Wiki iliyopita niliahidi kuanza kuandika masuala ya msingi katika kilimo cha muhogo. Nimepata simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakisema wanataka kulima muhogo, wengine tayari wanao muhogo na wengine wana mashamba au wengine wanatafuta mashamba ya kulima muhogo. Wengine wamepata furaha, na wengine wamekata tamaa.
Nimebaini kuna kiwango kikubwa cha watu kukosa uelewa katika suala la kilimo. Wakati nawaza suala la muhogo, Rais John Magufuli, Jumatatu ya Machi 19, mwaka huu akawa anazindua magari 181 ya Bohari ya Dawa Tanzania (MSD). Katika hotuba hiyo amezungumzia suala nchi yetu kutokuwa na viwanda. Amelizungumza kwa uchungu na naomba kwa ruhusa yako msomaji nimnukuu:
“Nilikuwa naonyeshwa baadhi ya madawa na vifaa mbalimbali ambavyo vinanunuliwa. Nimeonyeshwa vifaa vya wakina mama nimekuta ni pamba, lakini nilipoliangalia boksi zimeagizwa kutoka China! Na sisi ni wakulima wa kutosha wa pamba.
“Vifaa vya plastic (gloves) tunaagiza, mabomba ya sindano tunaagiza. Hii ndiyo ‘challenge’ [changamoto] kwa ndugu zangu Watanzania tungekuwa na viwanda vyetu hapa hizi bilioni 500 zingekuwa zinarudi kwa Watanzania.
“Tungekuwa na viwanda vyetu hizi fedha tunazozitenga zinapitishwa na waheshimiwa wabunge kwa ajili ya kununulia madawa bilioni 269 zingebaki hapa. Zingetengeneza ajira hapa.
“Lakini hili, tumezungumza, tunaimba. Sijui nitumie lugha gani? Labda niwaombe maaskofu wajaribu kuhubiri hili kwamba tunahitaji kutengeneza viwanda ili Watanzania wapate ajira.
“Labda niwaombe wahubiri na Watanzania wengine wanaojua kuhubiri vizuri, tuwaeleze Watanzania kwamba tunapoteza bilioni 500 kila mwaka kununulia madawa na vifaa mbalimbali kutoka nje wakati fedha hizi zingebaki hapa.
“Na kwa bahati nzuri Global Fund wametupa tenda sisi nchi ya Tanzania kununua madawa pia ya nchi zote za SADC hiyo nayo ni opportunity [fursa] nyingine. Lakini inapita…
“Tunalalamikia mengine yale ya kulalamikia mengine kwa maana ya manufaa ya Watanzania hatuyaangalii. Sijui Watanzania tumerogwa, sijui ni shetani amekaa mno hapa!
“Basi tumkemee kwa majina yote, jina la Mohammed na jina la Yesu akashindwe ili kusudi Watanzania tujue ni mahali gani tunatakiwa kupata fedha,” amesema Rais Magufuli.
Sitanii, ukimwangalia usoni Rais Magufuli utaona anamaanisha anachokisema katika hili la viwanda. Unaona uchungu alionao. Binafsi nimepata fursa ya kutembelea mataifa mbalimbali duniani, sijaona taifa lililoendelea bila viwanda.
Hata hiyo China tunayoona imeendelea kiviwanda sasa, mwaka 1979 chini ya Deng Xiaoping ilifanya uamuzi wa makusudi. Nchi zote zilizoendelea iwe ni Uingereza au Marekani ziliendelea si kutokana na jambo jingine, bali viwanda. Wiki tatu zilizopita niliandika makala nikakusihi msomaji uorodheshe vifaa vyote unavyotumia nyumbani kwako, nguo unazovaa na usafiri unaotumia halafu unionyeshe kilichoandikwa ‘Made in Tanzania.’
