Na Nizar K Visram
Maili 80 kutoka jijini London, Uingereza, ndege aina ya Boeing 767 ilikuwa inasubiri katika uwanja wa kijeshi wa Boscombe Down kuwachukua wakimbizi na kuwahamishia Rwanda bila ridhaa yao.
Hawa walitoka nchi mbalimbali kama Afghanistan, Iran, Iraq, Syria na kwingineko. Walitegemea kupata hifadhi Uingereza, lakini sasa wanapelekwa nchi ya Afrika iliyo umbali wa kilometa 9,000.
Ghafla ikaja amri ya zuio kutoka Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu (European Court of Human Rights – ECtHR), kwa hivyo ndege hiyo haikuondoka. Ndege ilitakiwa iondoke saa nne na nusu usiku wa Juni 14, mwaka huu. Ndege ilikodishwa na Serikali ya Uingereza kwa gharama ya dola 614,000.
Hapo awali idadi ya wakimbizi waliokusudiwa kusafirishwa walikuwa 130 lakini kutokana na kesi zilizofikishwa mahakamani dakika za mwisho, wengi wao waliondolewa na ndipo wakabaki saba tu. Miongoni mwa walioondolewa ni watoto watatu waliochanganywa kwa makosa na wakubwa. Pia aliondolewa mkimbizi aliyekuwa kamanda wa polisi nchini Iran.
Yeye alikataa kutii amri ya serikali ya kuwapiga risasi waandamanaji, kwa hiyo akalazimika kuomba hifadhi ya kisiasa Uingereza.
ECtHR ni mahakama ya kimataifa iliyoanzishwa mwaka 1959 na inashughulikia haki za kiraia na kisiasa katika nchi za Ulaya. Raia wa nchi hizo anaweza kufikisha malalamiko yake katika mahakama hiyo baada ya kumaliza ngazi zote katika nchi yake.
Kwa maneno mengine, mahakama hiyo ina uwezo wa kubatilisha hata uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ya Uingereza.
Na ndivyo ilivyofanyika katika ndege iliyozuiwa wakati ikisubiri kuelekea Rwanda. Wengine wanaweza wakauliza, kwani Uingereza si imejitoa kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU)? Ni kweli lakini mahakama hiyo ni kwa nchi zote za Ulaya hata kama ziko nje ya EU.
Kesi za wakimbizi hawa zilifikishwa Mahakama ya Ulaya baada ya Mahakama ya Uingereza kutoa idhini ya kusafirishwa. Hapo awali mahakama ya chini ilitupilia mbali ombi la kutaka kusimamishwa mpango wa kuwapeleka wakimbizi Rwanda.
Ndipo wakimbizi pamoja na wanaharakati wakaenda katika Mahakama ya Rufaa ya Uingereza. Nayo ikakubaliana na mahakama ya chini. Ndipo kesi ikafikishwa Mahakama ya Ulaya. Iliyo jijini Strasbourg (Ufaransa).
Pamoja na kesi kufikishwa mahakamani, kumekuwako upinzani mkali nje ya mahakama miongoni mwa wanaharakati na asasi za kiraia pamoja na mashirika ya kimataifa.
Kwa mfano, Juni 14 wanaharakati walilala barabarani jijini London kuzuia magari ya wakimbizi yasiwapeleke uwanja wa ndege. Maandamano pia yalifanyika jijini Manchester.
Pia asasi iitwayo Global Citizens ilitumia mtandao kuzishinikiza kampuni za ndege zisishiriki katika usafirishaji huo. Watu zaidi ya 120,000 waliunga mkono barua ya upinzani katika mtandao. Hata wafanyakazi wa uwanja wa ndege nao walishinikizwa wasishiriki katika mpango huu wa serikali.
Upinzani ulitoka hata kasri ya Bukingham wakati mwana mfalme Charles aliposema mpango huo ni wa kutisha. Naye mkuu wa Kanisa la Anglikana pia alipinga.
Wengi walipinga wakisema Rwanda yenye watu milioni 13 tayari ina wakimbizi 150,000 kutoka nchi za Kiafrika na kwingineko, wakiongezwa kutoka nje itawezekanaje?
Wengine walisema mpango wa Uingereza unahalifu makubaliano ya UN kuhusu wakimbizi yaliyosainiwa mwaka 1951. Kwa mujibu wa makubaliano haya nchi hairuhusiwi kuwafukuza wakimbizi au kuwahamishia kwingineko.
Upinzani ulitoka hata katika wizara ya mambo ya ndani inayoshughulikia wakimbizi na uhamiaji. Maofisa kadhaa wa wizara walitishia kugoma, wakisema kuwa mpango mzima ni kinyume cha maaadili na ubinadamu na ni aibu kwao kuutekeleza. Mabango yaliwekwa nje ya wizara yakieleza msimamo wao.
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Filippo Grandi, alikosoa uamuzi huo wa Uingereza wa kuwahamishia Rwanda watafuta hifadhi, akisema makubaliano hayo ya siri kati ya nchi mbili hizo ni makosa.
“Kuhusu Rwanda, nafikiri tumekuwa wawazi katika wiki chache zilizopita na tunaamini kuwa hili ni kosa kwa sababu kadhaa,” anasema Kamishna Mkuu huyo wa UNHCR.
