Ulinzi mkali unatarajiwa kuchukua nafasi yake, Rais wa Russia, Vladimir Vladimirovich Putin, atakapozuru Tanzania mapema mwakani kutokana na ‘mbabe’ huyo kuwa na uhasama na Marekani.
Wakati wowote Rais Putin anaposafiri — iwe ndani ya Russia au nje ya nchi — ulinzi wake ni mkali na ulio kamili (almost absolute) kama ule wa Barack Obama wa Marekani.
“Itakuwa balaa,” anasema ofisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye alidokeza kuwa ziara hiyo inaandaliwa. Ofisa huyo aliomba kutotajwa jina lake.
“Usalama wake ni kama ule wa Obama,” anasema ofisa huyo na kuongeza kuwa analindwa na hatari zote mpaka zile za moto, maji na uvamizi wa kivita hasa wakati huu akishutumiana na Obama katika kuleta malumbano huko Syria na Ukraine.
“Atakapotua hapa, hakuna ndege nyingine itakayokuwa inatua wakati huo huo yaani kama ilivyo kwa Obama,” anasema mtoa taarifa huyo akirejea taarifa ya jarida na mtandao wa Forbes unaomtaja Putin kuwa ndiye mtu mwenye nguvu zaidi duniani.
Ulinzi wa Putin uko chini ya kitengo cha usalama maarufu kwa jina la SBP, ambao kazi yake kubwa ni kuhakikisha ulinzi wa rais wa Russia. Kitengo hicho kina wakurugenzi tisa wa KGB na wote wako chini ya ukuu wa Oleg Clementiyev, ambaye ni mkuu wa usalama wa rais.
Kama ilivyo kwa Obama, popote anapokwenda Putin nchi husika inakuwa nyuma ya Russia katika masuala ya ulinzi. Baadhi ya maofisa wanaomlinda Putin huvaa miwani yenye kamera ambazo zinarekodi na kurusha moja kwa moja sura na watu mbalimbali anaokutana nao au wanaojitokeza kumpokea. Yote ni katika kuhakikisha usalama.
Rais Putin anayeripotiwa kuwa na mipango ya kuzuru Tanzania Februari mwakani, ndiye mtu mwenye nguvu zaidi duniani. Jarida na mtandao wa Forbes maarufu kwa kutoa orodha mbalimbali zikiwamo za watu matajiri duniani, wanathibitisha hilo kwa mara ya pili mfululizo katika rekodi ya miezi sita ndani ya mwaka 2014.
Mtandao huo wenye makao yake makuu Marekani, mwaka jana ulimtaja Rais Obama wa Marekani kuwa ndiye mtu mwenye nguvu kabla ya kupigwa kumbo na Putin.
Kwa mujibu wa mtandao huo, mbali ya marais Putin na Obama, wengine wenye nguvu ni Rais wa China, Xi Jinping, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha China; Papa Francis kutoka Vatican na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel. Ingawa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imekwepa kuthibitisha kuhusu ujio wa Putin, taarifa za uhakika zinasema kwamba mwanajeshi hiyo — rubani wa ndege za kivita, atatua nchini Februari mwakani.
Ujio wa Putin ni tafsiri ya uelewano mzuri ambao umejengwa na Serikali ya Tanzania chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambao tayari wamefanikisha ziara za viongozi mbalimbali kutoka mataifa yenye nguvu ya kiuchumi na kijeshi.
Vyanzo vya habari vya uhakika katika Wizara ya Membe, vinasema kwamba kuna mchakato unaendelea juu ya ujio wa rais huyo, ingawa bosi huyo anakataa kuthibitisha moja kwa moja taarifa ya ujio wa Rais Putin.
