Na Albano Midelo, JamhuriMedia,Songea

Serikali inatarajia kuanza mradi wa ujenzi wa barabara ya lami nzito ya mpakani mwa Tanzania na Msumbiji yenye urefu wa kilometa 124 kutoka Likuyufusi hadi Mkenda wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati anatoa maelezo ya kuanza kwa mradi huo kwa Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango ambaye yupo mkoani Ruvuma katika ziara ya kikazi ya siku tano.

Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Peramiho,Mhandisi Kasekenya amesema Ruvuma ndiyo Mkoa pekee nchini uliopo mpakani ambao barabara zake hazijaunganishwa kwa lami na nchi jirani ambapo amesema barabara hiyo iliyopo kwenye Ilani ya CCM,sasa inatekelezwa na serikali ya Sita katika mwaka huu wa fedha.

“Mheshimiwa Makamu wa Rais na wananchi wa Jimbo la Peramiho napenda kuwahakikishia kuwa Rais Samia Suluhu Hassan mwaka huu wa fedha, ameshatoa kibali cha kuanza kujenga barabara ya Likuyufusi-Mkenda na Mkandarasi ameshapatikana kuanza kujenga kipande cha kwanza chenye urefu wa kilometa 60 toka Likuyufusi hadi Muhukuru’’ amesema.

Naibu Waziri huyo wa Ujenzi na Uchukuzi amesema kinachosubiriwa hivi sasa ni kusainiwa mkataba wa kuanza ujenzi wa barabara hiyo na kwamba taratibu zote za kuanza ujenzi wa barabara hiyo zimekamilika.

Amesema katika utekelezaji wa mradi huo serikali imetoa shilingi bilioni 60 kuanza kujenga barabara hiyo,pia serikali imetoa shilingi bilioni 22 kujenga daraja imara la Mkenda kwenye mto Ruvuma ili kuwezesha kupita magari makubwa na madogo.

Amesema serikali pia imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 18 kujenga daraja katika eneo la Mitomoni katika Mto Ruvuma linalounganisha wilaya za Songea na Nyasa na kwamba kinachosubiriwa hivi sasa ni kusainiwa mkataba wa kuanza ujenzi wa daraja hilo.

Akizungumza na wananchi hao wa jimbo la Peramiho Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango amemuagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kusaini mkataba huo ndani ya mwezi Julai mwaka huu kwa kuwa kila kitu kimekamilika na Mkandarasi amepatikana hivyo mradi uanze kutekelezwa mara moja.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo mkoani Ruvuma katika ziara kikazi ambapo hadi sasa amekagua miradi na kusalimiana na wananchi katika wilaya za Songea na Namtumbo.