Watanzania jana waliadhimisha miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara). Maadhimisho haya yamekuja huku Afrika na dunia ikiwa katika simanzi kubwa kutokana na kifo cha Mzee Nelson Mandela (95), Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini.
Matukio haya mawili yanatoa changamoto nyingi kwa viongozi wa Tanzania, Afrika na dunia. Mzee Mandela atakumbukwa daima kwa kusimama imara kuhakikisha Waafrika Kusini ambao ndiyo wengi nchini humo, wanatendewa haki kama ilivyo kwa Wazungu wachache.
Mandela ni alama ya ukombozi, si Afrika Kusini tu, bali kwa bara zima la Afrika na kote duniani ambako kuna watu wanaonyanyaswa kutokana na rangi, jinsi au hali zao. Tanzania ina mchango mkubwa sana katika ukombozi wa Afrika Kusini.
Wakati tukiadhimisha miaka 52 ya Uhuru wetu, na tukiwa kwenye simanzi ya kifo cha Mzee Mandela, tunapaswa kujiuliza kama kweli malengo ya kudai Uhuru tunaendelea kuyatekeleza.
Uhuru wa bendera pekee si uhuru. Uhuru wa kweli ni ule unaowatoa wananchi kwenye adha za kuonewa, kunyanyaswa, kupuuzwa, kunyimwa uhuru wa demokrasi na kuwafanya wawe huru kujiamulia mambo yao wenyewe kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya taifa lao.
Tanzania, kama ilivyo Afrika Kusini na mataifa mengi katika Bara la Afrika, uhuru tunaoufaidi ni uhuru wa bendera tu! Bado hatujawa huru kiuchumi.
Ndiyo maana miaka 52 baada ya Uhuru wa Tanganyika, na miaka 19 tangu Afrika Kusini iwe na utawala wa walio wengi, bado Waafrika weusi hawajawa huru kiuchumi. Kwa nchi kama Afrika Kusini hali hiyo inaweza kuwa na sababu za msingi ambazo ni rahisi kuzikubali. Lakini kwa nchi kama Tanzania, hakuna sababu za msingi za kutufanya tuendelee kuelea kwenye lindi la umasikini uliopindukia.
Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi tatu zinazopokea misaada mingi zaidi miongoni mwa mataifa yote “masikini” duniani. Tanzania ikiwa na idadi kubwa ya masikini, ni moja ya nchi zenye rasilimali nyingi sana katika Afrika na duniani.
Pengo kati ya masikini na matajiri linakua kwa kasi. Idadi ya vijana wasio na ajira inaongezeka. Huduma za kijamii haziendani na kasi ya ongezeko la watu.
Kinachoonekana katika Tanzania ya miaka 52 ni kundi la weusi wachache kuwa mawakala wa wageni wanaokuja kuchota utajiri. Rasilimali ya madini ya kila aina, wanyamapori, mito, bahari, maziwa, milima, misitu, gesi na nyingine nyingi zinawanufaisha zaidi wageni kuliko Watanzania.
Tunashuhudia wageni wakichota mali na kutoa misaada midogo midogo ya kuwadhalilisha wananchi kama vile vyoo, madawati au kugharimia safari za “mafunzo” za wanasiasa. Hii ni aibu.
Wakati tukiadhimisha miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika, tunapaswa kutafakari maisha, malengo na maudhui ya mababa wa ukombozi katika Afrika. Tunapaswa kurejea kwenye misingi ya viongozi miamba ya Afrika, ambao walipigania Uhuru kwa kutaka kuona Afrika inapiga hatua mbele kimaendeleo.
Moja ya mambo yatakayotuwezesha kufikia hatua hiyo, ni kuwa na viongozi waadilifu na walio tayari kuwatumikia wananchi wao kama walivyokuwa Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Nelson Mandela. Uhuru wa kiuchumi una manufaa makubwa pengine kuliko uhuru wa kupeperusha bendera tu.