Takriban nchi 140 zimelitambua taifa la Palestina, kulingana na barua ya hivi majuzi kwa Umoja wa Mataifa.
Nchi hizo zinajumuisha wanachama wa Kundi la nchi 22 za Kiarabu katika Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi 57 za Ushirikiano wa Kiislamu na Harakati Zisizofungamana na Siasa zenye wanachama 120.
Uingereza na Marekani ni miongoni mwa mataifa ambayo hayaitambui rasmi taifa la Palestina.
Mapema mwezi huu waziri wa mambo ya nje Bwana Cameron alipendekeza kuwa serikali, pamoja na washirika wake, inaweza “kuangalia suala la kulitambua taifa la Palestina, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa”.
Israel haitambui utaifa wa Palestina na Serikali ya sasa ya Israel inapinga kuundwa kwa taifa la Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza. Inasema kuwa hali kama hiyo itakuwa tishio kwa uwepo wa Israeli.