Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imekamilisha ujenzi wa daraja la Berega lililopo Barabara ya Berega – Dumbalume lenye urefu wa meta 140 na upana meta 11 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Kukamilika kwa daraja hilo kumeweza kuunganisha Wilaya ya Kilosa, Gairo, Kiteto na Kilindi na hivyo kuondoa kero ya miaka mingi iliyokuwa ikiwakabili wananchi katika shughuli za usafiri na usafirishaji ikiwemo kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilosa Mhandisi Winston Munyanga, alisema ujenzi wa Daraja la Berega umekamilika kwa asilimia 100, pamoja na maboresho ya barabara ya Berega – Dumbalume yenye urefu wa Km 7 ambayo yamegharimu Sh Bilioni 7 na kuondoa kero ambayo wananchi wa wilaya hiyo na zile za jirani walikuwa wanazipata.
”Kwa sasa ujenzi wa daraja la Berega umekamilika na tumefanikiwa kuunganisha Wilaya ya Kiteto, Gairo, Kilosa na Kilindi pamoja na kurahisisha huduma za kijamii na kiuchumi kwa kuzifikia kwa urahisi hasa shule pamoja na hospitali zilizopo ng’ambo ya daraja hilo”, amesema Mhandisi Winston.
Mhandisi Winston ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa ongezeko la bajeti kwa Wakala wilayani Kilosa, ambayo imewezesha kutekeleza mradi huo mkubwa wa ujenzi wa daraja la Berega.
Naye Diwani wa Kata ya Berega, Filemoni Maube ameishukuru serikali kwa kukamilisha ujenzi wa daraja hilo, kwani hapo awali kipindi cha masika wananchi wa kata hiyo walikuwa wanapata tabu katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi na iliwalazimu kusubiri maji yapungue ndipo waanze kupita.
”Tunaishukuru sana serikali kwa kukamilisha ujenzi wa daraja hili, kwa sababu sasa tuna uhakika wa kupita hapa katika vipindi vyote tofauti na hapo awali, wanafunzi wataweza kufika shuleni, wagonjwa watafika hosptalini pamoja na kusafirisha mazao yetu kwa urahisi,” amesema diwani huyo.
Gideon Mshala, Mkazi wa Kijiji cha Berega ameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ambalo limewasaidia wananchi wa Kata ya Berega, Kiegeya na maeneo jirani kuvuka kwa urahisi na kuzifikia huduma za kijamii tofauti na hapo awali ambapo daraja lilikuwa limekatika.