Nafahamu juhudi za baadhi ya Watanzania waliokwamishwa katika juhudi za kujenga viwanda na taasisi mbalimbali. Unakuta Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) linakuwa na masharti magumu kwa Mtanzania kuanzisha kiwanda. Wanakwambia tutachafua mazingira. Wanaweka viwango visivyokuwapo hata mbinguni.
Mimi najiuliza sipati jibu. Nchi zinazotupatia misaada ndizo zinazoongoza kwa kuchafua mazingira. China walisema mwaka 1979 kuwa hawawezi kushiriki kusafisha mazingira wakati hawajashiriki kuyachafua. Wakajenga viwanda vyenye kutumia makaa ya mawe na kila nishati iwayo. Hawa ukiangalia kiuhalisia wamechafua kweli mazingira, lakini sasa wanafanya juhudi za dhati kuyasafisha.
Sitanii, analozungumza Rais Magufuli la ujenzi wa viwanda si katika dawa na vifaatiba pekee. Tanzania haiwezi kuendelea ikiwa inategemea jembe la mkono. Nchi yetu haiwezi kuendelea kwa kutegemea kuchemsha maji kwa kutumia mkaa. Nchi yetu haiwezi kuendelea kwa kutegemea kuwa wachuuzi wa hadi njiti za meno.
Sasa nirejee katika suala la muhogo. Nimeulizwa maswali mengi. Lakini naomba kusema tunapaswa kujiandaa katika kilimo cha kisayansi. Tunapaswa kutumia wataalam wa kilimo kuongeza kiwango cha mavuno (yields) ya muhogo kutoka tani mbili kwa ekari hadi tani 17. Hii inamwezesha mkulima kupata faida kutokana na kuongezeka kwa mavuno.
Sitanii, katika kilimo cha muhogo faida kubwa tunaipeleka China tukiuza makopa. Hali waliyonayo sasa China mazingira kwao yamechafuka. Kwa mantiki hiyo tukiwauzia muhogo watazalisha gongo (ethanol) watakayoitumia kuendesha magari. Hii itakuwa faida kwao.
Lakini hata sisi tunaweza. Tunapaswa katika uwakezaji wa muhogo kuwa na mashine za kuvuna muhogo. Huwezi kuniambia mtu atalima ekari 100 na kupalilia kwa mkono. Gharama ya wafanyakazi itakutoa kapa katika kilimo hiki. Ukiwa na mashine itakusaidia kulima, kupanda, kupalilia na hatimaye kuvuna muhogo wako. Hili la mashine nitalieleza kwenye makala zitakazofuata.
Baada ya kuvuna muhogo tutapaswa kuwa na mashine za kuosha ili kuondoa udongo, kumenya kama tunataka kutengeneza wanga, kukatakata na kukausha (flash driers). Nasisitiza mashine za kukausha kwani muhogo unaharibika ndani ya saa 12 tangu uvunwe. Ukiuacha kwa zaidi ya saa hizo unaanza kupata michirizi ya kijani.
Ukiishapata michirizi ya kijani unabadilika rangi na kuwa mweusi. Ukiona muhogo umekuwa mweusi, basi ujue fika kuwa huo hauna thamani tena. Kwa wanaozalisha wanga, muhogo una thamani ukiwa mweupe kama theluji. Hata ukitaka kuzalisha unga wa muhogo (udaga) unapaswa kuwa mweupe kama ngano ndiyo utakupatia wateja wa kutosha.
Sitanii, baada ya kukausha makopa zipo mashine za kusaga, kuchuja/kuchekecha na kujaza kwenye mifuko ya unga au wanga (starch) kulingana na nini unataka kuzalisha. Masalia yanayobaki yaani machicha, yanatumika kuzalisha mbolea. Vijiti vya mihogo inayokuwa haitumiki kama mbegu nayo kuna mashine ya kuvisaga kisha vinatengenezwa mbao za MDF.
