Nilipokuwa muhula wa mwisho kumaliza masomo ya shahada yangu ya kwanza, siku moja niliingia katika mjadala mzito na mama yangu mzazi. Mama alikuwa akishusha pumzi kuona kuwa mwanaye sasa ninaelekea kukamilisha ngwe ya elimu ya juu. Mawazo na kiu yake kubwa ilikuwa ni kuona natafuta ajira mapema, kitu ambacho nilitofautiana naye na hivyo kuzusha malumbano ya kihoja na kimtazamo.
Wakati mama yangu akiamini mafanikio kupitia kuajiriwa, mimi niliamini (na ndivyo ninavyoamini na kuiishi imani hiyo), kuwa ukombozi wa kweli wa kiuchumi na kifedha utakuja kwa kuanza kujiajiri na hatimaye kuwa mwajiri wa wengine katika biashara ama shughuli zangu mwenyewe.
Haikuwa kazi rahisi kuubadilisha mtazamo wa mama, hivyo nililazimika kutumia ushawishi wa hali ya juu na mifano hai. Kwa bahati nzuri nilikuwa nikibishana naye nikiwa tayari nimeshapata kufanya ujasiriamali na yeye alikuwa shuhuda wa namna nilivyofanikiwa na baadaye kufilisika kabla ya kuanza upya.
Hili tukio la kufilisika ndilo lililokuwa linampa ‘presha’ mama yangu, kwa sababu alinihoji maswali mengi (kwake yalionekana ni magumu lakini kwangu yalikuwa ni mepesi mno). “Mwanangu, biashara ni kama kubahatisha, hivi kweli na elimu yako hii unataka kuendelea kujiajiri? Je, itakuwaje ukifilisika tena? Huoni kama utakuwa mtu wa kubahatisha licha ya kuwa ni msomi? Kwa nini usitafute ajira uwe na uhakika na mshahara wako kila mwezi?”
Bahati mbaya mimi nina ndugu na jamaa wengi ambao wanaamini mno katika mfumo wa kuajiriwa (huenda Watanzania wote wako hivyo)! Nikiwa nimepangua (kwa ushindi) mjadala huo na mama, nikakutana na ndugu yangu mwingine ambaye alinishangaa kuona nimebadili kutoka masomo ya sayansi kwenda kusoma masomo ya biashara. Kidato cha tano na sita nilisoma masomo ya sayansi (Chemistry, Biology na Physics) lakini ngazi ya chuo kikuu, niliukana udaktari na kugeukia masomo ya biashara.
Yeye (ndugu yangu) alinipa kauli ifuatayo ambayo hadi leo huwa ninaihesabu kuwa ni ya kitumwa. “Umeacha fani ya sayansi umekimbilia fani ya biashara, utapata shida sana. Fani za biashara siku hizi hazina ajira, wanaozisomea ni wengi mno. Ungebaki sayansi ungekuwa na uhakika wa ajira yako bila shida.”
Niliamua ‘kumpotezea’ kwa sababu mawazo yake na yangu niliona ni kama mbingu zilivyo mbali na nchi. Anawaza niajiriwe wakati mimi ninaumiza kichwa jinsi ya kuwapata wafanyakazi bora niwaajiri!
Kiukweli nchi hii imekuwa ikizalisha wasomi bandia kutokana na misukumo hasi.
Wengi wanasoma fani ambazo si za miito wala karama (talents) zao, kwa sababu ya ama matarajio ya upatikanaji wa ajira ama upatikanaji wa mikopo. Ndiyo maana taifa hili linayumba na kuyumbishwa kila siku, kwa sababu aliyetakiwa kuwa mfanyabiashara unamkuta kwenye udaktari, aliyepewa kipaji cha ualimu unamkuta benki na haiyumkini tuna rundo la walimu katika mifumo yetu ya elimu ambao walitakiwa kuwa wanajeshi! (Yale yale ya mwalimu kuripotiwa kucharaza viboko kwa kutumia waya!)
Fikra hizi za kusomesha watoto ama kusoma ili kuajiriwa ndizo zilizojaa katika fahamu za Watanzania wengi. Kwa bahati mbaya sana, kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kisiasa na uchumi wa dunia; matumaini ya kila anayehitimu masomo yake kuajiriwa yanazidi kuyeyuka siku hadi siku. Hapa nchini Tanzania hadi sasa, kuna nafasi chache sana za ajira ikilinganishwa na idadi ya wasomi inayotapishwa na rundo la vyuo vikuu na vya kati.
Ukiacha hilo la ajira kuwa chache, bado kuna changamoto kwa wale wanaobahatika kuajiriwa. Changamoto hii ni kutotosheleza kwa mishahara (na marupurupu?) inayotolewa ikilinganishwa na hali ya maisha na malengo anayokuwa nayo mwajiriwa.
Tena lipo jambo linalozidisha mbinyo na misongo miongoni mwa wasomi wetu kutokana na imani ambazo huwa nazo kuhusu maisha. Wengi wawapo masomoni huwa na ndoto za mchana za kuajiriwa leo na kutajirika kesho! Wanapoingia kazini na kukutana na uhalisia kuwa mambo si rahisi kama wanavyodhani, hapo ndipo kinapoanza kizaazaa! Udokozi, wizi na ufisadi huanzia hapo. (Ingawa kuna kazi hazina cha kuiba)!
Kwa hiyo, wanaoajiriwa na wale wanaokosa ajira, wasomi na wasiosoma, wote wanajikuta katika changamoto moja kubwa – ‘msongo wa maisha’. Hivyo, mtu apende, asipende analazimika kufikiria tofauti kujiokoa. Suluhisho kubwa kwa changamoto hizi ni ujasiriamali.
Hii ni dhahiri kwa sababu mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yanasababisha matatizo, na matatizo siku zote ni fursa. Uhai wa ujasiriamali unategemea uwepo wa fursa. Ni bahati ilioje kuwa dunia ya leo (ikiwamo Tanzania) imekuwa na fursa nyingi za kiuchumi na kibiashara kuliko wakati mwingine wowote tangu kuasisiwa kwa taifa hili. Ni suala la kujizoeza kufikiri na kuona tofauti na wengine.