Ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama, hapa Tanzania imebadili mfumo mzima wa matumizi ya barabara na shughuli mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Katika hali ambayo haijazoeleka, wafanyabiashara na shughuli ndogondogo za kujipatia kipato zilizuiwa kandokando ya barabara jijini Dar es Salaam wakati wote wa ziara ya Rais Obama.

 

Miongoni wa makundi ya watu yaliyokumbwa na zuio hilo la serikali ni ombaomba, wamachinga, wang’arisha viatu na waendesha pikipiki (bodaboda).  Lakini pia baadhi ya maduka na hoteli zilizopo katikati ya jiji zilifungwa wakati wa utekelezaji wa ratiba ya ziara hii.

 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa, Said Meck Sadiki, alitangaza kwamba baadhi barabara jijini Dar es Salaam zitafungwa wakati wa utekelezaji ratiba za ugeni huu.

 

JAMHURI ilishuhudia barabara na mitaa mbalimbali vikiwa katika hali ya utulivu na usafi wa aina yake. Magari ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) yalionekana kufanya usafi wa kufuta vumbi na kunyunyiza maji barabarani.

 

Barabara hizo zilitumiwa na magari ya makachero wa Marekani na farasi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, miongoni mwa magari mengine ya msafara wa ugeni huu.

 

Inaaminika kwamba makachero 300 wa Marekani waliwasili hapa nchini kuweka ulinzi na kuhakikisha usalama wa hali ya juu katika kipindi chote cha ziara ya Rais Obama aliyefuatana na msafara wa watu zaidi 700.