Alhamisi Oktoba 16, mwaka huu napigiwa simu na Ofisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN), Stella Vuzo, kuwa nimeteuliwa kwenda kuripoti kazi zinazofanywa na Umoja huo katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Napokea habari hiyo kwa furaha kwa sababu sikutarajia kutembelea hifadhi hiyo kubwa kuliko zote na yenye vivutio vingi nchini na Afrika Mashariki kwa rekodi za sasa.
Ijumaa ya Oktoba 17, mwaka huu, naitwa katika Ofisi za UN zilizopo Mtaa wa Shaaban Robert mkabala na Mtaa Garden jijini. Napewa maelezo ya awali ya cha kufanya nitakapofika katika hifadhi hiyo, nakabidhiwa tiketi ya ndege kwa ajili ya safari ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Nilikuwa na Mwandishi wa Habari wa Daily News, Rose Athman.
Stella anatueleza kwamba, “Lengo la safari hiyo ni kuitangza siku ya Umoja wa Mataifa inayoadhimishwa Oktoba 24 kila mwaka. Na mwaka huu Umoja wa Mataifa unatimiza miaka 69 tangu uanzishwe mwaka 1945, hivyo ameona kwamba ni bora kuadhimisha siku hiyo kwa kutembelea miradi ya UN.
UN, kupitia Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Shirika la Mendeleo la Marekani, imeanzisha mradi unaoitwa Spanest unaoshughulika na kuzuia ujangili dhidi ya tembo katika Hifadi ya Taifa ya Ruaha.
Safari inaanza
Naamka saa 10 alfajiri siku ya Oktoba 21, najiandaa kwa ajili ya safari nyumbani kwangu Ubungo Kibangu, baada ya maandalizi natoka nje na kutafuta usafiri. Kwa wakati huo nililazimika kuchukua usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda hadi katika kituo cha Ubungo Darajani.
Kituoni nakutana na abiria wengi kila mtu akiwa katika pilikapilika za kutafuta usafiri ili kuwahi majukumu. Inanichukua dakika 35 hadi kupata basi la kutoka Ubungo kwenda Gongo la Mboto.
Napanda gari hilo saa 12:45 tunapita katika barabara ya Mandela. Barabara hii inasifika kuwa na foleni kubwa mara kwa mara kutokana na kuwa na malori mengi yanayotoka katika Bandari ya Dar es Salaam.
Daladala inashika Barabara ya Nyerere kuelekea katika ‘Terminal One’ (Uwanja Na. 1) wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Mungu ni mwema hakuna foleni, natumia dakika 45 kufika JNIA.
Hapo uwanjani, naungana na mwandishi wenzangu Rose na Mkuu wa Msafara Stella ambao wamefika mapema, nawaona pia abiria wengine kutoka katika mataifa mbalimbali wakiwa uwanjani hapo.
Saa 2:30 asubuhi tunatangaziwa kuingia katika ndege yenye uwezo wa kubeba abiria wanane. Ndani yake raia wa kigeni walikuwa watano na wengine ni Watanzania. Najiuliza maswali mengi kwa takwimu hizo kwamba hivi Watanzania wana utamaduni na kutembelea mbuga zetu za wanyama?
Saa 2:45 rubani akiwa kasimama nje ya mlango wa abiria anatutangazia kuwa safari yetu sasa imeiva, kabla ya kuingia ndani ya ndege na kukaa katika kiti chake na kuirusha ndege ambayo ilitua Uwanja wa Hifadhi ya Ruaha saa 3:50 asubuhi.
Tunashuka katika uwanja huo, lakini kwa kuwa hatukuwahi kuonana na mwenyeji wetu tunapeana majukumu ya kutupa macho huku na kule ili kumuona. Ghafla kwa mbali naliona gari aina ya Land Cruizer VX nyeupe ubavuni imeandikwa UNDP Spanest likija kwa kasi upande wangu na kisha linasimama jirani yangu. Nalisogelea.
Katika gari hilo anashuka kijana mrefu maji ya kunde, mtanashati mwenye asili ya Kimaasai, akiwa amevaa danglish na shati liloandikwa katika mfuko Spanest ananifuata na kuniuliza.
“Kaka habari yako” namjibu “safi kaka” “naitwa Godwell Meing’ataki, mimi ni Mratibu wa Spanest nadhani wewe ni mgeni wangu”, namjibu “inawezekana” kabla sijamaliza akadakia akisema, “Ok umetoka UN”, nikamjibu “ndiyo”, akasema “basi mimi ndiyo mwenyeji wenu. Dereva aliyejitambulisha kwa jina la Zuberi anaendesha gari hadi katika Ofisi ya Mhifadhi Mkuu wa Ruaha.
