Denis Galava alikuwa mhariri katika gazeti la Nation linalochapishwa kila siku jijini Nairobi.
Hili ni gazeti linalomilikiwa na Kampuni ya Nation Media Group (NMG), pamoja na mengine yaliyoko Uganda na Tanzania.
Mmiliki wake mkuu ni Aga Khan. Moja ya majukumu ya Galava ilikuwa ni kuandika tahariri. Mwishoni mwa 2015 ikaamuliwa kuwa aandike tahariri maalum kuukaribisha mwaka mpya wa 2016.
Alitumia muda wa saa sita akifanya utafiti katika maktaba, akisoma habari kuhusu mwaka 2015. Akakuta habari kuhusu skandali, migomo ya wafanyakazi, mashambulizi ya kigaidi, kutetereka kwa uchumi na kadhalika.
Mwishowe akaamua huo ulikuwa mwaka wa maumivu na mateso kwa wananchi wa Kenya.
Akaandika tahariri ikiwa katika mfumo wa barua kwa Rais Uhuru Kenyatta, ikisema: “Mheshimiwa Rais, jirekebishe katika mwaka huu wa 2016.”
Akamkumbusha Rais kuwa anasahau ahadi alizotoa kabla ya kushika madaraka mwaka 2013. Akaendelea: “Mheshimiwa Rais, mwaka 2015 ulikuwa ni mbaya kwa Wakenya. Misingi ya taifa letu imetikisika na kuingia nyufa. Familia chache za matajiri zimekuwa zikizoa mabilioni kupitia zabuni za ajabu kwa ushirikiano wa wanasiasa. Mwananchi anaachwa nyuma, mamilioni wanakosa ajira na idadi yao inaongezeka.”
Galava akabuni neno la kimombo’ tenderpreneurs’ kwa maana ya ‘wajasiriazabuni’ badala ya ‘wajasiriamali’ kuelezea tabaka la mafisadi wanaochota mabilioni kupitia tenda/zabuni bandia za serikali.
Alimradi Galava hakumung’unya maneno. Alisema yale aliyokusudia Januari 2, 2016. Tahariri hiyo ikachapishwa katika gazeti la ‘Nation.’ Mara moja mitandao ya jamii ikafurahia na kumpongeza Galava kwa kusema ukweli. Lakini si wote waliofurahi.
Siku iliyofuata Mhariri Mtendaji wa NMG (wikiendi), Eric Obino alimwita na kumwambia kuwa tahariri hiyo ilikuwa na maneno makali ingawa ni ya ukweli.
Baadaye Afisa Mwandamizi kutoka Ikulu ya Nairobi alipigia simu ofisi za NMG na kusema Mheshimiwa Kenyatta alikuwa amekasirishwa na anakusudia kumueleza Aga Khan ambaye ni mmiliki wa NMG.
Mhariri Mkuu wa NMG, Tom Mshindi akawa na wakati mgumu. Bila shaka mengi yalizungumzwa kati yake na Bodi ya Kampuni kwani siku tano baada ya tahariri kuchapishwa Galava akaitwa na bosi wake Tom Mshindi. Akamtaarifu kuwa anasimamishwa kazi. Januari 20, akaambiwa anafukuzwa kazi.
Galava aliambiwa kosa lake ni kutofuata utaratibu wa kushauriana na wakuu wake kabla ya kuchapisha tahariri. Yeye akajibu kuwa amewahi kuandika tahariri zaidi ya 100 na hajawahi kuelezwa kuhusu huo ‘utaratibu’.
“Huo utaratibu haukuwepo, ulibuniwa wakati nikisimamishwa na kufukuzwa,” akaongeza Galava. Anasema ukweli ni kuwa mabosi wake wamekuwa wakimkanya asiendelee kufichua kashfa za NYS, Eurobond na kahawa.
Walimwambia kashfa hizo zinahusishwa na muungano wa vyama (Jubilee) unaoongozwa na Rais Kenyatta. Hicho ndicho chanzo cha kufukuzwa kwake na wala si kutofuata taratibu.
Inakisiwa kuwa nchini Kenya asilimia 40 hadi 50 ya mapato ya vyombo vya habari yanatokana na matangazo ya serikali na mashirika yake. Hii inatumika kama njia ya kuwadhibiti wahariri.
Hata kampuni kubwa nazo zinatumia mbinu hiyo hiyo. Mwanaharakati wa Chama cha Wahariri nchini Kenya amesema, kwa mfano, ni vigumu kuandika habari zikizikosoa kampuni za mawasiliano na benki.
Akaongeza kuwa wakati huo huo vyombo vya habari vinazidi kuhodhiwa na matajiri wachache.
Hivyo, kampuni mbili za habari nchini zinamiliki magazeti 13, vituo vya redio vitatu, na vituo vya TV vitatu. Mara nyingi wanasiasa na watawala wanakuwa na hisa katika kampuni hizi.
Kwa maneno mengine, wamiliki wa magazeti na TV wakiwa wafanyabishara na wawekezaji, basi ni muhali kwa vyombo hivyo vikahatarisha maslahi yao ya kibiashara na kisiasa. Katika hali kama hiyo ni vigumu kuzungumzia uhuru wa habari.
