*Wataalamu wasema ni kinyume cha sheria za uwindaji wa kitalii

*Al Amry adaiwa pia kukiuka haki za watoto, kuwapa silaha hatari

*Kesi ya rushwa aliyobambikiwa mwandishi yapigwa tarehe

ARUSHA

Na Mwandishi Wetu

Wakati kesi iliyofunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha dhidi ya mwandishi wa JAMHURI mkoani humo, Hyasinti Hillary, ikipigwa kalenda, uchunguzi umebaini kuwapo kwa matumizi mabaya ya silaha za uwindaji wanyamapori katika mapori mbalimbali ya Kanda ya Kaskazini.

Matumizi hayo yanayokinzana na sheria za uwindaji wanyamapori nchini yanadaiwa kufanywa na mfanyabiashara wa jijini Arusha, Saleh Al Amry, kwa miaka kadhaa.

Chanzo kimoja cha habari kimesema bunduki yenye kiwambo cha kuzuia sauti imekuwa ikitumiwa na Al Amry mwenyewe pamoja na wateja wake kutoka Saud Arabia.

“Hii bunduki tumekuwa tukiambiwa kuwa huwa anaificha chini ya kiti cha gari lake. Maofisa wa kupambana na ujangili wamekuwa wakiamini kuwapo kwa matumizi batili ya silaha kwenye mapori ya uwindaji katika mikoa ya Manyara na Arusha,” anasema mtoa taarifa huyo ambaye ni mmoja wa maofisa wa kikosi cha kupambana na ujangili na kuongeza:

“Nilishituka sana nilipoona gazetini kwenu picha ya bunduki yenye ‘silencer’ (kiwambo cha kuzuia sauti) ikichezewa na watoto wa Al Amry.”

Picha hiyo ambayo imechapishwa tena katika toleo hili, ilichapwa kwa mara ya kwanza Desemba 28, 2021 na kuzua maswali mengi kutoka kwa wadau wa uwindaji na utalii nchini.

Ingawa hakusema mara moja iwapo kikosi cha kupambana na ujangili kitaifuata silaha hiyo kwa Al Amry, ofisa huyo wa taasisi nyeti nchini anasema: “Hii haitaruhusiwa kuendelea tena kutumika kwenye misitu yetu.”

Tayari picha za ujangili zinazomwonyesha Al Amry na washirika wake wakiwa wameua hovyo wanyama ndani ya Pori Tengefu la Simanjiro zimekwisha kuwasilishwa Makao Makuu ya Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA) kwa ajili ya hatua zaidi.

Kifungu cha 65(1) cha Sheria Namba 5 ya Uhifadhi Wanyamapori ya mwaka 2009 kinasomeka: 

“Any person shall not, except by and in accordance with the written authority of the Director previously sought and obtained or in accordance with regulations made under this Act- (a) use by purpose of hunting any animal – (iv) any device capable of reducing or designed to reduce the sound made by the discharge of any firearm.”

Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi, mtu yeyote haruhusiwi kuwinda mnyama kwa kutumia silaha yenye kiwambo cha kupunguza au kuzuia sauti ya risasi.

Akifafanua kuhusu sheria hiyo, Ofisa Maliasili Mkoa wa Katavi, Josephine Rupia, anasema sheria hiyo imewekwa ili kumpa mnyama nafasi ya kujitetea iwapo risasi itamkosa.

“Ndiyo maana tunasema ni game (mchezo). Kila upande unapaswa kushiriki. Mlio wa bunduki unampa mnyama nafasi ya kujitetea kwa kukimbia au kufahamu kwamba; ‘ohoo, kuna kitu kinaendelea hapa’.

“Sasa kama utaweka kiwambo cha kuzuia sauti ni kwamba utakuwa unaua wanyama bila kuwapa nafasi ya kujitetea au kufahamu kuwapo kwa ‘mchezo’. Inakosa maana,” anasema.

