Awali ya yote, mimi na wewe msomaji wa makala hii tumshukuru Mwenyeezi Mungu kwa neema zisizo na idadi alizotutupa na anazoendelea kutupa kwa hisani yake na ambazo tukijaribu kuzihesabu hatuwezi kamwe kudhibiti idadi yake. Neema za Mola wetu Mlezi kwetu ni nyingi sana na hazina idadi, Alhamdu Lillaah!
Nichukue fursa hii adhimu kukukaribisheni katika ‘Uga wa Dini ya Kiislamu’; safu ambayo itatuunganisha kila siku ya Jumanne kuzungumzia mambo mbalimbali yanayohusu Uislamu, kupitia Gazeti la JAMHURI ambalo limeisadifu asili ya neno katika lugha ya Kiarabu ambapo moja ya maana zake ni ‘watu’; hivyo Gazeti la JAMHURI ni chombo cha watu kwa ajili ya watu na ni sauti ya watu.
Maudhui ya makala hii kama yalivyoainishwa na anuani iliyotangulia ni ‘Uislamu ni Dini ya Kijamii’.
Uislamu ni dini inayojengwa kwa nguzo tano ambazo ni:
(1) Kutamka kwa ulimi na kuamini kwa moyo kwamba Hapana Mola Apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mungu mmoja na kwamba Muhammad ni Mtume wake.
Nguzo hii hii ya kauli hujulikana kwa jina la Shahada Mbili, mosi ni kule kushuhudia kuwa Mwenyeezi Mungu ni Mmoja aso mshirika; na pili ni kushuhudia Utume wa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani). Shahada Mbili ndio tiketi ya kuingia katika Uislamu na kwa yeyote anayetamka Shahada Mbili hizi na akazikariri huhesabiwa ni Muislamu.
(2) Kusimamisha Swala tano. Swala ni uti wa mgongo wa Dini ya Uislamu na ni Faradhi Muhimu sana katika Uislamu.
(3) Kutoa Zaka. Zaka ni fungu maalumu lililokadiriwa katika Sheria ya Uislamu kutolewa kutokana na mali za wenye-nacho na kugawiwa wanaostahili wakiwemo mafukara na masikini.
(4) Kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wenye fadhila kubwa na malipo makubwa.
(5) Kuhijji Makkah kwa mwenye uwezo.
Pamoja na Nguzo Tano za Uislamu kuna Nguzo Sita za IMAAN na Nguzo Moja ya IHSAAN.
Nguzo Sita za Imaan (kukubali kwa dhati ya moyo bila chembe ya shaka uwepo wa Mwenyeezi Mungu) ni:
(1) Kumuamini Mwenyeezi Mungu kwamba Ndiye Pekee Anayestahiki kuabudiwa kwa Imani ya dhati isiyoingiwa na chembe ya shaka.
(2) Kuamini Malaika wake, kwamba ni viumbe wa Mwenyeezi Mungu Aliyewaumba ili wamuabudu, wamtukuze na wamtakase.
(3) Kuamini Vitabu vyake Alivyoviteremsha kwa Mitume; Taurati, Injili, Qur’aan, Zaburi na Sahifa za Nabii Ibrahim (Allaah Ampe Amani).
(4) Kuamini Mitume wake ambao Amewatuma kuanzia kwa Mtume Adam (Allaah Ampe Amani) hadi Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ili kuwaongoa watu kutoka kwenye giza la upotovu na kwenda kwenye nuru ya uongofu.
(5) Kuamini Siku ya Mwisho na yanayofungamana na siku hiyo ikiwemo kufanyiwa hesabu ya matendo yako, kuonesha hesabu yako, Mizani ya Haki, Malipo Stahiki na Pepo na Moto.
(6) Kuamini Qadar (mpango wa Mwenyeezi Mungu); yale Aliyoyapanga Mwenyeezi Mungu na Akayaandika miongoni mwa mambo ya viumbe hadi Siku ya Kiyama, yaani, kheri zake na shari zake.
Amma IHSAANI nguzo yake ni moja tu ambayo ni kumuabudu Mwenyeezi Mungu kama vile unamuona na kama humuoni yeye anakuona. Nguzo hii ina maana ya kumzingatia Mwenyeezi Mungu kuwa anayaona na kuyadhibiti matendo na kauli za viumbe vya Siri na Dhahiri. Mwenyeezi Mungu Anayajua yaliyofichikana katika dhamira za viumbe kama ambavyo anamuona na kujua harakati za sisimizi katika usiku wa giza nene.
Kwa muktadha huo, nguzo za Uislamu Imani na Ihsaani zinatosha katika mtazamo wa awali juu ya kumfahamu Muislamu.
Kwa kuwa Uislamu ni dini na yule anayeutekeleza ndiye Muislamu, yaani Muislamu hapaswi kutambuliwa kwa jina kwani hakuna majina ya Kiislamu, bali majina yatokanayo na lugha za watu kama vile majina ya Kibantu, majina ya Kiarabu, majina ya Kizungu na kadhalika. Muislamu hapaswi kutambuliwa kwa mavazi kwa kuwa hakuna mavazi ya Kiislamu, bali mavazi anuia ya jamii mbalimbali. Muislamu anapaswa atambuliwe kwa kufuata kwake misingi ya Uislamu na utekelezaji wake.
