

Waheshimiwa Marais Wastaafu;

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Washiriki:

Baada ya kutaja sababu hizi, naomba mniruhusu, japo kwa ufupi, nitaje baadhi tu ya hatua ambazo, kama Taifa, tumeanza kuzichukua ili kusimamia matumizi bora ya maliasili ili hatimaye tufikie mageuzi ya kijamii na kiuchumi.  Kwanza, tumetunga Sheria ya kulinda Utajiri na Rasilimali zetu za Asili ya Mwaka 2017, yaani The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act, 2017. Pili, tumepitia upya na kurekebisha mikataba ya uchimbaji madini isiyo na manufaa kwa Taifa. Tatu, tumeweka msukumo mkubwa kwenye ujenzi wa viwanda na ukuzaji wa teknolojia ya viwanda ili mazao yanayotokana na maliasili zetu yasindikwe kwanza na kuongezewa thamani kabla ya kuuzwa nje. Nne, ili kudhibiti uharibifu wa maliasili za misitu na kulinda bayoanuwai kwa ujumla, tunatekeleza miradi mbalimbali ya nishati ya umeme, ukiwemo mradi wa Bwawa la Nyerere utakaozalisha Megawati 2115 kwenye Bonde la Mto Rufiji. Hii itapunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa, hivyo kulinda mazingira yetu. Sanjari na hili, tumeendelea kuongeza maeneo yetu ya uhifadhi, ambapo tumeanzisha Hifadhi tatu mpya za Taifa kwenye ukanda wa Kaskazini-Magharibi na ya nne iko mbioni kuanzishwa kwenye ukanda wa Kusini. Aidha, tumechukua hatua nyingine nyingi ikiwemo, kudhibiti nidhamu ya watumishi wa umma, kudhibiti ufisadi na ubadhirifu, tukiamini kwamba hatua zote hizi zitachangia kwenye matumzi bora ya rasilimali zetu na hatimaye kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Na, kwa bahati nzuri, tumeshaanza kuona matokeo ya hatua hizi.

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Washiriki:

Naomba nisiwachoshe kwa hotuba ndefu. Najua mtaendelea na majadiliano baada ya chakula cha mchana na kwa kweli nitafurahi, endapo nami nitapewa nakala ya maazimio mtakayokuwa mmeyafikia mwishoni mwa Kongamano hili. Nihitimishe kwa kuwapongeza tena kwa kuandaa majukwaa kama haya kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za uongozi Barani Afrika. Ni matumaini yangu kwamba Majukwaa haya yatakuwa chachu ya mapinduzi ya kifikra na kidira miongoni mwa viongozi wa Afrika na hatimaye kulikomboa Bara letu kiuchumi. Nawatakia majadiliano na maazimio mema! Sasa, kwa heshima, niwaalike kwa ajili ya chakula cha mchana.

Mungu Libariki Jukwaa la Uongozi Afrika!

Mungu Ibariki Afrika!

Asanteni sana kwa kunisikiliza.