Ofisini kwa Mhifadhi Mkuu
Baada ya kujitambulisha, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha naye anajitambulisha kwa jina la Dk Christopher David Timbuka. Anaanza kwa kueleza kwamba hifadhi hiyo ni moja ya maeneo machache Tanzania ambayo yapo katika hali ya asili bila kuharibiwa na shughuli za kibinadamu.
Hifadhi hii ina utajiri mkubwa wa mimea na wanyama adimu kama vile tandala wakubwa na wadogo, ambao hawapatikani katika hifadhi nyingine hapa Tanzania. Utajiri huu ni kuvutio kukubwa cha watalii.
Anaendelea kusema kwamba “Hifadhi hii ipo kwenye eneo ambalo uoto wa mimea ya Kaskazini mwa Afrika inakutana na uoto wa mimea ya Kusini mwa Afrika (Miombo).
“Sifa hii inachangia kuwa idadi na aina nyingi ya mimea na wanyama. Hifadhi hii ni kimbilio la wanyama wakati wa kiangazi kwa kuwa eneo ilipo ni kame. Mto Ruaha Mkuu pamoja na mito mingine kama Mwagusi Jongomero na Mzombe huwa ni tegemeo la maji yaletayo maisha katika eneo hili.
Hifadhi hii ilianzishwa mwaka 1964 kwa kupandishwa hadhi eneo la hifadhi ilikuwa pori la akiba la saba ambalo lilanzishwa mwaka 1910. Jina la hifadhi limetokana na neno la Kihehe ‘Luvaha’ ikimaanisha Mto Mkuu ambao ni Rauha. Ruaha iko kwenye eneo la mfumo wa kiikolojia la Ruangwa-Kizigo-Muhesi ambalo lina ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 45,000.
Mwaka 2008 eneo la Usangu liliongezwa kwenye eneo la Hifadhi ya Ruaha na kuifanya kuwa kubwa kuliko hifadhi nyingine Tanzania na Afrika ya Mashariki kwa kuwa na ukubwa wa kilomita za mraba takribani 20,226. Hifadhi hiyo inakadiriwa kuwa na aina za ndege zaidi ya 571 ambao baadhi yao wapo wanaohama kutoka maeneo mengi ya dunia kama Ulaya, Asia, Australia na Madagascar.
Ina ndege wa aina ya pekee ambapo hawapatikani sehemu nyingine duniani kama vile hondohondo. Kuna makundi makubwa ya tembo, nyati, swala, tandala wakubwa na wadogo, korongo na palapala. Pia ni moja ya maeneo machache yaliyobaki duniani ambayo unaweza kuona mbwa mwitu. Wanyama wengine ni simba, duma, chui, twiga, pundamilia, nyani, mbweha masiko, pofu na wengine. Ni hifadhi yenye tembo wengi wanaofikia 20,090.
Ujangili
Dk. Timbuka anaendelea kusema kwamba ujangili kwa sasa umepungua kwa asilimia 60, lakini si kwamba umekwisha.
“Kwa upande wetu sisi Operesheni Tokomeza ilitusadia sana kwa wakati ule, tulikamata silaha nyingi mno milimani,” anasema na kuongeza: “Sasa tumeongeza ufanisi, jangili akikamatwa tunamfuatilia yeye ni mbebaji tu au analipwa kwa ajili ya kushuti tu au ndiyo tajiri, na kama ni mbebaji katumwa na nani na huyo aliyemtuma yuko wapi si kama mwanzo tukimkamta moja kwa moja tunamfungulia mashtaka.”
Ruaha wamedhamiria kupambana na majangili na mwaka jana walianzisha kikosi cha msaada ambacho kina askari 40 wanaopata mafunzo maalum ya kupambana na majangili wakitumia silaha za kisasa zaidi ka SMG na AK 47. Mbali ya kikosi hicho, pia wameanza kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi na kwa kiasi kikubwa wamekuwa na mwitikio mkubwa.
Anasema kwamba lengo la kufanya hivyo ni kutoa wigo wa ushirikiano kwa wananchi katika kupambana na ujangili kwa kuwa wanakijiji wengi wamekuwa wakilipwa ujira kutokana na kubeba pembe za tembo, lakini baada ya kuelimishwa kuhusu ujangili wengi wao sasa wameona faida ya kuwa na wanyama.
Hali ya utalii katika hifadhi
Dk. Timbuka anasema kwamba pamoja na kuwa hifadhi hiyo ni kubwa kuliko zote, bado ni tegemezi wakati wote kutokana na kuwa chini kutalii.
“Kuna mwamko mdogo wa watu katika utalii, lakini tunapambana kuhakikisha kwamba tunajitangaza hadi tufike lengo, miaka miwili iliyopita tulikuwa tunapokea watalii 12,000 lakini baada ya kuongeza bidii sasa tunapokea watalii 25,000 kwa mwaka,” anasema.