Galava sasa amewasilisha kesi mahakamani, akiishitaki NMG kwa kumfukuza kazi kinyume cha sheria. Anadai fidia ya Sh milioni 400 za Kenya. Katika mashtaka yake anasema: “Naamini kuwa Mhariri Mkuu amekwepa weledi na wajibu wake kwa kunisimamisha kisha kuniachisha kazi ili kujikomba kwa vigogo wa kibiashara na kisiasa.”
Hata hivyo, utawala wa NMG umekanusha kwa kusema kuwa Galava alikuwa amekiuka taratibu na kanuni za kuchapisha tahariri. Galava anasema huo utaratibi haukuwepo na ulibuniwa baada ya yeye kusimamishwa.
Katika kesi yake anadai kuwa Tom Mshindi aliwahi kumuonya kuwa aache kuandika habari za skandali, hasa zile zinazohusu chama tawala cha Jubilee na Rais Kenyatta.
Anasema alikataa agizo hilo kwani lingewavunja moyo waandishi wanaofanya kazi chini yake. Galava anasema siku chache kabla ya Aga Khan kuwasili Kenya kama mgeni rasmi katika sherehe ya Jamhuri Disemba, 2015, Tom Mshindi alimuita na kumwambia makala za kashfa zisimamishwe.
“Akaniambia kuwa serikali inaweza kukasirishwa na hivyo kuikosesha NMG mapato,” akaongeza Magazeti ya NMG yamekuwa yakisifika nchini kwa msimamo wake wa kutetea haki na ukweli.
Msimamo huu ulianza katika awamu ya Rais Daniel arap Moi, ambaye alitawala kimabavu kwa muda wa miaka 24 chini ya chama chake cha KANU. Nation ilithubutu kusema ukweli na hata kumkosoa Moi.
Gazeti likajenga umaarufu na likawa linaongoza katika sekta ya habari. Moi alidai kuwa utawala wake ni “demokrasia ya chama kimoja”. Wakati huo alikosolewa na watu wengi, pamoja na viongozi wa dini waliofichua udikteta wake.
Mwishowe wafadhili walisimamisha misaada ya dola milioni 350. Ndipo Moi akatii amri na kuanzisha uchaguzi wa vyama vingi. Hiyo ikawa ni fursa ya kumwondoa madarakani, licha ya jitihada zake za kuwagawa wananchi katika misingi ya kabila na dini.
Pia, alifanya jitihada za kuchakachua matokeo ya uchaguzi, lakini akashindwa. Baada ya Moi akaja Mwai Kibaki kuanzia 2002 hadi 2013. Inasemekana chini ya utawala wake vyombo vya habari vilipewa nafasi ya kupumua.
Lakini Kenyatta alipoingia Ikulu mwaka 2013 mambo yakaanza kuharibika na wengi sasa waamini kuwa Kenya inarudia mfumo wa zamani Katiba ya Kenya ya mwaka 2010 kwa kuminya uhuru wa habari.
Hata hivyo, tangu muungano wa vyama vya Jubilee (sawa na Ukawa ya hapa petu) kuchaguliwa mwaka 2013, Rais Kenyatta amepitisha sheria zinazominya uhuru huo.
Kwa mfano iwapo mwandishi anaandika habari ambayo inakisiwa kuwa inadhoofisha jitihada za kupambana na ugaidi, basi anaweza kuwekwa gerezani miaka mitatu na kutozwa faini ya shilingi za Kenya milioni 5.
Asasi za wanahabari zikapinga sheria hizo mahakamani na kesi inaendelea. Wakati huo huo, wanaharakati wanasema waandishi wanaendelea kudhalilishwa. Asasi ya Freedom House (Kituo cha Uhuru) mwaka 2014 imeripoti kuwa waandishi wasiopungua 19 walishambuliwa.
Mmoja kati yao ni John Kituyi ambaye alipigwa hadi kufa mjini Eldoret, Aprili mwaka jana. Wauaji waliondoka na simu yake wakaacha fedha na saa ya mkononi.
Leo Kenya inashika nafasi ya 100 kati ya nchi 180 katika uhuru wa habari. Mwaka 2002 ilikuwa ya 75, yaani kiwango chake kimeporomoka.
Pia mwaka 2013 wanahabari takriban 300 walihojiwa kote nchini. Zaidi ya asilimia 90 walisema wamewahi kutishwa kutokana na kazi zao. Wengi wao walisema kutokana na mazingira hayo waaandishi wameamua kujizuia kuandika habari za kashfa.
Tukiachia kufukuzwa kwa Galava, mwingine aliyeachishwa kazi hapo Nation ni mchoraji maarufu wa vibonzo anayejulikana kama Gado. Huyu ni Mtanzania aitwae Godfrey Mwampembwa ambaye amekuwa na NMG tangu 1992.
Mwishoni mwa mwaka jana aliitwa na Tom Mshindi na kuambiwa kuwa mkataba wake umemalizika. Alipouliza sababu aliambiwa “wao wameamua” Alipouliza ni nani hao hakupata jibu.
Mara kadha Gado amewahi kuchora vibonzo vilivyowakwaza watawala wa nchi za Afrika Mashariki – kuanzia Kenyatta na Museveni hadi Kikwete.
Kufukuzwa kwa Gado kumelaaniwa na Asasi ya Kimataifa ya Kutetea Haki za Wanahabari (PEN) na matawi yake nchini Kenya na Afrika Kusini.
Mchoraji maarufu wa vibonzo nchini, Afrika Kusini aitwae Zapiro naye amelaani kufukuzwa kwa Gado.