Kombe la soka la FIFA (Kombe la Dunia) limeanza kwa wiki zaidi ya moja sasa. Lilianza kwa kuwakutanisha wenyeji Russia dhidi ya Saudi Arabia kwenye uwanja wa Luzhniki jijini Moscow.
Nimekumbuka jamaa yangu mmoja ambaye, tofauti na mimi, hana ushabiki hata kidogo wa soka. Miaka michache iliyopita nilimsikia akishangaa wenzake wakizungumzia kwa hamasa kubwa wachezaji wa timu mashuhuri za Ulaya.
Aliwaona kama wenye ushabiki wa kufuata mkumbo tu. Kwa kuwa karibia kila mtu katika kundi lao ni shabiki wa timu mojawapo mashuhuri ya soka Ulaya, basi wanajitokeza mashabiki wa timu zote za ligi kuu za Ulaya. Ni mfano wa wale mashabiki wa Manchester United ambao, mathalani, ukiwafungulia ramani na kuwauliza waoenyeshe Manchester iko wapi, hawana uhakika pa kuanzia.
Tupo mashabiki wa aina nyingi wa soka, wenye ushabiki na uelewa unaotofautiana kwa kiasi kikubwa. Wengine tunaweza kuwa tunafahamu jiji la Manchester lipo nchini Uingereza, lakini bila kuwa na uwezo wa kutaja jina la hata mchezaji mmoja tu wa timu hiyo.
Ni mashabiki wa msimu, tusioangalia mechi hata moja ya soka kwenye runinga kwa miaka minne, lakini pindi kinapowadia kipindi cha Kombe la Dunia, basi hali inabadilika. Runinga inafutwa vumbi na kuhakikisha kuwa inatoa picha nzuri isiyo na chenga. Hali kadhalika, king’amuzi kinalipiwa kwa angalau mwezi mzima, tukisubiri kwa shauku kubwa kuanza kwa michuano.
Si muhimu kufahamu sana majina ya wachezaji wa timu zinazoshiriki, hao tutawafahamu mechi zikianza. Muhimu ni kuwa tunafahamu zipo timu zinazowakilisha Bara la Afrika na hujiandaa kuzishabikia timu wa mashindano hayo.
Tupo mashabiki wengi wa aina hii na tunajiandaa kwa kila namna kuhakikisha kuwa zile mechi muhimu tunaziona mubashar. Nimemsikia shabiki mmoja ambaye ni mfanyabiashara akipangua muda wake wa kusimamia biashara ili awepo nyumbani kushuhudia mechi muhimu.
Si wote wanaopunguza mapato kwenye kipindi hiki. Kwa baadhi ya watu kipindi cha Kombe la Dunia ni kipindi cha mavuno, tena mavuno makubwa.
Kwa muda mrefu kwenye maeneo ya vijijini wamiliki wa kumbi za video wamekuwa wakitoza mashabiki pesa kutizama mechi mbalimbali za soka za ligi kuu za Ulaya. Ni biashara inayopamba moto zaidi zinapoanza mechi za Kombe la Dunia kwa sababu mashabiki wa msimu nao hujitokeza kuungana na wale wazoefu.
Na kama zilivyo biashara zote, hutumika mbinu za kuhakikisha kuwa biashara, siyo tu inaingiza mapato, lakini inaingiza mapato mengi. Fursa inayojitokeza kila baada ya miaka minne ni fursa inayowekewa kila aina ya mikakati kuhakikisha inatoa matokeo mazuri.
Jambo moja ambalo limekuwa desturi kushuhudia kijijini pindi mashindano makubwa kama haya yanapoanza ni kukatika kwa umeme kiholela kwenye nyakati ambazo mashabiki wanajiandaa kutizama mechi zinazoendelea.
Sikumbuki katikakipindi cha hivi karibuni umeme kukatika mara kwa mara, lakini sitashangaa tukirejea kwenye kipindi cha mgao wa umeme hasa mechi zinapokaribia kwenye utamu zaidi.
Tumeshuhudia kirusi cha kukatika umeme kiholela ambacho huambatana na kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia.
Kukatika umeme inapochezwa mechi iliyosubiriwa kwa shauku kubwa ni kitendo kinacholazimisha baadhi ya mashabiki kutoka majumbani na kuhamia kwenye kumbi za video, zilizojiandaa kutumia jenereta kuzalisha umeme mbadala. Umeme wa uhakika ni furaha kwa baadhi ya waliopo nyumbani, lakini si jambo la kufurahia hata kidogo kwa mmiliki wa ukumbi wa video au runinga.
Haupo ushahidi wa moja kwa moja kuwa yapo makubaliano ya chini ya meza kati ya wamiliki wa kumbi na mzima swichi wa TANESCO kuwa umeme ukatwe kwa baadhi ya mechi ili wamiliki wa kumbi waongeze ufanisi wa biashara yao.
Lakini, kama ambavyo waendesha mashitaka hupenda kusema, yapo mazingira yanapojitokeza watu wakaanza kuamini kuwa makubaliano hayo bila shaka yapo na mtuhumiwa anapaswa kukutwa na hatia.
Washabiki wa msimu hawawezi kuwa sababu ya wahusika kukosa usingizi kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika upo kipindi cha michuano. Lakini kwa bahati nzuri umeme ukikatwa, unakatwa kwa wote, wale wasio muhimu na wale wanaoutumia kwa masuala muhimu.
Huduma nyingi muhimu, kama za afya, zinahitaji umeme wa uhakika. Tatizo ni kuwa si kila mtoa huduma muhimu ana uwezo wa kununua jenereta ya kuzalisha umeme mbadala.
Kwa hiyo hujuma yoyote inayothibitishwa kukatisha umeme kwa makusudi, iwe kwa matumizi muhimu au kwa matumizi ambayo si ya muhimu ni hujuma sawa na hujuma inayofanywa na mwizi wa waya za umeme wa TANESCO, au mwizi wa mafuta ya transfoma ambaye, si tu anahatarisha transfoma kulipuka na kusababisha hasira kubwa, lakini pia anahatarisha afya na maisha ya watu kwa kutumia mafuta yale kukaangia viazi na kuwauzia watu kula.
Kwa haraka haraka linaweza kuonekana kuwa ni tatizo dogo, lakini athari zake ni pana na zinavuka mahitaji binafsi ya mashabiki wa msimu wa soka.
Ingekuwa vyema sana kama Tanzania ingekuwa Brazil au nchi nyingine ambako soka ni suala nyeti kabisa na masuala ya hujuma kama hizi yangesababisha vigogo kutumbuliwa. Wala isingejitokeza haja ya kujenga hoja pana ili kutumbua wahusika wanaohujumu upatikanaji wa umeme wa uhakika kwenye kipindi hiki cha michuano.
Lakini hii ni Tanzania kwa hiyo tatizo likijitokeza tutaanza kuguna sana, tena sana tu.