Unaponyima haki kutendeka ukweli unaruhusu dhuluma na unabariki upendeleo kutawala unafsi. Ni sawa na kufanya choyo, hiyana na batili kwa mtu mwengine.
Uamuzi au tendo la jambo kama hilo, ukweli unahalalisha chuki kujijenga, unaruhusu mgawanyiko wa watu na unavunja udugu, umoja na mshikamano ndani ya familia, koo, kabila, jumuiya au taifa.
Haki ni ya Mwenyezi Mungu na ameipa kila kiumbe alichokiumba. Viongozi wa dini, viongozi wa jamii, wataalamu wa sheria, wanasheria, majaji na mahakimu na vyombo mbalimbali vya haki, ukweli ni wasimamizi wakuu kuona haki inatendeka kati ya kiumbe na kiumbe ndani ya dunia yake aliyeiumba.
Kuzuia haki ya mtu yeyote ni kumkosea Mwenyezi Mungu. Ndiyo maana viongoi wa dini wanahubiri kufanya hivyo ni dhambi. Kwa maana unakataa kutii amri ya Mola wako ambaye anakupa pumzi ya kila siku. Anakujaza fahamu kila nukta. Anakupa nguvu na uamuzi juu ya matendo yako na anakupa riziki mchana na usiku.
Haki ina historia ndefu tangu kuumbwa binadamu wa kwanza. Kutokana na ongezeko la watu na maendeleo ya jamii duniani ndipo tulipoanza kupata tafsiri mbalimbali ya maana ya haki. Na chanzo ya migongano ya mawazo kuhusu haki na ukweli ulipojichomoza.
Katika tafsiri nyepesi na sahihi, haki ni jambo ambalo mtu anastahiki au anastahili kuwa nacho. Kwa maana nyingine ni uendeshaji wa jambo kufuatia kanuni au sheria zilizowekwa sahihi na insafu.
Kwa mfano, wajibu wa mwalimu ni kufundisha. Anapotimiza wajibu huo anastahili kupata ujira wake. Ujira huo ndiyo haki yake. Anayeanza uchokozi na ugomvi anastahili kuonywa ama kupigwa. Kipigo atachopata ndiyo haki yake. Anayekiri makosa hupata hukumu. Hukumu hiyo ndiyo haki yake.
Dhuluma ni tendo la uovu. Unapodhulumu maana yake ni kufanya isiyo haki, onea, tesa, taabisha, thakilisha, nyang’anya haki au mali. Vitendo kama hivyo anapotendewa mtu anakosa amani. Dhuluma ni adui mmojawapo mkubwa wa haki na ukweli kama ulivyo unafsi, rushwa na upendeleo.
Mtu anayedhulumiwa huwa dhalili. Anapojitutumua asiwe dhalili hukandamizwa na mwenye nguvu. Hata kidogo alichonacho hunyang’anywa na mdhalimu. Cha kushangaza hata fakiri humsaidia mdhalimu kumsema, kumteta na kumsimanga mtu dhalili.
Awali nimesema haki ni jambo au kitu mtu anachostahiki au anachostahili kuwa nacho. Pili, nimesema adui wa haki ni unafsi, dhuluma, rushwa na upendeleo. Naomba ieleweke pia dhuluma haifanywi kwa sababu ya mali tu, la hasha! Hufanywa pia na dhamira za kutaka cheo, utukufu na ufahari.
Utoaji wa mawazo na matakwa ya nafsi zetu hufanywa kuwa ni mawazo na matakwa ya watu ilhali si kweli. Kufanya hivyo ni kudhulumu nafsi za watu iwe wanamichezo, wanachama, waumini au wafanyakazi. Katika kutenda hivyo ni dhahiri unagawa watu na hilo ni kosa.
Makosa kama hayo mara kadhaa tumeyatenda au kuyashabikia pindi viongozi wetu wanapoturubuni kwa vizawadi na visenti vya kununua pilipili na binzari. Baadhi ya viongozi wetu wa siasa wanapokuwa majukwaani na kutuamrisha tusifanye jambo fulani madhali yeye halitaki akitoa kisingizio wananchi ‘hawataki’, hii ni dhuluma kwa wanachama.
Tumeshuhudia viongozi wetu wakitangaza unafsi wao wa kutaka madaraka kwa udi na uvumba wakitaja wananchi ndiyo wanaotaka yeye awe madarakani, lakini anatumia wapambe na rushwa kuwa nyenzo ya kumuweka madarakani. Hii ni dhuluma kwa wananchi.
Tumepata kuona na kusikia mahala pa kazi, kwenye jumuiya za michezo, viongozi wakitumia unafsi wao kujitajirisha kwa kupindisha kanuni na sheria za kazi au michezo kwa lengo la kuwakandamiza wafanyakazi au mwanamichezo. Hii ni dhuluma.
Tumepata kusikia baadhi ya viongozi wa dini wakitumia maneno matakatifu ya Mwenyezi Mungu kinyume cha maagizo yake kwa kubariki maovu kwa waumini. Wengine huwapumbaza waumini hao kwa maneno ya hofu na kuwafanya dhalili. Hii ni dhuluma kwa waumini.
Maadili yetu yanamomonyoka usiku na mchana kutokana na watu kujaa unafsi. Ili tuondokane na unafsi, haki na ukweli hauna budi kupata watu wake uhuru na nafasi ya kusahihisha makosa na kuondoa dhuluma.