Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali ya Uingereza imesema imefurahishwa na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa huduma katika bandari ya Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Bandari ya Dar es Salam jana, Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Bw Lord Collins amesema kuwa wakiwa kama sehemu ya wadau wa bandari ya Dar es salaam wanajivunia kuona miundombinu ya bandari imeboreshwa na kwa kiasi kikubwa imeongeza ufanisi mkubwa kiutendaji na pia imeendelea kupiga hatua katika Nyanja ya utoaji huduma bandarini hapo.

“Napenda kuchukau nafasi hii kuipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandaari Tanzania(TPA) pamoja na viongozi wote kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika hapa bandarini,” alisema Bw Collins ambaye aliambatana na Balozi wa Uingereza hapa Tanzania, Bi Marianne Young.
Waziri Collins alisema bandari ya Dar es Salaam ni mfano wa bandari ya kuigwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kwa sababu inaunganisha Tanzania na nchi zote ambazo zinaizunguka Tanzania, hivyo maboresho yake yataongeza tija zaidi.
“Najua maboresho haya yanaongeza tija na ajira hasa kwa Watanzania ambao ndiyo wanufaika wa kwanza wa uwekezaji huu, hivyo tunafurahi kuona neema zaidi kwa wananchi wa Tanzania” aliongeza Bw Collins.
Serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la misaada la (UK Aid) ni miongoni mwa Wadau wa Maendeleo walifanikisha kuchangia maboresho ya miundombinu mbalimbali katika bandari ya Dar es Salaam kama vile ujenzi wa barabara za ndani, uboreshwaji wa eneo la maegesho pamoja na teknolojia ya mtandao unaosaidia kazi mbalimbali bandarini hapo.

Kwaupande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Bandari Dkt Baraka Mdima amesema kuwa ugeni wa viongozi kutoka serikali ya Uingereza ni fursa kubwa kwa Tanzania katika nyanja ya uhusiano wa kiuchumi kupitia usafirishaji wa mizigo katika bandari ya Dar es salaam
Naye Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Dkt Baraka Mdima alisema ugeni huo ni chachu kubwa kwa maendeleo yanayoonekana kwenye bandari hiyo.
“Mchango wa Serikali ya Uingereza ni mkubwa sana na hatuna budi kuwashukuru kwani hivi sasa sasa tunapata meli nyingi ambazo hapo awali zilikuwa hazifiki na sambamba na hilo hata idadi ya shehena pia imeongezeka na kuchangia ongezeko la pato la la taifa” alisema Dkt Mdima.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Bw Mbelwa Kairuki ubalozi unafanya uhamasishaji mkubwa mkubwa kwa wafanyabishara nchini Uingereza kuja kufanya bishara hapa Tanzania.
Aliiomba Uingereza kufungua zaidi milango kwa watazania wanaopenda Kwenda kuwekeza zaidi nchini uingereza.