Kwa sasa wameweka lengo la kuongeza watalii 50,000 hadi kufikia mwaka 2019 lengo hili litakwenda sanjari na kujenga miundombinu ya barabara, hoteli na kambi kwa ajili ya kufikia watalii. Hata kama wakiongeza idadi ya watalii bado wana vyumba vichache mno ukilinganisha na hifadhi nyingine, wanachofanya ni kutoa elimu kwa wawekezaji wazawa kujenga hoteli katika hifadhi hii.
Hadi sasa wameanza kugawa maeneo tisa kwa ajili ya ujenzi wa hoteli katika hifadhi, lakini ni kampuni tatu tu ndiyo zimeanza kuonesha nia. Ndani ya hifadhi hiyo kwa sasa kuna Hoteli ya River Lodge yenye uwezo kwa kuwa na vitanda 100 hadi sasa.
Mradi wa Spanest
Mratibu wa Mradi wa Kuimarisha Mtandao wa Ulinzi wa Eneo la Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwell Meing’ataki, amesema ni ushirikiano kati ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Shirika la Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNDP).
SPANEST iliundwa ili kulinda mazingira na kusimamia viumbe hai, kwamba mradi huo una lengo la kuongeza ufanisi katika Hifadhi za Taifa na mazingira yanayozunguka, lengo likiwa ni kulinda viumbehai na kutoa mfumo endelevu wa kiikolojia, kijamii na kifedha. Malengo hayo yanakwenda sambamba na kuinua utalii katika eneo la kusini katika Hifadhi za Taifa ya Ruaha. Mradi huo imelenga katika wilaya saba, Greater Ruaha yenye ukubwa wa kilomita 37,000 za mraba na Greater Kitulo-Kipengere (Kilomita 2,150).
Meing’ataki amesema kwamba mradi kwa sasa unatoa mafunzo kwa askari 40 wa Tanapa kwa kuwapa mafunzo ya kisasa ili kukabiliana na majangili wa tembo.
“Tunachokifanya ni kwamba tunawachuja, tulianza kwa kuwachuja askari 100 wakapatikana 40 hawa ndiyo tunawapa mafunzo makali sanjari na mbinu za kisasa za kupambana na ujangili. Tunawapa mafunzo jinsi ya kutumia silaha za kisasa, kutoa huduma ya kwanza iwapo mmoja wao amejeruhiwa na majangili na pia jinsi ya kukamta jangili kwa kutumia teknolojia kisasa ya GPRS.
“Hii ni mpya na tuko katika hatua za mwisho kumpata mzabuni atakayetumia teknolojia hii, tutakachokifanya sasa ni kuwafunga tembo kifaa maalum cha mawasiliano ili kuwafuatilia tembo. Kifaa hiki atafungwa tembo mkubwa anayeongoza kundi, tembo huishi katika familia moja na tembo mkubwa yaani mama ndiyo kiongozi wa kundi, huyu hupewa jukumu la kuongoza familia na kungalia usalama wao kwa kuwa ameishi miaka mingi anajua mazingira.
“Akifungwa kifaa hicho kitakuwa kinatoa mawasiliano, makao makuu ya hifadhi na kama kuna mtu anawafuatilia tembo ataonekana, hivyo askari aliyefunzwa kutumia mtandao huu ataelekezwa ni wapi kuna ujangili na mara moja atawasili katika eneo husika na kupambana nao,” alisema.
Mbali ya mtandao huu pia wanatumia ndege ambayo inafanya doria kila mara, ikiwa na askari, nayo hutoa taarifa ofisini kwa kutumia GPRS.
Anasema; “Tutawafuatilia tembo kila mahali, kifaa hiki kinaweza kutoa taarifa kila baada ya dakika 30 hivyo tutaweza kuwafuatilia tembo hao kila wanapokwenda, tutaanza mradi huu kwa kufunga tembo 30.”
Amesema kutokana na mfumo huo na kwa kuwa askari hao watakuwa wamepewa mafunzo maalum, na iwapo watapewa taarifa ya kila tukio la ujangili linapotokea na watakimbia mara moja na kufanikisha kuzuia uharifu. Mbali ya kutoa mafunzo kwa askari pia wanatoa elimu kwa wanakijiji wanaozunguka maeneo ya hifadhi, jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Hadi sasa tumetoa elimu katika vijiji 44 tunawafundisha watu tabia za wanyama, tunawafundisha wadau mbalimbali kuhusu uhifadhi na pia kuwahamasisha kuwa utalii ni mzuri, sasa wanaelewa kuhusu hilo na limesaidia sana kupunguza ujangili,” amesema.
Amesema mradi huo wa miaka mitano hadi sasa umepunguza ujangili kwa asilimia 56 kwani katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2014 tembo 36 waliuawa ukilinganisha na tembo 82 waliouawa katika kipindi cha miaka 2012/13. Mradi huo umetengeneza barabara zaidi ya kilomita 400 katika hifadhi hiyo, hali inayofanya utalii kuongezeka baada ya kupitika kwa urahisi.
