Utunzaji wa mazingira ni kadhia inayozungumzwa sana ulimwenguni katika ngazi zote kutokana na umuhimu wake na maisha ya mwanadamu. Je, umepata kujiuliza mazingira ni nini?
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira nchini Tanzania ya mwaka 2004, mazingira yanahusisha maumbile halisi yawazungukao binadamu, ikiwa ni pamoja na hewa, ardhi, maji, tabianchi, sauti, mwanga, harufu, ladha, vijiumbe, hali za kibaiolojia za wanyama na mimea, rasilimali za kitamaduni na masuala ya uchumi jamii na inahusisha mazingira asilia na yaliyoundwa na binadamu na jinsi yanavyoingiliana.
Katika Uislamu, mazingira ni vyote vinavyomzunguka mwanadamu miongoni mwa vilivyopo, ikiwemo hewa, maji, viumbe vyote hai, maliasili na kwa ujumla, mfumo mzima wa alivyoviumba Allaah kwa nidhamu ya hali ya juu na ulinganifu wa mizania katika huu ulimwengu na mwanadamu akapewa jukumu la usimamizi.
Unapoisoma Quran Tukufu utaona msisitizo wa Uislamu juu ya mazingira na namna ilivyokusanya vipengele vingi juu ya uhusiano wa mtu na mazingira.
Msisitizo huu hauishii tu kwa mtu, familia na mazingira yanayoizunguka, bali unahusu ulimwengu mzima unaojumuisha mbingu na ardhi na viumbe vyote vya Mwenyezi Mungu vilivyomo ndani yake.
Quran Tukufu inazungumzia mambo yote ambayo huitwa maumbile (nature); inazungumzia misingi ya kijiolojia ya maumbile hayo, maji yake, safari tulivu na korofi za hapa na pale za maumbile na nyendo pamoja na aina nyingi na mbalimbali za maisha na uhai, na jinsi uhai unavyoyaendesha na kuyadumisha.
Kwa ujumla, Quran Tukufu imezungumzia kwa namna ya kipekee uhai, asili ya maumbile na ulimwengu. Kuna aya nyingi za Quran Tukufu zinazozungumzia masuala ya mazingira na kutoa mwongozo wa yale ambayo hata wana-mazingira na wataalamu wa mazingira hawajafikia kuyajadili, ikiwemo Mwenyezi Mungu alivyobainisha kwa usahihi kabisa jinsi gani mwanadamu asiye na mwongozo angekuwa mharibifu (fisadi) katika makazi yake ndani ya sayari hii.
Ndani ya Quran Tukufu utakumbana na aya zinazojenga kiroho na kiakili kama vile tunavyosoma katika Quraan Tukufu Sura ya 40 (Surat Ghaafir) Aya ya 57 kuwa: “Bila ya shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu. Lakini watu wengi hawajui.”
Na tunasoma pia katika Quran Tukufu Sura ya 6 (Surat Al-An-aam) Aya ya 38 kuwa: “Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake mbili, ila ni umma kama nyinyi (tunadhibiti kila wafanyalo). Hatukupuuza Kitabuni (mwetu) kitu chochote. Kisha watakusanywa kwa Mola wao Mlezi.”
Mtazamo wa Uislamu juu ya utunzaji wa mazingira umejengwa katika kuamini, bila ya chembe ya shaka, kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwanzishi na muumbaji wa viumbe wote, na yote na vyote vinavyokusanywa na neno mazingira na kwamba vyote vimeumbwa kwa mpango wa kimungu unaozingatia idadi, ubora na uhalisia na kwamba kila kilichoumbwa kimeumbwa kwa kazi na kusudio maalumu na kwamba binadamu ni kiumbe wa kimazingira anayepaswa kuishi kwa utangamano na mazingira.
Kwa pamoja, binadamu na mazingira yake ni viumbe vya Mwenyezi Mungu na vyote vimeumbwa kumwabudu yeye ukiacha tofauti moja moja ya kiufundi aliyonayo binadamu ambapo yeye ana hiari ya kukataa kumuabudu na kumtii Mwenyezi Mungu, ingawaje katika mambo mengine ya kimaumbile, humtii bila hiari. Kila kilichoumbwa na Mwenyezi Mungu kuna kusudi la kuumbwa kwake ambalo halina budi kutimizwa. Quraan Tukufu inatuwekea wazi hili tunaposoma Sura ya 46 (Surat Al-Ahqaaf)  Aya ya 3 kuwa: “Hatukuziumba Mbingu na Ardhi wala yaliyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda maalumu. Na waliokufuru wanayapuuza yale wanayoonywa.”
Kwa utunzaji wa uumbaji wake, Mwenyezi Mungu ameweka idadi kubwa ya rasilimali za mazingira zinazolingana na mahitaji ya jumla ya rasilimali katika ulimwengu. Hii inamaanisha uwepo wa urari wa mazingira katika mazingira ya asili. Kwa hivyo, Uislamu unaangalia mazingira kwa jicho la usawa na urari. Quran Tukufu inaelezea wazo la urari wa mazingira kwa maneno anuwai kama ‘adl’, ‘qadar’ na ‘mauzoon’. ‘Adl’ inamaanisha kutenda haki, sawa, au kwa usawa. ‘Qadar’ ni kipimo au kiwango fulani cha idadi au sifa. Neno hili linasisitiza wazo la urari katika aya zifuatazo:
Tunasoma katika Quran Tukufu Sura ya 54 (Surat Al-Qamar) Aya ya 49 kuwa: “Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.”
Aya hizi hapo juu zinatoa taarifa ya jumla juu ya uwepo wa urari katika kila kitu. Mchakato wa uumbaji na ukuaji wa vitu vyote hufuata kanuni ya usawa.
Tunasoma pia katika Quran Tukufu Sura ya 15 (Surat Al-Hijri ) Aya ya 19 na 20 kuwa: “Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi (kipimo) chake. Na tumekujalieni humo vitu vya maisha yenu, na hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku”.
Tunachojifunza kutokana na aya iliyotangulia ni kuwa vitu vya kila aina vimetengenezwa kwa ajili ya ustawi wa wanadamu na wasio wanadamu miongoni mwa viumbe wa Mwenyezi Mungu, kwa njia ambayo idadi ya mahitaji haya yanalingana na ugavi aliouweka Mwenyezi Mungu. Hakuna swali juu ya uhaba wala ziada katika mpango wa kimungu na usimamizi wake wa mazingira.