Membe anasema kuwa anatarajia kusafiri kwenda Moscow mwezi huu wa Novemba kwa mwaliko wa heshima uliotoka kwa waziri mwenzake wa Mambo ya Nje, Sergei Lavrov. Membe anasema hakuwa na taarifa yoyote inayohusu ujio wa Putin wala maandalizi ya ziara hiyo, “kama ipo, basi itafahamika baada ya ziara yake,” anayokwenda Russia.
“Ninachoweza kukwambia kwa wakati huu ni kwamba nimealikwa Moscow (mji mkuu wa Russia) mwezi ujao (Novemba). Ni lazima niende, na nitakuwa mtu pekee katika nafasi ya kusema chochote juu ya mjadala wetu,” anasema.
Mbali ya Membe kuruka, pia Ubalozi wa Russia uliopo jijini Dar es Salaam, unakana kuthibitisha juu ya ziara hiyo kwa kuwa hawakuwa na taarifa yoyote kutoka Moscow.
Kwa miaka miwili iliyopita, Tanzania imeweza kupokea viongozi wakuu wa mataifa yenye nguvu duniani — Rais wa China, XI Jinping, aliyeitembelea Tanzania Machi, mwaka jana na Obama miezi mitatu baadaye.
Ziara ya kiongozi wa Russia kwa Tanzania ni jambo ambalo tayari linaibua maswali kutoka kwa wataalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa na waangalizi wengine.
Moja ya mambo ambayo yako wazi ni kwamba kuna uwezekano wa Putin kutumia fursa ya ziara hiyo kuhamasisha uhusiano imara wa kiuchumi na kisiasa wa nchi hizi mbili ambao awali uliwanufaisha kabla ya kuanguka kwa Ujamaa mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Wachambuzi wa mambo wanasema Tanzania ambayo inapambana kuendeleza sekta yake ya gesi na mafuta baada ya ugunduzi wa hazina kubwa ya gesi asili, ina nafasi nzuri za kunufaika kutoka kwenye ziara ya kiongozi wa nchi yenye utaalamu mkubwa kwenye eneo hilo.
Kwa upande mwingine wanasema kuwa Putin atataka kupata baadhi ya makubaliano ya kibiashara kwa ajili ya kampuni za gesi na mafuta za Urusi kwa wakati huu ambao nchi za Afrika Mashariki zinakabiliwa na matatizo ya ndani na vikwazo vya uzalishaji nje ya nchi.
Putin ni nani?
Oktoba 7, mwaka huu Rais Putin alitimiza miaka 62 tangu kuzaliwa kwake. Alizaliwa Oktoba 7, 1952. Alikuwa Rais wa pili wa Shirikisho la Russia na Waziri Mkuu wa sasa wa Russia, vilevile mwenyekiti wa chama cha kisiasa cha Muungano wa Russia na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Russia wa Belarus.
Alikaimu kiti cha urais mnamo Desemba 31, 1999 mara baada ya Rais Boris Yeltsin kujiuzulu ghafla, na kisha Putin akashinda uchaguzi wa rais mnamo mwaka 2000. Mwaka wa 2004, alichaguliwa upya na kushinda, hivyo aliendelea na kipindi chake cha pili hadi Mei 7, 2008 kabla ya kuachia utawala wa nchi kwa Dmitry Medvedev aliyeshinda kiti cha urais.
Medvedev kwa kutambua umuhimu wa Putin, mara moja alimteua kuwa Waziri Mkuu katika kile kilichoelezwa kuongoza kwa pamoja bila kinyongo (tandemocracy).
Jina lake lina asili ya watu wa mashariki mwa Russia likiwa na maana ya mila katika mji wa Leningrad alikozaliwa.
Ni Luteni Kanali
Kwa miaka 16 Putin alikuwa Ofisa Mwandamizi wa Jeshi la Russia likifahamika kwa kifupi KGB, akipanda cheo hadi cha kufikia Luteni Kanali kabla ya kujiuzulu na kuingia kwenye siasa akijiunga na chama kilichoanzishwa huko Saint Petersburg, mwaka 1991.
