DODOMA.
EDITHA MAJURA.
Serikali na Vyombo vya habari, wametuhumiana kuminya uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Wakati serikali ikituhumiwa kutofanya vizuri katika kudhibiti usalama wa wanahabari wanapotekeleza majukumu yao, serikali nayo imesema vyombo vya habari vinaminya maslahi ya wanahabari kiasi cha kusababisha washindwe kutekeleza majukumu yao kwa weledi unaohitajika.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, akijibu hoja za wadau wa tasnia hiyo kutoka ndani na nje ya nchi, amesema mijadala kuhusu vikwazo vya uhuru wa vyombo vya habari ifanyike kwa wigo mpana badala ya kuilenga serikali peke yake.
Dk. Mwakyembe, alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, maadhimisho hayo hufanyika Mei 03 kila mwaka, ambapo mwaka huu kwa mara ya kwanza yamefanyika kitaifa jijini Dodoma.
“Nawapongeza waandishi wa habari wa Tanzania, wana roho ngumu sana yaani wanakufa na tai shingoni, mfumo wao wa ajira unawageuza mabubu, hawawezi kudai maslahi yao ingawa wapo mstari wa mbele kudai maslahi ya wengine, wakiwemo wanaowaminya,” amesema Dk. Mwakyembe.
Amesema makongamano mengi yanayofanywa na wadau wa tasnia ya habari yananyooshea kidole serikali, wakiihusisha na kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari, huku wakifahamu kuwa dhana hiyo haina ukweli.
Dk. Mwakyembe amesema kikwazo kikubwa cha uhuru wa vyombo vya habari, ni mfumo wa ajira yao unaong’ang’aniwa na vyombo hivyo na ameshauri makongamano yanayohusu taaluma hiyo kubadilika kwa kuanza kujadili vikwanzo vya uhuru wa habari kwa wigo mpana, hususan kwa kuanzia ndani ya vyombo vya habari vyenyewe.
“Mwandishi anakwenda kutafuta habari huku akitegemea nauli na posho kutoka kwa chanzo cha habari (mtoa habari), unategemea kupata habari gani kama siyo ukasuku?” amesema Dk. Mwakyembe.
Ametaka wamiliki wa vyombo vya habari kubadilika, waanze kujali maslahi ya wanahabari badala ya kuwa na ‘jeshi kubwa la ombaomba’ akaagiza wanahabari waajiriwe kwa kuzingatia viwango vya elimu vinavyoainishwa katika sheria na walipwe maslahi stahiki na kwa wakati.
Hata hivyo, pande hizo mbili zimeafikiana kuwa ni muhimu kuwa na jukwaa la mawasiliano lenye tija kwa wanataaluma hiyo kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla kwani ‘kalamu’ ina nguvu na athari zake huwa mbaya au nzuri kutegemeana na inavyotumika.
Kwa upande wa Jukwaa la Wahariri (TEF), kupitia Kaimu Mwenyekiti wake, Deodatus Balile, limetoa mifano kumi kati ya matukio mengi yanayominya uhuru wa vyombo vya habari, yaliyotokea nchini ndani ya mwaka wa kihabari uliyomalizika.
“Polisi kwenye Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Iringa na Dodoma wamekuwa wakinyang’anya simu, kuwaweka chini ya ulinzi na kuwaachia bila kuwafikisha mahakamani hali ambayo inawatia wasiwasi wa kudumu katika kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma,” amesema Balile
Matukio mengine yaliyotajwa na TEF katika taarifa yake ni kupotea mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda tangu Novemba 27, 2017 hadi wakati taarifa hiyo ikitolewa haikuwa ikifahamika alipo, watendaji wa vyombo vya habari kuitwa na kuhojiwa na mamlaka na baadhi ya vyombo kutozwa faini kubwa bila sababu za msingi.
Tukio jingine ni mwandishi Ansbert Ngurumo, kutoroka nchi na kuishi uhamishoni akihofia ‘watu wasiojulikana’ ambao wamekuwa tishio na wamejenga hofu kwa wanataaluma hiyo huku sehemu ya vipindi vya Bunge, kuzuiwa kutangazwa mubashara ikielezwa kuwa ni kunyima wananchi haki yao ya kupata habari.
TEF imemshitaki Waziri Mwakyembe kwa Rais, John Magufuli, kuwa anatumia vibaya kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma Vyombo vya Habari kinachompa mamlaka ya kuzuia maudhui, lakini yeye amekuwa akikitumia kufungia magazeti.
Naye mwanahabari mwandamizi nchini, Ndimala Tegambwage, amewataka wanahabari kusoma alama za nyakati kwa kutumia lugha zenye staha, kufikisha ujumbe unaokusudia kukosoa na kurekebisha serikali ili malengo ya kitaaluma yafikiwe bila kusababisha athari kwa pande zote zinazohusika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Fausta Musokwa, amehimiza jamii kwa ujumla kuhakikisha inawezesha nchi kuwa na vyombo vya habari vyenye uhuru na vilivyo imara, kwasababu hali ikiwa kinyume, amani, utulivu, maendeleo na mshikamano havitapatikana.
“Kuna wakati natamani kuwapa mfano kwa kuwaomba tufanye hivi, sote humu ndani tufumbe macho, tuzibe masikio, tufunge mikono yetu nyuma kisha tuanze kutembea hatua kwa hatua kila mmoja akitoka alipo kwenda mwanzo wa chumba hiki, ila shaka haitawezekana tutaishia kukanyagana na kupiga kelele na hivyo ndivyo ilivyo jamii isiyo na vyombo vya habari huru na imara,” amesema Musokwa.
Sambamba na maadhimisho hayo yamefanyika maonesho ya vyombo vya habari pamoja na taasisi nyingine za kihabari, ambapo kwa nyakati tofauti zilitembelewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
Akiwa katika banda la gazeti la JAMHURI, Spika Ndugai, amesema amekuwa ni msomaji wa gazeti hilo kutokana na habari za kusisimua zinazoandikwa na JAMHURI.
“Ninyi ni wazee wa kutumbua…hata bwana mkubwa anawatambua kwa jambo hilo. Kwa kweli ninapenda sana namna mnavyofanya kazi kwa weledi wa hali ya juu,” amesema Ndugai.
Naye Dk. Mwakyembe, alipotembelea banda hilo na kukutana na viongozi wa gazeti la JAMHURI, hakusita kuelezea hisia zake kwa kusema, JAMHURI limejijengea umaarufu mkubwa miongoni kwa magazeti mengi hapa nchini kwa kuandika habari za uchunguzi.
“Gazeti la JAMHURI mnafanya kazi nzuri sana…ukitaja magazeti manne ‘serious’ hapa nchini huwezi kulikosa gazeti la JAMHURI. Kwa kweli endeleeni kuchapa kazi kwa kuzingatia misingi ya weledi,” amesema Dk. Mwakyembe.
Vyombo vingine vya habari vilivyoshiriki maonesho hayo ni Majira, Mwananchi pamoja na Uhuru. Huku taasisi zinazojishughulisha na masuala ya habari ni Wakfu wa vuyombo vya habari Tanzania (TMF), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha Wanasheria (TLS),