Tatizo la mazingira liko wapi?

Kwa kuyatazama matatizo ya kimazingira tunayokabiliana nayo hivi leo, ambayo hapo kabla hayakupata kutokea, tunaona kuwa kinachoitwa uharibifu wa mazingira si chochote ila ni tatizo la mwanadamu mwenyewe. Tulipotokea takriban mamia kwa maelfu ya miaka, tamaduni za wanadamu zilijenga udadisi wa kimaumbile wa watoto kuhusu maumbile hadi katika umri wa utu uzima wa kujenga maarifa. Katika mzizi wake, tamaduni hizo zikafundisha watu kuyatazama mazingira kama pambo lililoletwa katika maisha haya na Muumba wetu na ziliheshimu ule uhusiano miongoni mwa viumbe duniani.
Zaidi ya hapo, tamaduni hizo ziliifungamanisha elimu hii na mwongozo wa maisha uliotoka kwenye chanzo hai kilicho nje ya ulimwengu unaoonekana, na kilicho ndani ya ulimwengu usioonekana. Kamwe tamaduni hizo hazikulitenganisha umbile la dunia na chimbuko lake.
Kwa sababu ya ule ufahamu wao halisi juu ya ulimwengu, wao wenyewe wakiwa ndani ya ulimwengu huo na ulimwengu ukiwa ndani yao, kwa namna tofauti, wao na ulimwengu huo wakitoka katika chimbuko moja la maisha, wakafahamu kuwa walitakiwa kuishi katika ulimwengu huo, kufanya kazi kutokana na ulimwengu huo, kutumikiana na ulimwengu huo, na kuhangaikia sehemu yao ya ulimwengu huo kwa kadiri ya uwezo wao, na kuutunza kwa uangalifu ulimwengu huo ili udumu kwa ajili yao, watoto wao, wajukuu wao na vizazi vyao.
Aidha, walifahamu kuwa dhambi zao dhidi ya viumbe zilikuwa ni dhambi dhidi ya Muumba, na kwa matokeo yake wangekumbwa na janga la kimaumbile likiangamiza moja kwa moja makazi yao, wasipojirekebisha.
Nimalizie makala hii kwa kuyanukuu yaliyopata kuandikwa kama maazimio matano ya Uislamu juu ya utunzaji wa mazingira ili sisi tukiwa ndio waharibifu wa mazingira yetu tunaojisababishia majanga ya kimazingira kwa kazi ya mikono yetu tujikumbushe kuwa:
Moja, binadamu ni kiumbe wa kimazingira. Hivyo, lazima aishi kwa utangamano na mazingira. Na ingawaje dunia na mazingira yaliumbwa kitambo kabla ya binadamu, lengo la vyote viwili ni lilelile la kufanya kazi pamoja-hadi mwisho-ndiyo kusema basi, lengo halisi ni kumnufaisha binadamu, hivyo aendeshe maisha yake kwa mtindo wa urafiki na mazingira yake na kwamba tatizo la mazingira ni jambo la kibinadamu ambapo ushirikiano wa kuzikabili changamoto zake usikwazwe na tofauti za kidini, kisiasa au nyingine zozote zile.
Pili, binadamu ndiye aliyepokea dhamana ya Ukhalifa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo inampa jukumu la kuyatumia mazingira kufikia lengo hili la maisha alilowekewa na Mwenyezi Mungu kwa sharti kwamba ayadumishe mazingira hayo kwa ajili ya vizazi vijavyo ambavyo vina haki nayo kama wenzao waliotangulia.
Tatu, binadamu hawezi na hataweza na wala hatakuwa mkweli katika utunzaji wake wa dunia bila kuwa na insafu kwa maumbile yote. Binadamu atakuwa mwadilifu katika kuendesha maisha yake katika ulimwengu huu kwa sababu Mwenyezi Mungu kauumba kwa kipimo cha mizani.
Binadamu akishindwa jambo hilo, basi dhuluma itasababisha vurugu ya ulimwengu, nao ulimwengu utashindwa kuendelea kutimiza mahitaji ya kumkirimu binadamu.
Nne, Binadamu atambue kuwa Mwenyezi Mungu kakataza kudhuru nafsi yake mwenyewe au nafsi za wengine, si dhara kubwa wala dogo. Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Hakuna sababu ya kudhuru wala kulipiza dhara.” (Ibn Majah). Na Mwenyezi Mungu anatuambia katika Quran Tukufu Sura ya 7 (Surat Al-Araaf) Aya ya 56 kuwa: “Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwishakutengenezwa.”
Tano, mwanadamu afuate njia ya kati na kati na matunzo, kwani kiasi kikubwa cha uchafuzi wa mazingira kinatokana na tamaa ya mali na ufujaji.
Tutambue kuwa jitihada za kurejesha urari bora wa mazingira hazitafanikiwa kwa kiwango chochote cha maana bila kupambana na uharibifu usioonekana wa vita ya matamanio yetu.
Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.
 
Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Simu: 0713603050/0754603050