Kutoka Saint Petersburg mpaka Moscow
Baada ya kuwa kwenye chama hicho kwa miaka mitano huko Saint Petersburg, mwaka 1996 alihamia jijini Moscow kuungana na utawala wa Rais Boris Yeltsin ambako alipaa kwa haraka sana hadi kuteuliwa kuwa kaimu rais Desemba 31, 1999 baada ya Yeltsin kujiuzulu ghafla.
Afanya marekebisho ya katiba
Septemba 2011, Russia ilifanya Marekebisho ya Katiba katika kipengele cha muda wa rais kukaa madarakani. Marekebisho ya kutoka miaka minne hadi sita na Putin akatangaza kuwania madaraka ya urais kwa mara ya tatu katika uchaguzi uliofanyika Machi 2012.
Nia hiyo ya Putin ilipingwa kwa maandamano katika miji mbalimbali nchini Russia, lakini ‘kidume’ alipambana na kushinda. Kwa sasa anashika madaraka ya urais mpaka mwaka 2017.
Mipango mingi ya Putin haipiti kwa wepesi kwani huwa inakutana na changamoto au vikwazo vingi kutoka kwa watu wa kawaida hadi hata waangalizi wa kimataifa kuona kuwa demokrasia imekiukwa, lakini mwisho wa siku, anashinda.
Tangu mwaka 2011, Putin amekuwa mbabe akitangaza Russia yenye mabadiliko ya kweli katika kila sekta badala ya kuwa na serikali isiyo na mamlaka.
Tangu atwae ukaimu rais, kuwa rais na kuwa rais kamili (1999-2008), uchumi wa Russia ulikua kwa kiasi kikubwa kwa viwanda kuongezeka kwa asilimia 2.5; mishahara ya wafanyakazi ilipanda kwa zaidi ya mara tatu; makabwela nchini humo walipungua hivyo kukawa na maisha bora kwa raia wa Russia.
Uchumi ulikua zaidi pale Putin alipochukua urais kwa mara ya kwanza na kushika kasi kwa miaka minane mfululizo, ambako pato la taifa (GDP) ilikuwa ni asilimia 72.
Putin na mzozo wake Marekani
Mara kwa mara Rais Putin amekuwa akiituhumu Marekani kwa kuzorotesha uhusiano na Russia akisema inaendekeza siasa za kiuadui na za kindumila kuwaili katika dunia ya sasa. Rais Putin anakumbuka na kusema uhusiano wa pande mbili ulianza kuzorota mwaka 2003 wakati Marekani ilipoishambulia kijeshi Iraq.
Luteni Kanali huyo wa Russia anasema kwamba Marekani inavunja amani ya dunia kwa kuwasaidia na kuwahami magaidi wa Daesh na kwamba kwa sasa kunahitajika umoja wa ukweli wenye nia ya kupambana na magaidi, na umoja ambao unahami makundi ya kigaidi.
Ni muhimu kuashiria kwamba Marekani na washirika wake ambao ndiyo walokuwa wakiwashajiisha na kuwasaidia magaidi wa Daesh kupambana dhidi ya serikali halali ya Bashar Asad ya Syria tangu mwaka 2011, na sasa wamegeuka na kuunda muungano wa kupambana dhidi ya magaidi hao.
Pia imeripotiwa kuwa ndege za Marekani zimeshusha shehena za silaha kwa magaidi wa Daesh, lakini Rais Obama amejitetea kwa kusema kuwa shehena hizo zilikuwa ni msaada wa silaha kwa wapambanaji wa Kikurd, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya silaha hizo zimeshushwa katika maeneo ya magaidi hao.
Urusi na Iran ni nchi ambazo zilitangaza wazi kuuhami utawala halali wa serikali ya Syria. Rais wa Russia ameongeza kuwa uamuzi wa kimakosa uliofanywa na nchi za Magharibi na hasa Marekani kuhusiana na vita ya Iraq, mgogoro wa Libya na masuala mengine muhimu ya kimataifa, haukuungwa mkono hata kidogo na Serikali ya Russia.
