Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Bw. Gabriel Migire amesema kufikia Januari, 2023 Bandari kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani itaanza kuhudumia mizigo itakayotoka Bandari ya Dar es Salaam na kuelekea mikoa mbalimbali nchini na nchi jirani.
Katibu Mkuu Migire ameyasema hayo wakati alipokagua ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 15 kutoka Vigwaza mpaka Bandari Kavu ya Kwala inayojengwa kwa kiwango cha zege na Kampuni ya Stem kutoka Jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha utendaji wa bandari unaboreshwa ili kuvutia wateja wengi zaidi.
“Kuanza kutumika kwa Bandari hii ya Kwala itasaidia kupunguza msongamano wa mizigo na magari makubwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwani bandari hii itahifadhi makasha ya kwenda nchi Jirani kama vile Burundi, Rwanda, DRC Congo, Uganda , Zambia na Malawi”, amesisitiza Bw. Migire.
Kwa upande wake, Mhandisi Joseph Marandu kutoka SUMA JKT anayesimamia ujenzi wa Bandari ya Kwala amesema kuwa ujenzi mradi wa barabara hiyo utakamilika mwishoni mwa mwezi huu na kazi zilizoendelea kutekelezwa kwa sasa ni za uwekaji wa taa, kamera pamoja na kumalizia kuweka sakafu ngumu kwa ajili ya kuhifadhia makasha.
Naye, Mhandisi Jacob Mambo kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), amesema katika utekelezaji wa mradi huo mradi umezingatia mzigo mkubwa utakapohifadhiwa kutoka bandarini hivyo wakala umehakikishia unakamilika kwa viwango..
Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Kavu ya Kwala unategemewa kupunguza kwa kiasi kikubwa foleni ya malori katika Bandari ya Dar es Salaam na utarahisisha utendaji wa bandari hiyo kwani mizigo itaweza kushushwa kwenye meli na kupelekwa kwenye bandari hiyo kavu.