Ujasiri wa leo ni tumaini la kesho, hebu fumbua macho yako uone. Mungu anakuonesha mamilioni ya fursa siku ya leo. Mwandishi Robinson Maria anasema, hakuna anayeweza kurudi nyuma na kuanza mwanzo mpya, lakini yeyote anaweza kuanza leo na kutengeneza mwisho mpya.
Katika maisha tumwombe Mungu vitu vitatu; Kwanza kutambua na kukubali mambo ambayo hatuwezi kubadili. Pili, tuombe ujasiri wa kubadili tunayoweza kubadili. Tatu, tuombe hekima ya kutambua tofauti ya mambo tunayoweza kubadili na tusiyoweza kubadili. Yasiyo na suluhisho la kibinadamu tuyakabidhi mikononi mwa Mungu.

Mungu akiwa dereva wa maisha yako, shetani haombi lifti. Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kukupa mafanikio unayoyataka kwa sekunde moja, lakini anakutaka kwanza uoneshe juhudi za kuyataka mafanikio unayoyataka. Mwandishi Henrieta C. Mears anasema hivi; Mungu anatuacha tushindwe katika jambo ambalo si la msingi ili tuweze kufanikiwa katika jambo ambalo ni la msingi.
Kuna nyakati fulani, mtu anahisi kuwa hawezi kuona njia kwa urahisi. Anawahi kuhitimisha kwa kusema, ‘Hapa siwezi’. Kumbuka: Pale unaposema, hapa nimefika mwisho, Mungu anasema ‘Huu ni mwanzo mpya’. Mwandishi na mshairi wa Marekani, Albert Laighton, anatutia moyo kwa ujumbe huu, ‘Pale mwanadamu anapoona majani yamekauka, Mungu anaona maua mazuri yamechanua.’

Mwenyezi Mungu ni mtaalamu wa kuwapa watu mwanzo mpya. Daima Mungu yupo karibu na kila mtu, lakini siyo kila mtu yupo karibu na Mungu. Mwombe Mungu akusaidie kuyaona maisha ya duniani kama anavyoyaona yeye mwenyewe. Kama umekata tamaa kwa vile kuishi na watu ni kazi, ujue kwa Mungu hakuna lisilowezekana. Kama umekata tamaa kwa sababu ya kupoteza nafasi yako ya kazi ujue, kwa Mungu hakuna lisilowezekana, kama umekata tamaa kwa vile huna hata senti mfukoni, ujue kwa Mungu hakuna lisilowezekana.
Kama umejikwaa nyanyuka, kama umelala amka, kama unashangaa shangaa, changamka, kama umekaa, simama na kama unatembea kimbia. Kanuni mojawapo ya kufanikiwa katika maisha ni kuona mbele. Leo na kesho yako inategemea mtazamo ulionao kwa sasa.
Niseme, kwamba inawezekana kabisa ukafanikiwa kuishi maisha unayoyapenda lakini pia inawezekana kabisa ukafanikiwa kuishi maisha usiyoyapenda.
Uchaguzi wa maisha yako unao wewe mwenyewe. Nakusihi; chagua mtazamo sahihi ili uishi maisha sahihi, maisha ni swali linalojibiwa kwa jibu la uthubutu. Ukiamua kuthubutu utaweza, usipoamua hutaweza kamwe.
Mwanamuziki Bob Dylan siku moja aliulizwa swali na mtoto wake. Mtoto wake alimuuliza, Baba unapenda sana kuimba, je, siku ukilewa na sifa za watu halafu ukawa unaimba vibaya vibaya utafanyaje? Baba yake alimjibu hivi, nitaacha kuimba. Kama unaishi kwa kuyajaribu maisha acha! maisha hayajaribiwi.
Mafanikio siyo ajali, ni kujifunza, kuvumilia, kujituma, kujitoa mhanga na kikubwa kuliko vyote ni kupenda unachokifanya. Mafanikio yapo hayawabagui, mafanikio bado yanakungoja usiyakimbie. Tumia muda mwingi kubuni namna ya kusonga mbele na namna ya kutorudia makosa ya nyuma.