Ifahamike basi kwamba Muislamu kwa upande wa pili ni mwanaadamu anayehitaji kula, kunywa, kuvaa, kusafiri, kulala, kupumzika, kuoa au kuolewa, kuzaa na kadhalika. Hivyo basi, Muislamu atawajibika na kuwajibikiwa kuamaliana na jamii yake kwa kufanya kazi, biashara, kilimo, kusafiri na kadhalika.
Tukiyatazama hayo namna Uislamu unavyojali na kuyawekea muongozo katika maisha ya mwanaadamu, inatudhihirikia kwamba Uislamu ni Dini ya Kijamii.
Dhana zilizoko mitaani zinauona Uislamu kama dini ya kiroho tu na mambo yote ya kijamii katika jamii zetu kama vile kuuziana, kukodishana, kuazimana, kuwekeana rehani, kukopeshana, kuwekeana mikataba ya ushirika katika kazi au huduma; hayo hayana majibu katika Uislamu.
Ukweli ni kwamba Uislamu unatambua ibada na pia unatambua miamala na umebainisha usahihi wa kila kimoja ili jamii iweze kuishi salama kwa upendo.
Na namna Uislamu ulivyofafanua na kuweka sawa miamala, lau kama jamii ingeamua kufuata miamala kama ilivyoelekezwa na Uislamu, basi jamii ingepunguza mifarakano inayochangiwa na matatizo ya miamala kwa kiwango kikubwa sana.
Lakini hata katika ibada za kawaida kama vile Swala, Swaumu, Hijja na Zaka, Uislamu umeweka usahihi wa ibada hizo katika kukubaliwa kwake uzingatie kwanza maisha ya Muislamu katika jamii yake na hata utekelezwaji wenyewe pia uiangalie jamii. Na hapo ndipo hubainika wazi kwamba Uislamu ni dini ya kijamii.
Ibada yoyote ndani ya Uislamu ambayo Muislamu ameitekeleza itakiwavyo na akaandikiwa ‘ujira’ wake, basi ieleweke wazi kwamba anaweza kunyang’anywa ujira huo kama ameishi ‘vibaya’ na jamii yake.
Bwana Mtume Muhammad (Allah Amrehemu na Ampe Amani) amesema (namnukuu): “Je, mnamjua mtu aliyefilisika? Maswahaba wakajibu Aliyefilisika ni yule asiye na fedha wala bidhaa. Bwana Mtume akasahihisha kwa kusema: Aliyefilisika katika umma wangu ni yule atakayekuja siku ya Qiyama (Siku ya Hukmu) na ujira wa Swala, Zaka, Swaumu na Hijja lakini (kule duniani hakuishi vyema na jamii) alimtukana huyu, alimdhulumu huyu, alimwaga damu ya huyu, atanyang’anywa malipo ya ibada zake ili wapewe wale ambao aliwadhulumu au aliwatukana”(mwisho wa kunukuu).
Hapo tunajifunza kwamba pamoja na ibada anazozifanya Muislamu, kama ataishi vibaya na jamii yake, basi ibada zake hazitomfikisha katika malengo ambayo ni kupata radhi za Mola wetu Muumba.
Jamii imepewa kipaumbele na Uislamu kwa kiasi kikubwa sana.
Tukiiangalia ibada ya Swala, tunaona namna inavyojenga mazingira ya wanajamii kukutana kwa lazima mara tano kwa siku kwa wale wanaoishi jirani na mara moja kwa wiki Swala inalileta pamoja kundi kubwa la wanajamii wanaoishi katika mji mmoja.
Ibada ya Zaka, kwa upande wake, ni ibada ya kijamii zaidi yenye jukumu la kuona wale wasio nacho wanafaidika japo kwa uchache kutoka kwa walio nacho ili kupunguza chuki kati ya walio nacho na wasio nacho.
Ibada ya Swaumu pamoja na kwamba ni ya kiroho, lakini kwa jicho la pili ni ibada ya kijamii kwani aliyefunga atapata uhalisia wa ukali wa njaa na kiu. Hivyo anapokisikia kilio cha mwenye njaa na kiu atakielewa vyema na kupata huruma ya kusaidia.
Vilevile ibada ya Hijja ni ibada ya kijamii kwani anayehijji ni lazima ajichunge sana kuwakera Mahujjaji wenzake kwa namna yoyote ile mbali ya kuwa ni uwanja wa kuwakutanisha watu wa jamii mbalimbali toka pembe zote za dunia mwaka mara moja.
Kwa muktadha huo, jamii imepewa nafasi kubwa na Uislamu hivyo Muislamu wa kweli kipimo cha Uislamu wake kitazamwe ni namna gani anaishi na jamii yake.
Muislamu anapofanya matendo mabaya kama vile ufisadi, rushwa, wizi, kusema uongo, kudhulumu, kuudhi kwa namna yoyote ile na kadhalika, huyo hauwakilishi Uislamu. Muislamu wa kweli ni lazima jamii ifaidike kwake na isipate madhara yoyote kupitia yeye na ninaposema jamii namaanisha Waislamu, wasiokuwa Waislamu na hata wanyama.
Uislamu ni dini ya kijamii.
Tukutane Jumanne ijayo Inshaallaah.
Mwandishi wa makala hii, Sheikh Khamis Mataka, ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Baraza Kuula Waislamu Tanzania (BAKWATA). Anapatikana kwa namba: 0713 603050, na 0784 603050.