Pia wametengeneza mipaka kilomita 275 na kuweka bikoni 192 Ruaha kilomita 200 na kuweka bikoni 100 na kazi bado inaendelea, Kitulo kilomita 25 na bikoni 78 Mapanga na Kipengere Kilomita 50 bikoni 14.
Michezo
Amesema ili kuboresha mtandao wa hifadhi zilizo kusini mwa Tanzania (SPANEST) kwa kushirikiana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, waliandaa mashindano ya mpira wa miguu yaliyoshirikisha tarafa za Idodi na Pawaga. Mashindano hayo yaliandaliwa kwa mara kwanza kwa lengo la kushirikisha kundi la vijana katika tarafa ambazo zina jumla ya vijiji 21, vyote vikiwa wanachama chini ya Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori Jamii, MBOMIPA (Matumizi Bora ya Maliasili Idodi na Pawaga). Amesema vijiji hivyo 21 vinapakana na Hifadhi ya Taifa Ruaha na shughuli nyingi za jamii huathirika kwa njia moja au nyingine.
Mradi wa SPANEST pamoja na Hifadhi ya Taifa Ruaha zimekuwa zikifanya mikutano mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha uhifadhi kwa wananchi kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na kuonesha sinema za wanyamapori na mabango yenye ujumbe mbalimbali.
“Kutokana na tatizo la ujangili wa pembe za tembo kukithiri miongoni mwa wananchi na kuanzishwa kwa kampeni mbalimbali za kupinga ujangili, wazo la kuunganisha vijana katika vita dhidi ya ujangili bado limeonekana kuwa njia mwafaka ya kuutokomeza, kutokana na ukweli kwamba vijana ndiyo walengwa wakubwa katika kushawishika kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhi na kufanya ujangili.
“Hivyo, vita hii haitaweza kumalizika bila kushirikisha kundi hili kubwa la vijana kupitia njia ya michezo,” anasema.
Amesema lengo la mashindano hayo lilikuwa ni kuunganisha vijana katika vita dhidi ya ujangili wa wanyamapori (tembo), kujenga uelewa juu ya uhifadhi wa wanyamapori miongoni mwa jamii ya vijiji jirani, kujenga mtazamo chanya kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, kuinua vipaji kwa vijana wanaoishi jirani na hifadhi, kutoa burudani kwa jamii inayoishi jirani na hifadhi.
Amesema kuwa katika mashindano hayo, kaulimbiu ilikuwa ‘Pinga Ujangili, Okoa Tembo’ na pia wametoa namba ya simu ya bure ili kufichua ujangili. ‘Piga simu bure 0800751212 fichua majangili‘.
Amesema mashindano hayo yameleta mtazamo chanya juu ya uhifadhi wa wanyamapori, jamii imepata uelewa kuhusu uhifadhi wanyamapori na kusaidia kufichua vitendo vya uhalifu, pia imeibua vipaji vipya na jamii imepata burudani na hamasa ya uhifadhi.
Mshindi wa Kwanza kwa tarafa alizawadiwa Sh 300,000 na kombe, ziara ya kutembelea hifadhi, jezi seti moja, medali ya dhahabu, cheti na mipira miwili. Mshindi wa pili Sh 200,000 mipira miwili, medali ya fedha, cheti, mpira mmoja na mshindi wa tatu Sh 100,000, medali ya shaba, cheti na mfungaji bora Sh 100,000, timu yenye nidhamu Sh 100,000.
Katika mashindano hayo kulikuwa na mabango yenye ujumbe wa mashindano ili kusaidia kufikisha ujumbe kwa watazamaji ili waweze kusoma moja kwa moja. Kila kiwanja kilichoteuliwa kwa ajili ya mashindano kiliwekewa mabango yenye ujumbe na kaulimbiu na kuondolewa kila mchezo unapomalizika.
Wanakijiji wanasemaje kuhusu mradi huo
Mmoja wa vijana katika Kijiji cha Kitisi, Denis Kaguli, amesema kwamba mradi huo umesaidia kutoa elimu kwa vijna, na kwa asilimia 60 umesaidia kuanzisha michezo mbalimbali ikiwamo mchezo wa mpira wa miguu, kwani kila mara baada ya mchezo hutolewa elimu ya kupambana na ujangili.
“Binafsi sikujua umuhimu wa uhifadhi wa maliasili, sasa naelewa kila kitu kuhusu hilo, sina shaka wanyama hasa tembo sasa ni rafiki zangu,” amesema.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kitisi, Zawadi Gembe, amesema mradi huo umerahisisha utendaji wa kazi hasa katika mambo ya uhifadhi, kwani hadi sasa malalamiko ya ujangili yameapungua.