Ni yule wa FC Lupopo ya Kongo
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam imemrejesha rasmi, Ismail Baduka, ambaye alikuwa wakala wa golikipa namba moja wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Juma Kaseja, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ile ya kuishi nchini na kuendesha shughuli zake bila ya kuwa na kibali maalum.
Taarifa kutoka Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam zilizolifikia JAMHURI hivi karibuni, zilisema kuwa wakala huyo ambaye alikuwa nchini kwa takriban mwezi mmoja sasa akijitambulisha kama mmojawapo ya viongozi juu wa timu ya soka ya FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliondoka nchini chini ya ulinzi wa askari ya jeshi la Uhamiaji Agosti 29, 2013 kupitia mpaka wa Tunduma.
Banduka alifika hapa nchini akiwa na lengo la kukamilisha taratibu za kumsajili Kaseja ili akaichezee timu ya FC Lupopo ya Kongo. Hata hivyo mchakato huo uliingia dosari baada ya kukamatwa na jeshi la uhamiaji kwa kosa la kuishi nchini kinyume cha sheria.
Taariza zinaeleza kwamba, Banduka alitakiwa kuondoka na ndege ya shirika la ndege la Kenya (KQ) moja kwa moja hadi Lubumbashi, lakini aliomba abadilishiwe ndege baada ya kudai kuwa mke wake ni mjamzito kwa hiyo isingekuwa vyema yeye kupanda ndege ya moja kwa moja hadi Lubumbashi.
Katika harakati za kuhakikisha kuwa wakala huyo anaondoka nchini, Idara ya Uhamiaji ilifanya jitihada za kubadilisha ndege na kufanikiwa kupata ile ya Shirika la ndege la Precision iliyokuwa ikielekea mjini Mbeya.
“Ameondoka hapa Dar es Salaam na mke wake kwa ndege ya shirika na ndege la Precision ya saa tano kuelekea Mbeya. Baada ya kushuka pale uwanja wa ndege wa Mbeya alisafirishwa kwa basi kuelekea mpaka wa Tunduma. Hakukuwa na jinsi ya kumuachia huyu bwana kuendelea kuishi hapa nchini kwasababu kwa jinsi tulivyomuhoji, ni mtu ambaye afai kabisa kuendelea kuwepo hapa nchini,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Kuondoka kwa Banduka kumewaweka njia panda vijana wawili raia wa Nigeria waishio jijini Dar es Salaam ambao aliwatapeli pesa zao kwa kisingizio cha kutaka kuwatafutia timu za soka nje na ndani ya nchi.
Wakiongea na gazeti JAMHURI vijana hao walisema kuwa hawakujua kama Banduka anaondoka, kwani siku ile ya kuondoka alikuwa ameahidi kukutana nao ili awarudishie pesa zao. Vijana hao walimpatia kiasi cha dola 1,350 za Marekani.
Huyu jamaa katwambia leo asubuhi tukutane nae ili aweze kutupatia pesa zetu lakini tulipofika hatukumkuta, kumbe alijua kuwa anaondoka. Kweli ametuacha katika wakati mgumu na mpaka sasa hatujajua hatima yetu. Tulitegemea kuwa tungetumia pesa hizo kama nauli ya kurejea kwetu Nigeria,” Alisema mmoja wa vijana hao kwa njia ya simu.
Baada yakupata taarifa za awali, Agosti 7 mwaka huu, askari kutoka Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam walifanikiwa kumtia mbaroni Banduka akiwa katika moja ya nyumba za kulala wageni eneo la Magomeni Kondoa jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumfanyia msako alikutwa na hati nne za kusafiria zenye majina ya tofauti. Tatu za raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakati moja ilikuwa ya mtanzania ambaye pia aliwahi kuwa golikipa wa timu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Aman Simba.
Agosti 14 Banduka alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka ya kuishi nchini bila kibali kinyume cha kufungu cha 31(1) (i) na (2) cha sheria yaUhamiaji, Sura 54 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Banduka alikiri makosa hayo ambapo Hakimu mkazi, Hellen Riwa, alimhukumu kifungo cha miezi mitatu jela ama kulipa faini ya Sh. 150,000. Alilipa faini hiyo na kunusurika kwenda jela. Baada ya hapo Banduka alikabidhiwa tena katika mikono ya Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria.