📌 MD Nyamo-Hanga na Viongozi wengine (TANESCO) wakagua Maendeleo ya ujenzi wa Mradi huo na kuahidi kuendelea kuusimamia hadi ukamilike

📌Megawati 1175 kutoka kwenye mashine tano zilizokwishakamilika zinazalishwa na tayari zimeungwa kwenye Gridi ya Taifa

📌 Utekelezaji wake kwa Ujumla wafikia asilimia 99.55

Na. Agnes Njaala, Rufiji

Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) Desemba 19, 2024 umetembelea Mradi wa Kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere kujionea kasi ya maendeleo ya ujenzi unavyoendelea na kuweka mkazo kwa wasimamizi kuhakikisha usimikaji wa mashine nne zilizobakia unafanyika ipasavyo ili umeme utakapozalishwa uingizwe kwenye Gridi ya Taifa kwa mafanikio yatakayoleta tija inayotarajiwa kwa watumiaji wa umeme.

Akizungumza wakati wa Ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Mha. Gissima Nyamo-Hanga amesema kwasasa jumla ya mashine tano (05) zimekamilika kwa asilimia 100 yaani mashine namba 9, 8, 7, 6 na 5 na tayari zimeanza uzalishaji wa umeme.

” Tumetembelea mradi huu kujionea shughuli zinazoendelea na kuweka msisitizo wa usimamizi bora kwa maeneo ambayo bado hayajakamilika ambapo utekelezaji kwa ujumla umefikia asilimia 99.55 huku shughuli za uzalishaji wa umeme zikiwa zimeanza na wastani wa megawati 1175 zinazozalishwa kutoka mashine tano za mradi huu zimeingizwa kwenye grid ya Taifa ” ameeleza Mha. Gissima.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa usimikaji wa mashine namba 4 umefikia asilimia 100 ambapo kwasasa mashine hiyo ipo kwenye majaribio huku mashine namba 3 ikiwa kwenye asilimia zaidi ya 87 za usimikwaji, asilimia ambazo zinadhihirisha kuwa kiwango cha utendaji kazi ni kizuri .

Amewahimiza wasimamizi wa mradi kuhakikisha wanaendeleza bidii kusimamia maeneo ambayo bado hayajakamilika kuhakikisha kazi inafanyika kwa viwango vilivyoainishwa wakati wa usanifu wa mradi huo.

” Niwaombe msimamie vizuri kuhakikisha ufanyaji kazi wa mashine unakuwa ni mzuri ili umeme unaoendelea kuzalishwa unapoungwa kwenye Gridi ya Taifa usilete changamoto yoyote ” amesisitiza Mha. Gissima.

Katika hatua nyingine, Gissima ameishukuru , Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Nishati na viongozi wake wote kwa namna ambavyo mara zote imeunga mkono kwa kutoa fedha na ushirikiano katika kusimamia utekelezaji wa mradi mpaka kufikia hatua iliyopo sasa pamoja na miradi mingine mingi inayoendelea nchini .

” Ninawaahidi watanzania wenzangu kuwa, sisi kama viongozi wa TANESCO tutahakikisha tunasimamia mradi huu kwa dhati na umadhubuti mkubwa ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuleta tija ya kiuchumi na kijamii katika taifa letu la Tanzania” alihitimisha Mha. Gissima.

Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere tayari umeanza kuleta matumaini makubwa ya Kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini ikiwa ni kati ya Juhudi kubwa za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt Samia Suluhu Hassan.