Siku chache zilizopita Waingereza wamepiga kura kujitoa katika Muungano wa Nchi za Ulaya (EU), na haikuchukua muda, thamani ya pauni ya Uingereza ikaporomoka na kufikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu mwaka 1985. Zaidi ya asilimia 52 ya waliopiga kura walipiga kura ya kujitoa.
Kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya Uingereza ni kielelezo cha muda mfupi cha imani ndogo ya wadau wa sekta ya biashara juu ya ustawi wa uchumi wa Uingereza.
Kwa sababu kura ilihusisha pande mbili zilizokinzana. Kipindi cha kampeni cha miezi miwili kimehusisha tafiti mbalimbali zilizokusudia kutabiri nini yatakuwa matokeo ya muda mrefu ya kujitoa, au kubaki kwa Uingereza ndani ya muungano wa nchi 28 za Ulaya.
Na kama ilivyo tafiti nyingi za aina hii, hakuna makubaliano kuhusu athari au faida za kujitoa. Wapo wanaosema kuwa hasara za kujitoa zitakuwa kubwa kuliko faida zake, na wapo wanaodai kuwapo kwa faida za kujitoa.
Jambo ambalo halina ubishi ni kuwa uamuzi wa kujitoa umeibua nyufa ndani ya nchi ambayo tunaiita Uingereza, au United Kingdom kwa lugha ya Kiingereza, ule muungano wa nchi unaojumuisha England, Wales, Scotland, na Ireland ya Kaskazini.
Tunakumbushwa maneno ya Mwalimu Nyerere aliyotoa kwenye hotuba yake ya mwaka 1995 kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, Dar es Salaam akitahadharisha dhidi ya mawazo ya kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Walioshinda kura ya kuiondoa Uingereza Ulaya walitumia hoja kadhaa, ikiwa ni pamoja na kurejesha uhuru wao wa kudhibiti uchumi wa Uingereza ulioonekana unaongozwa na Jumuiya ya Ulaya.
Hali kadhalika, Tanzania ilikuwa ina Wazanzibari na Watanganyika walioamini wananyimwa uhuru wa kutetea maslahi yao, wakiamini uhuru huu utashamiri tu ndani ya nchi mbili huru – Tanganyika na Zanzibar, na bado wapo.
Mwaka 2014 wananchi wa Scotland walipiga kura ya maoni kuamua iwapo nchi yao iendelee au ijiondoe katika muungano wao. Waliotaka kujitenga walishindwa katika kura hiyo kwa kupata asilimia 48 pekee. Sasa wale walioshindwa mwaka 2014 wameibua tena madai ya uhuru wa Scotland baada ya wenzao kupiga kura ya kujiondoa kwenye Jumuiya ya Ulaya.
Wanasaikolojia wanasema kuwa makundi hubadilisha mawazo kwa kuangalia mafanikio yaliyofikiwa na makundi yanayowazunguka. Kama wenzetu wamefanikiwa kujiondoa kwenye muungano wa wengi, basi wazo lile lile, hata kama halina manufaa dhahiri, linaanza kufukuta miongoni mwetu na hatimaye na sisi tunaanza mikakati ile ile ambayo wenzetu wameikamilisha.
Waskochi waliopiga kura kujitenga mwaka 2014 waliambiwa kuwa ingekuwa vigumu kwa nchi huru ya Scotland kujiondoa United Kingdom na kukubaliwa kujiunga na Jumuiya ya Ulaya. Waliambiwa hivi Waingereza wenzao, lakini waliambiwa hivi na baadhi ya nchi wanachama za Jumuiya ya Ulaya ambazo zinakabiliwa na maeneo yanayotaka kujitenga.
Sababu ya msingi ya wapiga kura wa Scotland kuibua tena hoja ya kujitenga baada ya matokeo ya kura hii ya juzi, ni ukweli kuwa kwenye kura hii ya sasa, asilimia 62 ya wapiga kura wa Scotland walipiga kura ya kubaki ndani ya Muungano wa Ulaya.
Hakuna uhakika kwamba kura ya pili ya maoni inaweza kufanikisha kujitenga kwa Scotland, lakini ilichofanikiwa kufanya kura hii ya juzi na kuibua tena hisia za utengano miongoni mwa raia wa United Kingdom.
Siyo Scotland tu, lakini hata Ireland ya Kaskazini nako kumeibuka hoja za kuwapo kwa kura ya maoni ya kuiondoa sehemu hiyo ya Uingereza na kuiunganisha na Jamhuri ya Ireland, ingawa uwezekano wa kufanikisha azma hii ni mdogo kwa sababu wanaoiunga mkono ni wachache.
Kwa wanaounga mkono jitihada za kujenga umoja, uamuzi wa Uingereza kujitoa kwenye Muungano wa Ulaya ni pigo kubwa sana. Na si ajabu wapo wanaoomba kuwa Uingereza, kwa kujitoa, itajikuta katika miaka ijayo kwenye hali mbaya zaidi ya kisiasa na kiuchumi, na katika mahusiano yake na Umoja wa Ulaya.
Kama Uingereza itastawi na kushamiri, basi kazi ya kuhubiri umoja itakuwa ngumu zaidi. Na huu ukweli upo kwa Umoja wa Ulaya, na vilevile kwa jitihada zetu za kujenga umoja wa kikanda miongoni mwa nchi za Kiafrika na ndani ya bara la Afrika.
Hatuwezi kuilinganisha Uingereza na nchi zetu zinazoendelea. Uingereza ilikuwa inachukua nafasi ya pili baada ya Ujerumani kwa kuwa na uchumi mkubwa kuliko yote kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya. Wao kuamua kujitenga ni rahisi kuliko ambavyo itakuwa kwa nchi yenye uchumi tegemezi kwenye bara la Afrika.
Ni nadra kusikia mtu mwenye shida kukataa ushirikiano na wenzake. Jeuri ya kujitenga inaambatana na uwezo wa kuukataa umoja. Hapa ndiyo iko salama yetu sisi tunaojaribu kujenga umoja katika mazingira ya mataifa yanayoendelea. Kwetu sisi bado tunaweza kusisitiza umuhimu wa umoja, kama Mwalimu Nyerere alivyosisitiza.
Si hivyo tu, fukuto za kujitenga zinazoibuliwa Scotland na Ireland ya Kaskazini kutokana na matokeo ya uamuzi wa nchi ya Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya, zinatufundisha kuwa jitihada za kujitenga na wengi zinaweza kuibua mtiririko tusioutarajia wa utengano mkubwa zaidi.
Waingereza walidhani wao ni wamoja. Kumbe ndani yao wamo wapiga kura wa Scotland na wa Ireland ya Kaskazini ambao nao wana dukuduku zao.
Mwalimu Nyerere alituambia kuwa Watanganyika tunaamini ni wamoja, kumbe tukianza kuchambuana tutajikuta tumo Wazanaki, Wamwera, Wakabwa, Wahaya, Wasukuma, na makundi mengine mengi tu.
Kwa kifupi, ubaguzi unazaa ubaguzi.