Uhuru ni uwezo au haki aliyonayo mtu binafsi, jumuiya au taifa ya kujiamulia mambo yake kwa hiari yake bila kuingiliwa na mtu au taifa jingine.
Kuna uhuru wa mtu binafsi, ambao humpa haki ya kuishi akiheshimika sawa na watu wengine. Mtu binafsi huwa na haki ya kutoa mawazo yake, kufuata dini anayoipenda na kushiriki katika uamuzi wa mambo yote yanayohusu maisha yake na jamii yake.
Kuna uhuru wa wananchi wa kutosumbuliwa na ujinga, maradhi na umaskini. Wananchi wanakuwa na sauti ya pamoja katika kuacha utegemezi wa utawala wa watu wengine. Wanakuwa na haki ya kupanga mipango ya maendeleo yao.
Wananchi wanapokuwa huru wanajenga umoja na mshikamano na kutambua kuwa bila uhuru haupati maendeleo, na bila maendeleo uhuru wao unapotea. Maendeleo yoyote hupatikana mahali penye mazingira ya haki na uhuru.
Kuna uhuru wa nchi au taifa ambao huwa na uwezo wa kisiasa unaotumika kuendesha nchi na maendeleo ya wananchi katika siasa, uchumi, utamaduni na ustawi wa jamii. Taifa huwa na uwezo wa kuamua, kupanga na kutekeleza mipango ya uchumi na maendeleo ya taifa.
Uhuru wa mtu binafsi, uhuru wa wananchi na uhuru wa taifa hauna maana iwapo hakuna juhudi za kujenga uchumi imara na kuinua kiwango cha elimu cha wananchi katika fani zote za maisha. Hii ina maana elimu na uchumi vitajengwa iwapo uhuru wa aina zote zitashirikishwa pamoja.
Dunia inao wanafalsafa wengi katika fani mbalimbali zikiwemo za siasa, sheria, ustawi wa jamii na kadhalika, ambao wamepata kuzungumzia maana, faida, gharama na matumizi ya uhuru katika kuleta maendeleo ya mtu binafsi, jumuia au taifa. Hapa nawataja wawili miongoni mwao.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kitabu chake ‘UHURU NA MAENDELEO’ anasema: “Uhuru na Maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana, uhusiano wao ni sawa na uhusiano baina ya kuku na yai! Bila ya kuku hupati mayai, na bila mayai, kuku watakwisha. Vilevile, bila ya uhuru hupati maendeleo, na bila maendeleo ni dhahiri kwamba uhuru wako utapotea!” Mwisho wa kunukuu.
Mwanafalsafa wa pili ni Jiddu Krishnamurti kutoka India, ambaye alizaliwa Mei 13, mwaka 1895 na kufariki dunia Februari 17, mwaka 1986. Yeye alitamka: “Ni ukweli ndio unaokuweka huru na si juhudi zako katika kujikomboa.” Mwisho wa kumnukuu.
Wanafalsafa hawa wanatufahamisha mtu kuwa huru ni jambo jema kwake, kwa wenzake na kwa taifa. Uhuru unakupa uwezo wa kujiletea maendeleo. Uhuru una asili ya ukweli. Na ukweli wako au wenu utawawezesha kupata maendeleo muyatakayo, mkisindikizwa na juhudi katika madhira ya kujikomboa.
Watu tunataka maendeleo na tunapenda kuwa huru, tusibughudhiwe katika mipango, mikakati na harakati za kujenga maisha mazuri na bora. Tunataka heshima na kuheshimiwa, kushika madaraka na kuongoza wananchi au taifa. Picha hizi zinaonekana kila siku katika taasisi za kazi na vyama vya siasa.
Jambo la kushangaza, ama tunashindwa kusoma na kutambua maana ya picha hizi au hatutaki kuziona na tunazipuuza kwa hisia kuwa hazina tija! Lakini pembeni tunalalama, tunanung’unika na kusononeka kwamba hatuna uhuru. Je, kati ya haya, yapi ni dhahiri?
Kuepukana na hali ya manung’uniko, lawama na sononeko, ni busara kutambua vitu vinavyotukwaza kupata mambo mema tuyatakayo, ni uhuru ambao ni haki, ukweli ambao ni nyenzo, na kufuata au kutii kanuni na taratibu za uhuru. Kwa vipi?