Rais Putin amesema kuwa azma ya Marekani ya kuweka mfumo dhidi ya makombora huko Ulaya, inapingwa vikali na Moscow kwani ina shabaha ya kuudhoofisha mfumo wa kujilinda wa Russia. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa hivi sasa kunashuhudiwa dalili za kutokea kwa mara nyingine tena vita baridi baina ya Marekani na Russia ya Putin.
Inaonekana kuwa mara baada ya kuchaguliwa tena Putin kuwa Rais wa Russia mwaka 2012, mivutano na misuguano kati ya pande mbili imezidi kuongezeka. Hii ni katika hali ambayo, madai matupu yaliyotolewa na Rais Obama wakati wa kuanza kipindi chake cha kwanza cha urais cha kuboresha uhusiano wa Marekani na Russia na kuondoa hitilafu zilizopo, yamesababisha uhusiano wa pande hizo mbili kuzorota zaidi.
Kuongezeka harakati za vikosi vya NATO katika mpaka wa Russia, uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa kisingizio cha kuimarisha misingi ya demokrasia nchini humo, ni miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa yakipigiwa upatu na vyama vyote vikuu viwili nchini Marekani, na kuwakera viongozi wa Moscow.
Katika kuonesha radiamali yake dhidi ya siasa za kutaka kujitanua za Marekani katika uga wa kimataifa, wiki chache zilizopita Russia ilifanya mazoezi na maonesho makubwa ya kijeshi katika maeneo ya Bahari Nyeusi na ya Mediterranean, na kuhesabiwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika katika historia ya nchi hiyo.
Russia pia ilizifanyia majaribio nyambizi zake na manowari maalum za kijasusi ambazo zina uwezo wa kukusanya taarifa za mfumo ulio dhidi ya makombora. Mikakati ya Moscow ya kurusha angani satalaiti za kisasa za kijasusi, ni sehemu ya mipango ya kuonesha nguvu zake za kijeshi za kukabiliana na nchi za Magharibi na hasa Marekani.
Wadadisi wa masuala wanaeleza kuwa kila uliposhadidi mgogoro wa kidiplomasia kati ya Moscow na Washington, viongozi wa nchi hizo walionekana kuwa makini kuuzuia usivuke mstari mwekundu, ama hivi sasa kuna uwezekano mkubwa wa kuanza mashindano mapya ya silaha, ambayo yanaweza kusababisha hali kuwa tata zaidi na isiyoweza kutabirika baina ya pande hizo mbili katika siku za usoni.
Russia yatetea Syria
Kwa zaidi ya miaka miwili, Syria imeingia katika mzozo uliosababisha machafuko makubwa nchini humo na kusababisha watu zaidi ya 1,300 kupoteza maisha. Mzozo huo unasababishwa na wananchi wa nchi hiyo kutoikubali serikali inayongozwa na Rais Bashar al-Assad.
Hatua iliyofikiwa katika vita hiyo sasa imesababisha mataifa makubwa na yenye nguvu kichumi na kijeshi kama Uingereza, Marekani, Russia na China kuingia katika vita hiyo. Marekani ilipeleka meli zake za kivita katika Bahari ya Mediterranean, hatua iliyopingwa na Russia na China ambazo zinaripotiwa kumsaidia Rais Assad kwa madai kuwa Syria ilitumia silaha za sumu katika vita hiyo.
Katika hili, Rais Putin anasema tuhuma kuwa Serikali ya Syria ilitumia silaha za kemikali ni upuuzi mtupu. Amesema Jeshi la Syria lilikuwa linasonga mbele, hapakuwa na sababu ya serikali kuwapa kisingizio wanaotaka kuingia kijeshi.
