Wale wanaosikiliza hotuba za Rais John Magufuli, kuna kitu wanakipata mara kwa mara. Sijasikia hotuba yake yoyote akikosa kutaja neno ‘uzalendo’.
Amediriki kusema viongozi, akiwamo yeye, watapita lakini Tanzania itabaki; na ili ibaki, Watanzania wote hatuna budi kuwa wazalendo.
Rais anaamini kuwa kwa kujenga uzalendo, Tanzania itakuwa na nguzo imara za kuifanya iwepo leo na hata kesho.
Kwa wale wanaosikiliza hotuba na kusoma maandishi ya viongozi wetu wakuu waliotangulia, watakubali kuwa suala la uzalendo limesisitizwa mno.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), neno uzalendo maana yake ni: “Hali ya mtu kuwa tayari kuifia nchi yake, hali ya kuwa mzalendo”.
Hakuna taifa katika sayari hii ya dunia lililoweza kuendelea bila kuwa na wananchi wazalendo. Marekani ikiwekwa kwenye kundi la mataifa mengine ya dunia hii yaliyoendelea, ni taifa changa kabisa. Si taifa la kulinganisha na mataifa mengine kama Italia, Ufaransa, Uingereza na kadhalika. Tunaweza kutafuta sababu nyingi za kuhalalisha mtazamo wetu juu ya nguvu za kivita na kiuchumi ilizonazo Marekani sasa, lakini ukweli ni kuwa taifa hilo limekuwa kinara wa maendeleo kwa sababu ya uzalendo. Wakitambua kuwa wao ni watu walioonekana hawafai kuishi na wengine Ulaya – Wazungu wale waliopelekwa Marekani walijitambua. Wakauvaa uzalendo na kuibadili nchi.
Tunaweza kusema maendeleo ya Marekani ni matokeo ya utumwa. Sawa, utumwa una nafasi kubwa katika maendeleo ya Marekani. Hebu tuchukulie watumwa kama ‘kitendea kazi’. Wao ndivyo walivyofanya. Waliwaona Waafrika na watumwa kutoka mataifa mengine kama nyenzo muhimu kabisa kuifikia dhamira yao ya maendeleo. Walijua ndoto yao ya maendeleo hawawezi kuifikia kama wasingeingiza uzalendo hata kama ni kwa kuwatumia binadamu wengine kama wanyama. Kwa maneno mengine, kwao watumwa walikuwa nyenzo iliyounganishwa kwenye uzalendo na kuwafanya wawe taifa kubwa na lenye nguvu za kiuchumi na kijeshi.
Hao walitumia binadamu kufikia malengo yao. Sisi hatuwezi kuwatumia watumwa kufikia malengo ya kuifanya Tanzania kuwa taifa la kupigiwa mfano kiuchumi, lakini tumeshindwa kuwatumia punda na wanyamakazi wengine ndani ya uzalendo wetu kubadili kilimo chetu.
Lakini tunapozungumza uzalendo, hatuna budi kujua ni mambo gani yanayoleta uzalendo. Wale waliosoma filosofia wanatambua nini maana ya uzalendo na namna uzalendo unavyojengwa. Kwa lugha nyepesi ningependa niyaeleze machache katika hayo mengi yanayosaidia kujenga uzalendo.
Uzalendo unaanzia kwa watu wanaotambua aina ya jamii au nchi wanayotaka kuijenga. Kama lengo lao ni kuona jamii au nchi yao inakuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani, hiyo inakuwa dira yao kuu. Sasa katika kuifikia dira hiyo, ndipo wanapoweka misingi ya kufuatwa ili, kwa kufanya hivyo, basi iwadie siku ya kutimilizwa kwa maono yao.
Pili, uzalendo kama ilivyo tabia nyingine, ni suala linalopaswa kujengwa ndani ya akili na mioyo ya watu wakingali wadogo. Huwezi kujenga moyo wa uzalendo kwa watu waliokwishakuwa wakubwa. Katika hili utaona kuwa sehemu nzuri ya kuanza kujenga uzalendo ni katika familia zetu, shule hadi vyuoni.
Wale waliosoma kwenye miaka ya 1960, 1970, 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 wanatambua namna Serikali yetu ilivyojitahidi kupandikiza mbegu ya uzalendo miongoni mwa watoto wa nchi hii. Sisi wa miaka hiyo tulifundishwa, tulikaririshwa, tuliaminishwa maadui wa nchi yetu. Kwenye nyimbo za mchakamchaka tuliimba kwa kuwataja maadui wa Tanzania. Tukaambiwa nini cha kuwafanya maadui wetu.
Tulicheza magwaride mbalimbali ya chipukizi yaliyopambwa na nyimbo za uzalendo. Tukaimba nini kilichopaswa kuwapata wale wote wasiopenda kufanya kazi. Uzalendo ukaendelea kufundishwa katika shule za sekondari, vyuo na hata katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Kwa ufupi kabisa, uzalendo unajengwa. Uzalendo ni tabia. Tabia ni tokeo la mazoea. Hili tunda la uzalendo linapatikana kuanzia kwa watoto wadogo wanaofunzwa kuipenda nchi yao na kuwa tayari kuifia.
Tatu, uzalendo unajengwa kwa wapigiwa kura kuishi kadiri wanavyowahubiria wapigakura wao. Mfano mzuri wa hili tunaweza kuuona kwa waasisi wa Taifa letu. Maisha ya viongozi wengi wa wakati huo yalishabihiana na yale waliyowaeleza wananchi. Maisha na tabia za viongozi kama Mwalimu Nyerere, Sheikh Abeid Karume, Mzee Kawawa, Mzee Edward Sokoine na wengine wengi wa aina yao yalitosha kabisa kuwaaminisha wananchi na kuwafanya waishi kadiri walivyotakiwa. Kiongozi akihubiri uzalendo, lakini yeye mwenyewe akawa mwizi, wananchi watampuuza tu.