Grandi anaendelea kubainisha kuwa, Rwanda ilikuwa na historia ya kipekee ya kukaribisha na kusaidia maelfu ya wakimbizi kutoka DRC na Burundi. Akaongezea kuwa nchi hiyo kwa hiyo haina uwezo na miundombinu ya kuwahudumia wakimbizi kwa kuzingatia mahitaji yao.
Akafafanua kwa kusema: “Ingekuwa ni kutoka Rwanda kwenda Uingereza, pengine tungeliweza kujadili, lakini hapa tunazungumzia Uingereza, nchi ambayo ina mifumo na inahamishia jukumu lake kwa Rwanda.”
Tangu Machi mwaka huu wakati muswada wa sheria ulipopitishwa na bunge nchini Uingereza, UNHCR ilisema sheria hii inakiuka sheria ya kimataifa inayohusu wakimbizi.
Mpango huu wa kuwasafirisha wakimbizi kutoka Uingereza kuwapeleka Rwanda (Asylum Partnership Arrangement) ulisainiwa nchini Rwanda Aprili 14, mwaka huu. Uingereza iliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Ndani, Priti Patel na Rwanda iliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Vincent Biruta.
Muda wa ushirikiano huu ni miaka mitano na gharama yake inakisiwa kuwa zaidi ya dola milioni 147. Sheria inasema lengo lake ni kuwasafirisha wakimbizi walioingia Uingereza bila ya kufuata sheria au kwa kutumia njia hatarishi au zisizo za kawaida, yaani kwa kutumia mitumbwi na mashua au malori.
Wakiwa Rwanda watapewa kazi, makazi na matibabu na wataendelea kuishi Rwanda wakipenda. Lakini hawataruhusiwa kurudi Uingereza. Uingereza imeahidi kuilipa Rwanda dola milioni 147.
Wachambuzi wanasema kinachofanyika hapa ni Uingereza kuwauzia Rwanda wakimbizi wake waliotoka Afghanistan, Libya, Somalia na Syria. Rwanda nayo itapokea malipo kwa kuwahifadhi wakimbizi hao.
Haiyumkiniki kuwa wakimbizi wa Ukraine nao ‘watauzwa’.
Wengine wanajiuliza, kwa nini Uingereza ikachagua Rwanda? Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AP, Uingereza ilianza kuzungumza na Albania, Gibraltar na Ascension. Nchi hizo zilikataa ndipo Uingereza ikageukia Rwanda, bila kujali kuwa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) Uingereza imesema Serikali ya Rwanda inakiuka haki za binadamu.
Mfano mmoja unaotolewa ni ubomoaji wa maelfu ya nyumba katika Wilaya ya Nyarutarama karibu na Kigali Machi 2020. Wakazi waliahidiwa nyumba mbadala lakini wengi wamekuwa wakilalamika kutokuwa na miundombinu na kuwa mbali kutoka mahali pa kazi. Wengine walisema hawakulipwa fidia waliyoahidiwa.
Wakati mmoja Australia iliwasafirisha wakimbizi wake hadi Nauru. UNCHR na mashirika mengine yaliilaumu Australia. Sasa na Uingereza nayo inarudia yale yale.
Rwanda inasema imetayarisha hoteli tano jijini Kigali watakapofikia wakimbizi 350. Tatizo ni kuwa tayari Rwanda ina wakimbizi zaidi ya 170,000 kutoka nchi kama DR Congo, Burundi, Libya na Afghanistan. Hawa wanaishi katika kambi sita nchini humo.
Halafu kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2020, karibu nusu ya kaya zote nchini Rwanda zina upungufu wa chakula na asilimia 37 ya watoto wana utapiamlo. Kwa upande wa uchumi, deni la nchi hiyo ni asilimia 73 ya uzalishaji wake (GDP).
Juu ya yote hayo, kuna hili tatizo kubwa la mapigano kutokana na shutuma za DRC kuwa Rwanda inaunga mkono waasi wa M23 nchini DRC. Matokeo yake mipaka imefungwa na biashara kati ya nchi hizo imesimama.
Hata hivyo, Balozi wa Rwanda nchini Uingereza, Johnston Busingye, aliandika makala katika Gazeti la Daily Telegraph, Juni 12, akisema kuwa nchi yake ina nia safi katika kuwapokea wakimbizi kutoka Uingereza. Akakanusha kuwa nchi yake haina uwezo wa kuwatunza, akisema ingawa Rwanda kama zilivyo nchi nyingine ina changamoto lakini; “ikumbukwe kuwa Rwanda ya leo si ile ya 1994 wakati wa mauaji ya kimbari.”
Naye Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, anasema: “Watu wanaweza wakawa na mawazo yao lakini kwa upande wetu sisi tunajaribu kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya ulimwengu kuhusu wakimbizi. Tunafanya hivyo kwa nia njema, kwani hatuamini kuwa kuwasaidia watu kupata hifadhi ni makosa.”
Naye Waziri Patel, baada ya safari ya ndege kufutwa, aliliambia Bunge la Uingereza kuwa serikali yake haitaacha kufanya mipango ya safari nyingine. “Jitihada hizo zitaendelea na mawakili wetu wamo mbioni kufuta zuio la mahakama. Hatutajali ghasia za mitaani.”
+1 343 204 8996 (WhatsApp)