chikawa copyMaisha ya Watanzania yapo hatarini kutokana na mtandao wa wafanyabiashara ya kusafirisha binadamu duniani (human traffickers) kutoka nchini Pakstan kuivuruga Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, kwa kutengeneza mtandao ndani ya Idara ya Uhamiaji.
  Vyanzo vya habari vya uhakika vimelidokeza JAMHURI kuwa mtandao huo umeweza kuwateka baadhi ya wakubwa katika Idara ya Uhamiaji na kusimika mizizi yake, hali inayowawezesha kusafirisha Wapakistani na Wasomali bila wasiwasi kupitia hapa nchini kwenda Afrika Kusini.
  Wapakistan hao waliojenga mtandao kwenye idara wamekuwa na mawasiliano ya karibu na baadhi ya makamishna katika Idara Uhamiaji nchini na kuafikiana wasibughudhiwe katika biashara yao ya kusafirisha binadamu.  
 Imeelezwa kuwa baadhi ya makamishna katika idara hiyo wamekuwa wakiwasiliana na kukutana na Wapakistan hao Jijini Dar es Salaam na wakati mwingine nje ya nchi.
 Katika maafikiano yao ya mwaka 2014 ilikuwa ni kuwashughulikia wote wanaokwenda kinyume na mtandao huo katika Idara ya Uhamiaji kwa kuwahamisha vituo vya kazi mpango ambao ulikamilika mwishoni mwa mwaka jana na kuilazimu idara kufanya uhamisho wa watendaji nchi nzima, uhamisho ulioigharimu Serikali kiasi cha Sh billion 2.6, ambazo hadi sasa hazijalipwa kwa maafisa hao.
  Mtandao uliopo ndani ya Idara ya Uhamiaji ulikasirishwa na kitendo cha kuondolewa kwa mfadhili wao ambaye ni mmoja wa vigogo wa mtandao wa biashara ya usafirishaji binadamu nchini, aliyefahamika kwa jina la Ajaz Ahmed.
 Ahmed alifukuzwa nchini Oktoba 29, 2014 kwa kupewa PI (Prohibited Immigrant) na Idara ya Uhamiaji  ambapo aliondolewa nchini chini ya ulinzi mkali na kupandishwa ndege kurudishwa kwao Pakistan.
  Pamoja na Ahmed kuondolewa nchini chini uangalizi maalum, mtandao wake ulifanya mpango wa kumtorosha katika uwanja wa ndege cha Doha ambapo alipumzika kwa muda huku ndege aliyosafiri nayo ikiondoka bila uwepo wake. Kwa kufanya hivyo alifanikiwa kuwakwepa maafisa waliokuwa wakisubiri kumpokea nchini Pakistan.
  “Ajaz alikaa Doha kwa zaidi ya saa 12 hivyo kuwapoteza maafisa waliotakiwa kumpokea na kumfikisha panapohusika, kutokana na mpango huo, aliweza kuingia nchini kwake bila tatizo lolote na kufanya mpango wake wa kupata hati mpya ya kusafiria kwa njia anazozjijua mwenyewe,” kinasema chanzo chetu.
  Pamoja na kuondolewa kwa PI Oktoba, mwaka jana, Ajaz aliweza kurudi nchini kupitia Nairobi, Kenya, kisha akaingilia Namanga na kuanza maisha upya jijini Arusha, wiki mbili tangu alipoondolewa huku akielezwa kuingia nchini kwa kutumia hati mpya ya kusafiria kutoka nchini kwake.
 Ajaz anatuhumiwa kwa kosa la kufanya biashara ya kusafirisha binadamu, kuhusika na mauaji ya wahamiaji haramu yaliyofanyika katika msituni ya Kilambo, karibu na mpaka wa Msumbiji mkoani Mtwara, mwaka jana.
  Pamoja na kuondolewa chini ya ulinzi mkali, Ajaz aliendelea kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na wanamtandao katika Idara ya Uhamiaji ambao ndiyo waliomuwezesha kurudi nchini bila usumbufu.
Kiongozi wa mtandao aliyebaki nchini, ambaye awali alikuwa anauza magari katika eneo la Morocco, kwa sasa anafanya biashara ya furniture (samani) eneo la Magomeni, na huyu ndiye anayetajwa kufadhili harakati zote za Ajaz kurejea nchini kuendeleza biashara hiyo haramu.
 “Ajaz ana mawasiliano ya karibu na watu wake waliopo idarani, na waliweza kufanikisha ujio wake wa mara ya pili kwa kuhakikisha hazuiliwi uwanja wa ndege, na ameingia kwa madai ya kutopewa PI bali inaonesha alipewa OD (Order for Departure) na tayari ameshafanya maandalizi ya kumuwezesha kupata mpaka uraia,” alisema mtoa habari wetu.
  Imeelezwa kuwa Ajaz amekasirishwa na kitendo cha baadhi ya maafisa Uhamiaji kusimamia kuondolewa kwake nchini mwishoni mwa mwaka jana, hivyo amejipanga kuhakikisha anawashughulikia wote waliofanikisha kuondolewa kwake.
  Ajaz Ahmed raia wa Pakistani aliondolewa nchini na kunyang’anywa hati yake ya kusafiria iliyokuwa na namba KH.377690  iliyotolewa Karachi ya Mei 12, 2013.
 Pamoja na kurudi nchini kinyemela, Ajaz amelazimika kujificha mkoani Arusha ambako amepewa hifadhi na raia mwingine wa Pakistan ambaye amekuwa akiwahifadhi Wapakistani wenzie waliofukuzwa nchini.