Anasema sheria hiyo ya wanyamapori pia inazuia kuwinda kwa kutumia silaha ya ‘automatic’ (inayotoa risasi mfululizo) na kwamba matumizi ya silaha za aina hiyo ni haramu.

Watoto na silaha ya moto

Mbali na kiwambo cha kuzuia sauti kinachoonekana kwenye silaha inayoaminiwa kuwa ni mali ya Al Amry, haki za binadamu pia zinazuia watoto kupewa au kuchezea silaha.

JAMHURI limezungumza na wataalamu mbalimbali wa saikolojia na malezi ya watoto waliolaani kitendo cha Al Amry kuwapiga picha watoto wake wakichezea silaha.

Hata hivyo, watu karibu wote hawakutaka kutajwa majina yao gazetini wakihofia usalama wao.

“Hawa majangili ni watu hatari sana. Si salama hata kidogo kuwazungumzia, kwa kuwa wakikufahamu wanaweza kukupoteza.

“Wana fedha nyingi na sisi watu wa Arusha tunalifahamu hilo. Lakini ukweli unabaki kuwa watoto hawapaswi kupewa au hata kuona namna silaha hatari kama bunduki inavyotumika,” anasema mtaalamu wa malezi na saikolojia mkazi wa Arusha aliyezungumza na mwandishi wa habari hii wiki iliyopita.

Akizungumzia ushiriki wa watoto katika uwindaji na masuala ya silaha, mwindaji mahari (professional hunter – PH) anayemfahamu vema Al Amry, amesema sheria inakataza wazi.

“Katika uwindaji haturuhusiwi kusindikizwa au kuandamana na watoto wenye umri chini ya miaka 18. Sheria hairuhusu, sasa kama kuandamana nao hairuhusiwi, itakuwaje kuwaacha wachezee silaha?” anahoji PH huyo.

Tangu JAMHURI lilipoanza kuandika taarifa za ujangili unaodaiwa kufanywa na Al Amry, yeye amegoma kutoa ushikikiano kwa kutopokea simu wala kujibu ujumbe wa maandishi anaotumiwa mara kwa mara.

Kesi ya rushwa ya mwandishi

Kwa upande mwingine, kesi namba 136/2021 iliyofunguliwa mwishoni mwa mwaka jana kwenye Mahakama ya Wilaya ya Arusha dhidi ya Mchau, imeahirishwa hadi Februari 8, 2022.

Kesi hiyo imefunguliwa katika mazingira ya kutatanisha baada ya Mchau, mwandishi wa JAMHURI, kufika ofisini kwa Al Amry Jumapili ya Desemba 26, mwaka jana kupata ufafanuzi wa maswali kadhaa kuhusu tuhuma za ujangili.

Kabla ya mkutano huo, JAMHURI lilimtaarifu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, James Ruge, kuwapo kwa uwezekano wa mwandishi kubambikiwa kesi ya rushwa.

Tahadhari hiyo iliyopokewa na kujibiwa na Ruge inatokana na taarifa zisizokuwa na shaka kwamba Al Amry huwatumia maofisa wa TAKUKURU kuficha maovu yake.

Hata hivyo, Ruge alizitumia taarifa alizopewa na kushirikiana na Al Amry kumkamatisha kwa rushwa mwandishi na kisha kumfungulia kesi mahakamani.

“Nilipofika ofisi za TAKUKURU nilikutana na Ruge. Akaniuliza jina la mhariri aliyenituma, nikamtajia naye akaliandika; kisha akaniuliza wamiliki wa Kampuni ya JAMHURI, nikawataja naye akaandika majina yao,” anasema Mchau.

Wakati Ruge akiongoza mahojiano hayo ndani ya ofisi za TAKUKURU Arusha, alimwambia Mhariri wa JAMHURI aliyekuwa akizungumza naye kwa njia ya simu mara kwa mara kuwa hakuwapo jijini Arusha.