Gazeti la JAMHURI ni miongoni mwa midomo, macho na masikio ya Watanzania na wadau wengine wa habari. Uhuru wa habari – ambao dunia yote inautangaza na kuuenzi kwa sasa – ni haki ya kila raia na chombo cha habari.
Pamoja na JAMHURI, yapo magazeti mengine yaliyolitangulia na yanayokuja baada yake, kwa malengo mahsusi ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii. Hiyo ndiyo kazi ya magazeti, redio, televisheni na vyombo vingine vya habari. Licha ya dunia kuwa kama kijiji kutokana na utandawazi, kuna nguvu zinazotumika kuturejesha kwenye ujima.
Sheria mbovu na kanuni zinazosimamia vyombo vya habari ni miongoni mwa vigingi vinavyotakiwa kuondolewa haraka iwezekanavyo, ili wananchi wafurahie hasa uhuru wao. Magazeti mbalimbali yaliangukiwa na rungu la dola kupitia kwa maofisa waliopewa kazi za kusajili, kusitisha na kufuta vyombo hivyo muhimu.
Machache ninayokumbuka ni Majira na MwanaHALISI, wakati Tanzania Daima iliwahi kupewa karipio au maonyo. Hali hiyo si nzuri wala haitii moyo kuhusu suala zima la utawala bora wa sheria, demokrasia na uhuru wa maoni na habari kwa ujumla wake. Bila kujali uhuru huo unatumiwaje, hakuna ruhusa yenye baraka za walio wengi za kuufunga. Linapotokea kosa kuna namna ya kusahihishana na wala si kutumia mabavu.
Huwa nacheka kwa jinsi viongozi wetu wanavyokuwa ndumilakuwili kuhusu mambo. Wakati mwingine watakwambatia mfumo wa kununua bidhaa, urasimu na ukiritimba serikalini, ukiuliza wanakwamba ni sheria zetu zilivyo, maana tumezinakili huko Uingereza na ndugu zao Marekani au labda Jumuiya ya Madola.
Lakini likija suala la uhuru wa vyombo vya habari, wakubwa wetu wa habari wanajifumbata kwenye kwapa za sheria mbovu, katili na kandamizi kama ya magazeti ya mwaka 1976. Wanatulia hapo tuli. Ukiwauliza hivi na kwa hapa Uingereza mnayojificha haipo? Wangekuwa wajanja wangesema kwapa zake hazitoshi, lakini watakwambia sisi tulishapata uhuru bwana, tunajitegemea wenyewe.
Lakini ukiangalia ni jambo zuri sana kufuata sheria za wenzetu ambazo ni nzuri – kama ya uhuru wa vyombo vya habari ni jambo zuri zaidi kuepuka zile mbaya kama za mambo ya manunuzi na kadhalika. Marekani inaongoza dunia nzima kwa uzuri wa sheria ya vyombo vya habari, na Uingereza ikiwa sambamba nayo. Huwezi kutishia hivi hivi tu kufungia gazeti. Eti mtu amelala, akiamka na kwa kushauriana na wale anaowajua yeye mwenyewe na kwa sababu zake, anafungia gazeti bila kusema hadi lini.
Hapa London sasa watu wanacheka kweli, wanamcheka mjukuu wa malkia aliyesaula vinguo vyake vyote huko Marekani na akapigwa picha na visichana alivyokuwa navyo akiwa uchi wa mnyama! Unaambiwa hakuna waziri, mbunge, msajili wa magazeti, mkurugenzi wa Maelezo ya huku (kama ipo) au katibu mkuu kutoka na kuzuia au kuchukulia hatua waliochapisha picha zile.
Gazeti la The Sun la Uingereza imeziweka vizuri kabisa, Prince Harry akiwa uchi wa mnyama, lakini ameweka mikono yake mbele chini ya tumbo. Picha nyingine ninayo kwenye gazeti hapa amemwegemea changudoa aliyemwokota nje ya hoteli ambayo chumba alicholala Las Vegas ni pauni 5,000 kwa usiku mmoja.
Hii amepigwa picha kwa nyuma, kwa hiyo makalio yalikuwa wazi kabisa kwenye picha ya orijino. Wao kwa ajili ya ubinadamu tu na pia kuepusha kinyaa kwa wasomaji wao, wakapafunika pale, lakini kama bezo wakapachika pale nembo ya taji la kifalme! Kasri ya Kifalme ya hapa ilijaribu kutafuta mawakili maarufu na ghali zaidi ili kuona (kabla ya kuchapishwa) kama wanaweza kuzuia kuchapishwa picha, lakini linabaki suala la kuzozana tu, ikiwezekana watashitakiana binafsi kudaiana basi.
Niambie ingekuwa hapo picha za mtu aliyefanya madudu yake zinawekwa hivyo, ungeshangaa kwanza nakala zote zinanunuliwa na kuchomwa moto, kama maofisa usalama wangechelewa kuzuia huko kiwandani. Huyu ni mtu wa tatu katika ngazi ya kukifikia kiti cha ufalme wa Uingereza, lakini anapelekeshwa kama mtu mwingine yeyote. Haki sawa kwa wote, uhuru wa habari kwa kila mmoja.
The Sun iliweka vizuri kitu kimoja, kwamba picha zile zimetokea huko Marekani, habari imesikika, Prince Harry yu uchi na wateja wa The Sun walikuwa na haki ya kuziona kukata kiu yao, nao wametimiza wajibu wao kuwapatia wateja wanachohitaji. Hakuna mambo ya siri, kulindana na kufungia wanaochunguza, kubaini na kuweka wazi uovu au ukiruka njia wa namna yoyote.
Tuwasiliane tafadhali – [email protected]