Putin anasema ikiwa Marekani ina ushahidi wa kuthibitisha tuhuma zake, basi iukabidhi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Anamkumbusha Rais Obama kuwa aliwahi kutwaa Tuzo ya Amani ya Nobel, na alimsihi kuwakumbuka wanyonge katika mashambulio.
Anakaribisha uamuzi wa Bunge la Uingereza ambalo halikuunga mkono Uingereza kuingilia kati Syria, na anasema ameshangazwa na uamuzi huo wa bunge.
Wachambuzi wa mambo ya kivita wanasema hatua ya mataifa haya kuingia katika mzozo huo inaweza kusababisha vita kuu ya tatu ya dunia au kurudisha vita baridi baina ya mataifa ya Marekani na Urusi.
Tayari Rais Al-Assad anazidi kuionya Marekani katika mashambulio yake nchini Syria kwamba atalisambaratisha taifa hilo lenye nguvu kubwa ya kiuchumi na kijeshi duniani. Harakati za kijeshi zinazoendeshwa na taifa hilo hazitafua dafu.
“Marekani itafeli kama ilivyoshindwa hapo awali katika vita waliyoianzisha kuanzia Vietnam hadi sasa,” anasema.
Ubabe dhidi ya Ukraine
Kuna wakati Putin anayetafsiriwa kuwa ni mbabe, anakuwa na roho nzuri. Hii ni kwa sababu raisi huyo alitoa wito kufanywe mazungumzo ya haraka kuhusu uhuru wa mashariki mwa Ukraine, kama sehemu ya mazungumzo ya kumaliza vita vya huko.
Putin amenukuliwa akisema, “Maslahi ya haki” ya watu wanaoishi katika jimbo hilo lazima yalindwe. Matamshi ya Rais Putin ni ishara kuwa Russia inataka Serikali ya Ukraine izungumze moja kwa moja na wapiganaji wanaoipendelea Russia kuhusu amani.
Rais Putin alionesha hivyo kabla ya mazungumzo kuanza mjini Minsk, Belarus (nchi jirani na Ukraine) baina ya Ukraine, Russia na Umoja wa Ulaya, kujadili msukosuko huo.
Na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Ukraine wameonya kuwa hali katika eneo hilo inakaribia kufika kiwango ambapo hali ya zamani haitoweza kurejeshwa tena. Na katika tukio jingine, Ukraine imekabidhi askari 10 wa miamvuli kwa Russia, na nchi hiyo iliwarejesha wanajeshi 63 wa Ukraine. Mvutano mkubwa kati ya Russia na Ukraine ni kuwania eneo la Jimbo la Crimea lililojitenga kutoka Ukraine.
Wakati wote Putin huwa anasifu uzalendo wa majeshi ya Russia na moyo wao wa kujitolea kwa uhuru wa taifa lao, wakiwamo wanajeshi 11,000 walioshiriki kuitaifisha Crimea ambao walikuwa na zana za kivita zikiwamo vifaru, mizinga na ndege za kivita.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, anasema ni jambo la huzuni kwa Putin kutumia maadhimisho hayo kwenda Crimea.
Ijue Russia ya Putin
Russia ni nchi ya Ulaya ya Mashariki na Asia. Mji mkuu ni Moscow. Ni nchi kubwa duniani kieneo. Kuna wakazi 144,000,000. Eneo lake ni 17,075,400 km². Hadi 1991 Russia ilikuwa sehemu ya Umoja wa Kisovieti na kiini chake. Wakati ule iliitwa Shirikisho la Jamhuri ya Kisovieti ya Kijamii ya Kirusi. Nchi hiyo ilikuwa ya kidikteta chini ya chama cha kikomunisti. Tangu 1990 imekuwa demokrasia. Muundo wa serikali ni shirikisho la jamhuri chini ya rais mtendaji.
