Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, ametoa wito wa amani kufuatia maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha wa 2024 ambayo siku ya Jumanne yalikumbwa na matukio ya vurugu baada ya waandamanaji kuvamia Bunge la Taifa.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Uhuru alielezea masikitiko yake kuhusu Wakenya waliouawa wakati wa maandamano, akisisitiza umuhimu wa viongozi waliochaguliwa kuwasikiliza waliowapigia kura.

“Wakati huu wa majaribu, nataka kuwakumbusha viongozi wote kwamba walichaguliwa na wananchi. Kuwasikiliza wananchi si chaguo bali ni wajibu uliowekwa katika misingi ya katiba yetu na katika misingi ya demokrasia,” alisema.

Bw. Uhuru, aliongeza kuwa serikali haifai kutumia nguvu na kuwa na upinzani dhidi ya Wakenya wanaotekeleza haki zao za kikatiba kwa maandamano ya amani.