Wakati mwingine watu hujibagua wenyewe wasifanikiwe. Wanafanya hivyo kwa kujua au kwa kutokujua. Tafadhali usijione kama mtu wa kushindwa. Mafanikio hayategemei kile ulichonacho au usichonacho kwa sasa. Yanategemea namna unavyotumia kile ulichonacho ili kupata usichonacho.
Kila mtu ana kitu muhimu kinachoweza kutumika vizuri kikamfanikisha haraka. Kitu hicho si pesa, elimu, umaarufu, ajira n.k. Kitu hicho ni nia ya dhati. Aliye na nia ya dhati ya kufanikiwa na anajua kuwa ana nia ya kufanikiwa atafanikiwa. Arnold Schwarzenegger anasema; Huwezi kuipanda ngazi ya mafanikio ukiwa umeweka mikono mfukoni.
Maisha ni safari ukisimama hakuna kinachoenda sawa. Baadhi ya watu wanajizuia kufanikiwa bila ya kujua kwamba wanajizuia kufanikiwa. Ifahamike kwamba, mafanikio sio kwa ajili ya wasomi tu au kwa wafanyabiashara wakubwa. Hapana. Mafanikio yanapatika kwa kila mtu anayeyataka. Ndugu msomaji, bado una fursa ya kufanikiwa kiroho, kiuchumi, kimwili, kifamilia, kimaadili na kiafya.
Jiamini. Usiruhusu fursa yoyote iende bila kuitumia. Uamini uwezo ulinao kwa sasa. Ukijishusha thamani na ulimwengu utakushusha thamani. Tafadhari, usijishushe thamani jithamini. Kufanikiwa ni mchakato wa kubadilika kutoka hali ya kujiona huwezi na kuelekea hali ya kujiona unaweza.

Kumbuka; ugumu wa maisha au wepesi wa maisha ni chaguo la mtu. Hatukuumbwa tufe maskini, bidii ni mama wa bahati njema. Mlima wa umaskini utaondoka katika maisha yako endapo utajitambua kwamba wewe ni nani, na unataka wewe uwe nani baada ya miaka 10, 20, 30 ijayo.
Kila mlango mmoja unapojifunga, mlango mwingine unafunguka, hata hivyo tatizo letu ni kwamba tunapoteza muda mwingi kuangalia kwa masikitiko mlango uliojifunga kiasi kwamba hatuoni mlango uliofunguka. Bado unayo fursa ya kufanikiwa, dunia inasubiri kwa shauku kubwa kuuona uwezo wako.
Kumbuka hukuumbwa kwa bahati mbaya. Maisha siku zote yamejaa hatari tupu, lakini kuna hatari moja kubwa ambayo unatakiwa kuizuia kwa gharama yoyote na hiyo ni hatari ya kutofanya lolote. Maisha ni malengo, kama unapenda maisha yako yawe na mvuto yape mwelekeo.

Wanaume na wanawake walioingia kwenye historia ya mafanikio ni wale wanaoishi na walioishi maisha yanayoongozwa kwa malengo. Bila kujali sababu, watu wanaoongozwa na woga mara nyingi hupitwa na fursa kubwa kwa sababu wanaogopa kuchukua hatua. Woga ni kifungo kikubwa ambacho mtu hujifunga mwenyewe.
Tofauti hii kubwa ya pato miongoni mwa watu, inashinikiza mmomonyoko wa maadili ya kijamii kama kuwadharau na kuwabeza maskini. Umaskini ni fedheha, umaskini ni mzigo, umaskini unanuka. Tuuchukie umaskini.
Mwanafalsafa wa Ufaransa, Francois- Marie Arouet, anasema; Mwenyezi Mungu alitupatia zawadi ya maisha, hivyo ni juu yetu kujipatia zawadi ya kuishi maisha mema. Mwenyezi Mungu anapenda tufanikiwe. Tunasoma hivi katika Maandiko Matakatifu, Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo (3Yoh1:2).

Kila kukicha hakuna asiyekabiliwa na zoezi la kufanya uchaguzi fulani. Tunatakiwa kuchagua kati ya kulala au kuamka. Kuchagua kuwahi mahali fulani au kuchelewa. Kuchagua kuwa na furaha au hasira. Kufanya uchaguzi ni jambo lisiloepukika. Methali ya Kifaransa inatukumbusha kwa ujumbe huu; ‘Yeye anayengojea kuvaa viatu vya marehemu anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu.’
Nilichojifunza katika maisha ni kwamba ni rahisi kufanikiwa kuliko kutokufanikiwa. Huwezi kushindwa kufanikiwa kiroho, kimwili, kiafya, kifamilia, kimaadili na kiuchumi. Labda uamue mwenyewe ya kwamba hutaki kufanikiwa. Jifunze kuwa rafiki wa matumaini, kila siku washa mshumaa wa matumaini, maisha ni matumaini na mafanikio ni matumaini.

Huwezi ukaishi kwa kukosa matumaini halafu ukafanikiwa. Ni jambo ambalo halitakaa litokee kwa binadamu yeyote yule. Mafanikio yanavutwa kwa shauku ya matumaini. Ishi kwa matumaini kama kucha. Sifa ya kucha ni kwamba, haijalishi unaikata mara ngapi, kila unapoikata inajiandaa kuota tena.
Binafsi sifahamu unaishi maisha ya namna gani, lakini ni shauku yangu nikuone unaishi maisha ya matumaini. Iko hivi, anayeweza kuyaboresha maisha yako ni wewe mwenyewe, wewe mwenyewe unaweza kuamua kuishi maisha unayoyataka. Mwanasayansi Charles Darwin anatufundisha hivi; ‘Binadamu anayethubutu kupoteza saa moja kwa kukaa bure, bado hajafahamu thamani ya maisha yake’.

Na WILLIAM BHOKE

0719700446