Jiografia
Russia imepakana na Norway, Finland, Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Belarus, Ukraine, Georgia, Azerbaijan, Kazakhstan, China, Mongolia na Korea ya Kaskazini. Iko karibu vilevile na maeneo ya Marekani (jimbo la Alaska iko ngambo ya mlango wa Bering na Japan (kisiwa cha Hokkaido kiko ng’ambo ya mlango wa La Pérouse).
Eneo la Shirikisho la Russia linajumlisha sehemu kubwa ya kaskazini ya mabara ya Ulaya na Asia. Umbali kati ya upande wa magharibi na upande mashariki kabisa ni karibu kilomita 8,000. Mkoa wa Kaliningrad haufuatani moja kwa moja na maeneo mengine ya Russia umetengwa nayo na nchi za Kibaltiki.
Mara nyingi Russia hutazamiwa kama sehemu mbili za Urusi wa Ulaya hadi Milima ya Ural na Siberia au Russia wa Kiasia ambayo ni nchi pana kati ya Ural na Pasifiki. Pwani ndefu la kaskazini linatazama Bahari ya Aktiki. Sehemu kubwa ya Urusi ni tambarare penye vilima vidogo tu. Milima mirefu iko kusini mashariki ya Siberia.
Mito
Kati ya mito mikubwa kama vile Volga ambao ni mrefu Ulaya ukiishia katika Bahari ya Kaspi, Dnepr unaoishia katika Bahari Nyeusi; ni njia ya maji muhimu Oka, Moskva, Ob, Irtysh, Yenisei, Lena, Neva, Don na Amur.
Miji mikubwa ya Urusi
Majiji mawili makuu ni Moscow na Sankt Peterburg. Sankt Peterburg ilikuwa mji mkuu kuanzia mwaka 1703 hadi 1918 kama makao makuu ya Tsar au Kaisari wa Russia. Mwaka 1924-1989 ikaitwa Leningrad kwa heshima ya kiongozi wa mapinduzi. Moscow ni mji mkuu wa kale uliorudishwa nafasi yake baada ya mapinduzi ya kikomunisti ya 1918. Miji mingine mikubwa ni pamoja na Novosibirsk, Nizhniy Novgorod, Yekaterinburg, Samara, Omsk, Kazan, Ufa, Chelyabinsk, Rostov, Perm na Volgograd.
Hali ya hewa
Sehemu kubwa za Russia huwa na vipindi vya majira tofauti sana; joto jingi linafuatana na baridi kali. Kaskazini ya Siberia ina ardhi iliyoganda milele maana yake baridi imeingia katika ardhi kabisa.
Wakati wa joto sentimita za juu zinapoa na mimea kama nyasi na maua inastawi, lakini hakuna miti mikubwa kwa sababu nusu mita chini ya ardhi halijoto inakaa daima chini ya 0C°.
Historia
Historia ya Russia kama nchi ya pekee, ilianza polepole pale ambapo makabila ya wasemaji wa Kislavoni ya Mashariki walipoanza kujenga maeneo yao kuanzia karne ya nane Kabla ya Kristo (BK).
Waskandinavia waliunda dola la kwanza katika eneo la Kiev wakaitawala kama dola la Kislavoni. Wenyewe waliingia haraka katika lugha na utamaduni wa wenyeji lakini waliacha jina lao kwa sababu “Rus” kiasili ilikuwa jina kwa ajili ya Waskandinavia wale kutoka Uswisi ya leo.
Mwaka 988 Kiev ilipokea Ukristo wa Kiorthodoksi kutoka Bizanti. Dola la Kiev iliporomoka kutokana na mashambulio ya Wamongolia baada ya Jengis Khan na maeneo madogo zaidi yalijitokeza yaliyopaswa kukubali uwana wa Wamongolia.
Upanuzi wa utemi wa Moscow
Kubwa kati ya maeneo yale madogo ilikuwa utemi wa Moscow. Watemi wa Moscow walichukua nafasi ya kwanza kuunganisha Wasalvoni wa mashariki dhidi ya Wamongolia na kupanuwa utawala wao. Baada ya anguko la Konstantinopoli mwaka 1453 watawala wa Moscow walipokea cheo cha Kaisari wa Roma kilichoitwa “Tsar” na kuwa cheo cha watawala wa Urusi hadi 1917.
