Serikali ya Uingereza imesisitiza itahakikisha inasaidia sekta ya afya nchini ili wananchi wapate huduma bora hasa upande wa mama na mtoto.

Balozi wa Uingereza David Concar alisema hayo, wakati wa kumbukumbu ya miaka 70 ya Utawala wa Malkia wa Uingereza Queen Elizabeth ambapo pia amepanda mti kwenye Hospitali ya Wilaya ya Lulanzi, Mjini Kibaha.

Ameeleza kwamba ,kutokana na kuthamini sekta ya afya ameona umuhimu kuweka kumbukumbu kwenye Hospitali hiyo.

Amesema kuwa nchi ya Uingereza imekuwa na mahusiano mazuri na serikali ya Tanzania na wanajivunia ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.

“Tutahakikisha huduma bora za afya zinatolewa kwa kuendelea kusaidia na tunafurahishwa na utoaji huduma za afya na itapandwa miti 70 maeneo mbalimbali hapa Tanzania,”amesema Concar.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema kuwa nchi ya Uingereza ni moja ya nchi zenye uwekezaji mkubwa ikiwemo kwenye afya.

Amesema kuwa mkoa umepiga hatua kwenye suala la afya na suala la uzazi wa Mpango ni la watu wote si kwa wanawake pekee na wazazi wasiwaoze watoto wa kike kwani wanakosa haki zao za msingi.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkazi wa shirika lisilo kuwa la Kiserikali la Engender Health Dk Moke Magoma amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu ya kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza yatokanayo na kujamiiana, unyanyasaji wa kijinsia na kuharibika mimba.

Naye mganga mkuu wa mkoa wa Pwani Gunini Kamba amesema kuwa kwa mwaka 2019 matumizi ya uzazi wa mpango yaliongezeka kutoka asilimia 44 hadi asilimia 58 na lengo ni kufikia asilimia 60.