  Mohamad Arshad, ambaye naye alifukuzwa nchini mwaka 2010, aliweza kurudi Tanzania mwaka 2014 akifahamika kwa jina la Mohamad Bilal ambaye kwa sasa anaishi mkoani Arusha pamoja na Ajaz wakiwa wamehifadhiwa na rafiki yao anayefahamika kwa jina la Ikbar, ambaye kazi yake kuu ni kutengeneza viza bandia za nchi mbalimbali.
 JAMHURI imedokezwa kuwa raia wengi wa Pakistan walioondolewa nchini kwa nguvu, hivi sasa wamerejea na wanaendelea na biashara ya kusafirisha binadamu kama ilivyokuwa awali.
  Idara ya Uhamiaji iliwafukuza nchini Golana Mortoza, raia wa Bangladesh, aliyekuwa na makazi yake Dar es Salaam na Mombasa  ambaye alipewa PI Na. 0056771, Abdul Kashem, raia wa Bangladesh aliyekuwa na makazi yake Dar es Salaam na Uganda PI yake ilikuwa ni Na. 0047437, Mohammed Aqeeb Farouk, raia wa Pakistan  PI Na. AA1333562 aliyekuwa na makazi Dar es Salaam na Kenya.
  Wengine waliofukuzwa nchini ni Jamal Uddin Abddul, raia wa Bangladesh aliyekuwa na makazi jijini Dar es Salaam, PI Na. 0049580, Mobin Mohammed Arif, raia wa Malawi, PI Na.0047454, Salim Ashraf Jaffer, raia wa Kenya alikuwa na makazi yake jijini Dar es Salaam, Nairobi na Uingereza.
  Wafanyabiashara hao wamekuwa wakisafirisha binadamu kwa kutumia boti zinazosafiri usiku kutoka Zanzibar na kuwashushia Bagamoyo katika bandari bubu nyakati za usiku.
 Baada ya safari hiyo ya usiku, husafirishwa kwa njia ya barabara na kufichwa Kibaha Mkoa wa Pwani katika moja ya ngome yao (jina linahifadhiwa), kisha husafirishwa mpaka Kongowe ambako hutumia usafiri wa pikipiki huku wasafirishaji wakiwapitisha njia za panya mpaka Chamazi  hadi Nyamisati, ambako hutumia njia ya bomba la gesi hatimaye kufika mikoa ya kusini na kisha kuvushwa na kuelekea nchi ya Msumbiji.
  Mtandao wa biashara hiyo nchini, makao makuu yake yapo nchini Afrika Kusini, pia umekuwa ukiwasiliana kwa ukaribu na wanamtandao waliopo katika nchi za  Kenya, Malawi, Pakistan, Bangladesh, Nepal, India,  Msumbiji na Zimbabwe.
  Taarifa zinaonesha kuwa katika kujizatiti na kuboresha mtandao wao, wanamtandao hao wamejiweka karibu na baadhi ya vigogo wenye nia ya kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa kuwawezesha kifedha huku mmoja wao akidaiwa kuandaliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya kupita katika uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.
  “Hivi unavyoona kuna watu wameshaahidiwa na wengine kusaidiwa katika harakati zao za kusaka ubunge, hivyo wanafanya kila liwezekanalo kufanikisha hilo ili kujijenga zaidi hapa nchini. Huwezi kuamini mtandao huu unabebwa na watu ambao huwezi kuwadhania,” kilieleza chanzo.  
  Pamoja na mtandao huo kujitanua nchini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia kwa watendaji wake wakuu, imekuwa ikijidai inapambana kufa na kupona kuvunja mtandao huo hatari.
  Vyanzo vya habari kutoka wizarani humo vimedokeza kuwa baada ya taarifa za kuingia nchini kwa Ajaz, Wizara ilimtaka Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile, kueleza ni kwa nini Ajaz amerudi nchini, jambo ambalo hajalifanya.
  Inaelezwa kuwa pamoja na juhudi za Serikali kuhakikisha idara hiyo nyeti ya usalama wa nchi inatimiza wajibu wake, imekuwa na makundi  katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku kutokana na kuvurugwa na mtandao huo hatari duniani.
  Kamishna wa Operesheni na Mipaka, Abdullah Abdullah, aliiambia JAMHURI kuwa maafisa wake wanafanya juhudi kumsaka Ajaz kama kweli yupo nchini.
  “Vijana wangu wanaendelea na msako, kama una taarifa zozote itakuwa vyema kama utaweza kutupatia maana hii nchi ni yetu sote. Nakuhakikishia kama yupo nchini tutamkamata tu, maana taarifa zake zipo kila mpaka wa nchi,” alisema Abdullah.
 Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, amesema ulinzi wowote wa nchi unategemea ushirikiano, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kusaidia kupatikana kwa Ajaz.
  Pereira alieleza kuwa wizara itafanya uchunguzi wa kina kubaini iwapo kuna watendaji wanaokiuka maadili na iwapo watabainika hatua stahiki kuchukuliwa dhidi yao.
  Alieleza kuwa wizara hiyo imekuwa ikipata taarifa mbalimbali kutoka kwa raia wema na kuzifanyia kazi, hivyo kusaidia kupambana na uhalifu nchini.
  “Taarifa kama hizo ofisi yangu haijazipata, ila kutokana na jambo hilo kuendelea kuonekana kuwa ni tatizo, tutajipanga na kupambana na uhalifu huo pamoja na mwingine wowote utakaojitokeza, ukizingatia idara hii ni ya kipolisi, ni jukumu la kila askari kufanya kazi kwa weledi. Ninaloweza kusema ni kuwa idara ni imara na inafanya kazi kwa  maslahi ya usalama wa nchi yetu,” amesema Silima.