Hadi karne ya 18 eneo ya Moscow lilikuwa tayari kubwa likabadilika kuwa milki ya Kirusi iliyoendelea kupanua katika Siberia na Asia ya Kati. Sasa ilikuwa kati ya milki kubwa kabisa za historia ikienea kutoka Poland upande wa magharibi hadi Bahari ya Pasifiki upande wa mashariki.
Matengenezo ya kisiasa chini ya Peter I
Tsar Peter I (1689-1725) alitambua ya kwamba nchi yake ilikuwa nyuma kiteknolojia na kielimu kulingana na mataifa ya Ulaya. Alianzisha mabadiliko mengi ya kuiga mfano wa Ulaya ya Magharibi akahamisha mji mkuu kutoka Moscow kwenda mji mpya aliouunda sehemu ya magharibi ya milki yake, akauita Sankt Peterburg.
Tangu Peter I nchi ilishiriki katika siasa ya Ulaya pamoja na vita nyingi za Kiulaya. Mwanzo wa karne ya 19 milki ikashambuliwa na Napoleon aliyeteka Moscow lakini Warusi walifaulu kuwafukuza maadui.
Upanuzi katika Asia
Tsar wa Russia waliendelea kutawala kwa kuwa na mamlaka zote bila kushirikisha wananchi kama ilivyokuwa kawaida katika sehemu nyingine za Ulaya. Miji iliona maendeleo ya viwanda na jamii ya kisasa lakini sehemu kubwa ya wakulima waliendelea kukaa chini ya utawala wa makabaila.
Katika sehemu ya pili ya karne ya 19 Russia ilipanua utawala wake kwenye maeneo makubwa ya Asia ya Kati na Milima Kaukasus ikashindana na milki ya Osmani, Uajemi na athira ya Uingereza katika Asia.
Mapinduzi ya 1905 na 1917
Mwanzoni wa karne ya 20 Russia ikaonekana tena kuwa nyuma ya nchi za Magharibi na sababu kubwa ilikuwa nafasi kubwa ya serikali kuu iliyojitahidi kusimamia mabadiliko yote katika jamii na kuzuia mabadiliko iliyoonekana kama magumu machoni pa Tsar, makabaila na Kanisa Orthodoksi.
Mwaka 1904 upanuzi wa Russia katika Asia uligongana na upanuzi wa Japan. Katika vita dhidi ya Japan, Russia ilishindwa na tukio hili lilisababisha mapinduzi ya nchi ya 1905. Tsar Nikolas alipaswa kukubali uchaguzi wa Bunge la Duma mara ya kwanza. Hata hivyo, haki za Duma zilikuwa chache na mabadiliko yalitokea polepole mno.
Russia ilijiunga 1914 na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ikisimama upande wa Uingereza na Ufaransa dhidi ya Ujerumani na Austria-Hungaria. Vita haikwenda vizuri, wananchi wakawa na njaa na mapinduzi ya Februari 1917 yakamfanya Tsar ajiuzulu.
Vita ikaendelea na Wajerumani wakazidi kusonga mbele. Serikali mpya ya Bunge ikapinduliwa mnamo Oktoba 1917 na Mapinduzi ya Bolsheviki chini ya kiongozi wao Vladimir Ilyich Lenin.
Utawala wa kikomunisti na Umoja wa Kisovieti
Hii ilikuwa mwanzo wa vita ya wenyewe kwa wenyewe. Wakomunisti chini ya Lenin walishinda na kuigeuza Russia kuwa Umoja wa Kisoveti kuanzia 1922 wakiitawala kwa mfumo wa kiimla wa chama chao.