Hili tumeliona baada ya kulegezwa kwa masharti na kutupwa kwa miiko ya uongozi. Kwa kasi ya aina yake, wale waliokuwa mbele kuhubiri Ujamaa wakawa ndiyo mabepari wakuu. Mashirika ya umma yalipouzwa wakajitwalia mali nyingi. Wananchi kwa kuyaona hayo nao wakawa hawana jingine isipokuwa kuachana na uzalendo maana waliona wanadanganywa.
Nne, uzalendo unajengwa na msingi mkuu wa usawa. Huu usawa unaweza kuwa kwenye uchumi, kwenye haki, kwenye kuheshimiana na kwa ujumla wake lazima upatikane katika kutendeana haki.
Wananchi wanaopigwa virungu na polisi bila kuwa na makosa ya kusababisha wapigwe, wanaichukia Serikali. Wanajiona hawana thamani na kwa maana hiyo kuwahubiria uzalendo ni kazi bure.
Uzalendo unajengwa pale inapoonekana kuna usawa mbele ya vyombo vya utoaji haki. Hili kwa kiasi kikubwa limeanza kuleta matumaini katika Serikali ya Awamu ya Tano. Zamani zile ilijulikana mahabusi ilionekana kuwa ni sehemu ya makabwela, lakini leo walau inaonekana hata wasio makabwela nao kumbe wanaweza kuingia huko. Bila usawa hakuna uzalendo.
Pengine haitakuwa vema kwangu kuyazungumza haya bila kugusia matukio kama matatu hivi. Mosi, kuna tukio la kufariki dunia kwa wanafunzi zaidi ya 30 katika ajali ya basi mkoani Arusha mapema mwaka huu. Pili, kuna tukio la kuuawa kwa kupigwa risasi polisi wanane eneo la Jaribu Mpakani mkoani Pwani.
Tukio la tatu ni la kuuawa wanajeshi wetu 14 nchini DRC ambako walikwenda kulinda amani. Nimeishi na wanajeshi. Nimeshiriki nao kumng’oa Kanali Bakar kule Anjouan, Comoro. Najua umuhimu wa watu hawa. Wanastahili kuenziwa na kuoneshwa upendo kwa kila namna. Wakati sisi mitaani tukila na kunywa, wao wanashinda kutwa na kukesha wakiilinda mipaka yetu.
Matukio haya matatu hayajumuishi raia wenzetu waliofariki dunia katika ajali mbalimbali nchini.
Kwa kuyatazama matukio haya matatu, unaona yamekuwa matukio yaliyowagusa Watanzania wengi. Lile la kuuawa polisi kuna wananchi walikamatwa kwa tuhuma za ‘kushangilia’ kuuawa kwao. Kama Taifa tulipaswa kujiuliza kwanini wananchi wafurahie polisi kuuawa? Bila shaka kuna tatizo, tena si tatizo dogo. Wananchi kadhaa wanawaona polisi kama watu waonevu wasiokuwa na huruma. Wanajua namna wanavyosumbuliwa mitaani na vituoni. Hili Amiri Jeshi Mkuu alishalitolea maelekezo. Kazi imebaki kwa IGP na timu yake kuhakikisha imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi inarejeshwa. Vyovyote iwavyo, bado kuuawa kwa polisi ni kosa kwa sababu kunasababisha upungufu wa walinzi hao wa raia na mali zao.
Kwa ujumla wa matukio haya, naona kuna chembechembe za kufifishwa kwa uzalendo. Bado wananchi kadhaa wanajiuliza maswali mengi. Kwa mfano, kwanini msiba ule wa watoto kule Arusha, Serikali haikutangaza japo siku moja ya maombolezo – kupeperusha bendera nusu mlingoti na kazi zikiwa zinaendelea kama kawaida?
Wananchi wanajiuliza, kwanini mauaji ya wanajeshi wetu 14 kule DRC hakujapewa siku ya maombolezo ya kitaifa kama sehemu ya kuonesha uzalendo kwa Watanzania hao wenzetu pamoja kwa dhima kubwa waliyokuwa nayo ya kuwalinda Waafrika wenzetu? Bado kuna wananchi wanajiuliza, kwanini polisi wale wanane waliagwa kwa staili ambayo haikuleta msisimko kitaifa? Je, hawa polisi na wanajeshi hawakustahili hata wenzao kuonekana wamevaa vitambaa vyeusi?
Kama wacheza mpira wenyewe hufanya hivyo anapokufa mwenzao, kwanini isiwe hivyo kwa watu hawa muhimu sana katika usalama na ulinzi wa Taifa na majirani zetu? Je, wafe wangapi ili tuguswe? Hili si langu, lakini linaulizwa mitaani, mbona Amiri Jeshi Mkuu hahudhurii misiba hii mizito? Nasisitiza kuwa hili swali la mwisho si langu. Ni la wananchi wazalendo wanaouliza huku mitaani na hata kwenye mitandao ya kijamii.
Na sijui kwanini wanauliza maana tulikuwa na Amiri Jeshi Mkuu aliyehudhuria misiba mingi. Akasemwa kweli kweli. Kaja huyu wa sasa, watu wameanza kuhoji kwanini hahudhurii. Sijui binadamu wanataka nini, lakini nilicho na hakika nacho ni kuona wanakuwa na viongozi wanaowaunganisha ili wajione wamoja katika Taifa lililo moja, Taifa lenye kupambwa na sare za Taifa badala ya vyama vya siasa hasa kwenye matukio ya kitaifa.