Kimsingi nimesikitika kwa mawazo ninayopata kutoka kwa watu walio wengi. Wamekisikia kilimo cha muhogo, wananipigia simu wakitaka niwaunganishe na wawekezaji. Ninapowambia kuwa wao ndiyo wawekezaji baadhi wanachukia. Katika mnyororo wa thamani, hatua nilizozieleza tangu kulima, kuvuna, kuosha, kumenya, kukausha, kusaga na kupakia katika viroba au mifuko hizo zote ni ajira na ni faida endapo mchakato wote huo ukifanyika hapa nchini.
Sitanii, nawaomba Watanzania tuondokane na mawazo ya uchuuzi. Kutafuta wawekezaji ni kujipunguzia faida. Benki zetu zipo hapa nchini. Tunachopaswa kutafuta sasa ni masoko ya bidhaa zetu na si wawekezaji. Ukisoma makala yangu vizuri, zao la muhogo pekee utaona kuwa unaweza kuwa na viwanda saba katika hatua mbalimbali.
Kwa kuwa na viwanda hivi vinavyoongeza thamani, unajiongezea kiwango cha faida. Kwa mfano, muhogo mbichi kilo 6 zinazalisha makopa kilo 3, na wataalam wanasema makopa haya yanazalisha unga kilo 2.5. Bei ya muhogo mbichi kilo moja ni Sh 150, hivyo kilo 6 ni sawa na Sh 900. Kilo ya unga wa muhogo safi ni Sh 2,000. Hivyo kwa kupata kilo 2.5 mkulima kwa kilo 9 zilezile ambazo angepata Sh 900 anapata Sh 5,000. Ni tofauti iliyoje?
Ombi na msisitizo wangu kwa Watanzania na taasisi zote zinazolenga kuzalisha muhogo, tuwaze katika kuwekeza kwenye viwanda. Viwanda vitaimarisha uchumi wa taifa letu. Viwanda vitaongeza thamani ya muhogo na kuwaongezea pato wananchi. Nikiri kwamba pamoja na kuingia mkataba wa kuuza muhogo (makopa) China kiwango chetu cha uzalishaji kiko chini.
Mchina anataka kuleta meli anunue makopa tani 100,000 kwa mwezi. Sisi tunazalisha wastani wa tani 2 kwa kila ekari ya muhogo. Kwa maana hiyo kuzalisha tani 100,000 kwa mwezi ina maana tunapaswa kuwa na ekari 50,000 za muhogo. Ikiwa tutazalisha kisasa tukapata angalau tani 17 za makopa kwa ekari, basi walau tunaweza kuhitaji ekari 5,800 kuzalisha hizo tani 100,000 kwa mwezi.
Sitanii, hapa ninachosisitiza ni kuwa kwa mwaka tukitaka kumuuzia huyu mteja mmoja tukilima kisasa, basi tunapaswa kama nchi kulima angalau ekari 60,000 na hizi nazo zilimwe kisasa kabisa ili zizalishe kati ya tani 17 na 20 ndipo tupate huyu mteja mmoja. Sasa nauliza; je, ndugu mkulima kati ya hizo tani 60,000 zinazotakiwa kulima wewe umejipanga kulima ngapi? Hiki kilimo cha ekari 1 hadi 5 ni cha kujikimu.
Unawezaje kulima ekari zote hizo? Zipo mbinu. Wananchi wanapaswa kujiunga katika vikundi na kuwa na eneo kubwa la kulima muhogo. Wakiishajiunga kwenye vikundi wanakuwa na andiko la biashara. Si andiko la mradi, maana watu wengi wanawaza ufadhili, andiko la biashara. Kama ni mtu mmoja anayo ardhi angalau kuanzia ekari 30, basi naye aandike andiko la biashara achukue mkopo benki, anunue matrekta na mashine za kuchakata muhogo. Ni kwa msingi huo tutaiona faida ya muhogo, bila hivyo tutapiga miayo hadi siku ya mwisho.