Ili kurahisisha utawala wao, Wakomunisti waliamua kutawala Russia ya awali kwa muundo wa shirikisho, wakaunda jamhuri mbalimbali kufuatana na mataifa ndani ya eneo hili kubwa. Russia ilikuwa sasa jina la jamhuri kubwa katika umoja huu ikaitwa Shirikisho la Jamhuri ya Kisovyiet ya Kijamii ya Kirusi.
Kikatiba, jamhuri hizi zote zilikuwa nchi huria lakini hali halisi zilitawaliwa zote kutoka makao makuu ya chama cha kikomunisti huko Moscow. Katiba hii ilipata umuhimu kuanzia 1989 wakati wa mwisho wa utawala wa Wakomunisti ambako jamhuri zote zilitafuta uhuru wao zikaachana na Umoja.
Mji mkuu wa Saint Peterburg ukabadilishwa jina kuwa Leningrad na baadaye makao makuu ya nchi yakahamishwa tena kwenda Moscow.
Kiongozi aliyemfuata Lenin mwaka 1924 alikuwa Josef Stalin, aliyeweza kugeuza utawala wa chama kuwa utawala wake mwenyewe akiongoza kwa jina la Katibu Mkuu wa chama cha kikomunisti.
Mwaka 1939 mwanzoni wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Stalin alipatana na Adolf Hitler wa Ujerumani kugawa maeneo ya Poland na nchi za Baltiki kati yao lakini mwaka 1941 Hitler alishambulia pia Umoja wa Kisovyeti.
Warussia walipoteza askari kwa mamilioni lakini waliweza kuwazuia Wajerumani wasiiteke Moscow na Leningrad. Kwa msaada wa Marekani, Warusi waliweza kurudisha Jeshi la Ujerumani na kusogea magharibi. Umoja wa Kisovieti ukawa kati ya nchi washindi wa Vita Kuu ya Pili.
Mashindano ya vita baridi dhidi ya Marekani
Tangu mwaka 1945 Jeshi la Urusi lilikaa katika nchi zote za Ulaya ya Mashariki hadi katikati ya Ulaya. Katika nchi hizo zote serikali za kikomunisti zilianzishwa na kusimamiwa na ofisi kuu ya chama cha kikomunisti huko Moscow.
Russia ikiwa kiongozi wa nchi za kijamii, ilishindana katika vita baridi dhidi ya nchi za Magharibi zilizoongozwa na Marekani. Athira ya Umoja wa Kisovieti ilipanua hadi Afrika, Asia na Amerika ya Kati ambako nchi mbalimbali zilianza kuiga mtindo wa kikomunisti.
Kuachana kwa Umoja kwa Kisovieti
Utawala wa kikomunisti uliendelea hadi mwaka 1990. Mwishoni matatizo ya kiuchumi yalizidi kwa sababu mfumo wa uchumi ulioongozwa moja kwa moja na serikali kuu pamoja na utaratibu wa kiimla uliozuia wananchi kupinga siasa ya viongozi na kuleta hoja tofauti, ulisababisha tena nchi kubaki nyuma.
Tangu mwaka 1990 jamhuri kadhaa za Umoja wa Kisovieti zilijitoa katika umoja na kutangaza uhuru wao ilhali serikali ilishindwa nguvu ya kuwazuia. Mwaka 1991 jamhuri za mwisho wanachama wa Russia, Belarus na Ukraine ziliamua kuumaliza Umoja wa Kisovieti.
Russia mpya
Tangu mwaka 1991 Russia iliyopungukiwa na maeneo mengi yaliyotwaliwa wakati wa karne ya 19 na 18 ilibaki peke yake ingawa bado ni dola kubwa duniani. Marais wa Russia baada ya mwaka 1991 walikuwa Boris Yeltsin na Vladimir Putin. Dmitry Medvedev alichaguliwa kuwa rais wa Russia mwaka 2008 na mtangulizi wake Vladimir Putin akawa waziri mkuu.