Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam inatuhumiwa kwa kukiuka sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia idara hiyo, huku Kamishna wa Idara hiyo, Mkoa wa Dar es Salaam (RIO), John Msumule, akibebeshwa mzigo.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umethibitisha pasi na shaka kwamba kamishna huyo amekuwa akifanya uamuzi unaogharimu usalama wa raia na mali zao, kwa kukiuka taratibu za nchi na Idara ya Uhamiaji nchini.
Uchunguzi umebainisha kwamba Mei 28, 2015 maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji walimkamata Khaled Abduel Latif Daasenous, raia wa Jordan, katika nyumba aliyokuwa akiishi Upanga, Jijini Dar es Salaam.
Mtuhumiwa alikamatwa akiwa anawafundisha vijana michezo ya judo na karate. Khaled amekuwa akitoa mafunzo hayo nchini bila kupata kibali kinachomruhusu kufanya hivyo.
Khaled aliingia nchini Aprili 17, 2014 na kibali chake cha kuwapo nchini kilikwisha Julai 17, 2014. Pamoja na kukamatwa na kutakiwa kutoa maelezo kwa maafisa Uhamiaji, mtuhumiwa hakutii maelekezo.
Raia huyo wa Jordan anamiliki hati ya kusafiria yenye namba M 224917 iliyotolewa Aprili 15, 2013 na itakwisha muda wake Aprili 14, 2018. Aprili 17, 2014 alipatiwa viza ya Tanzania namba URT 0217726 iliyokuwa ikimzuia kufanya kazi yoyote nchini kwa siku 90, iliyomalizika Julai 17, 2014.
Kwa mujibu wa nyaraka za siri zilizoko katika ofisi ya Kamishna wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, ametoa maelekezo kwa maafisa wa Uhamiaji kwamba; “Mtuhumiwa (Khaled) hana hadhi ya uhamiaji (immigration status) tangu mwaka 2014 na amekataa kutoa maelezo.
“Naelekeza awekwe ndani katika Kituo cha Polisi cha Kati hadi kesho atakapokuja kutoa maelezo,” inasomeka sehemu wa waraka wa siri wa mkuu huyo wa Idara ya Uhamiaji.
Katika waraka mwingine wa Mei 29, 2015, ambao JAMHURI imeuona, Kamishna huyo ananukuliwa akieleza kuwa Khaled akikataa kutoa maelezo tena afukuzwe nchini mara moja.
“Akikataa kutoa maelezo tena afukuzwe nchini mara moja chini ya ulinzi hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). Anaonekana ana vurugu. Pia mke wake ambaye ni raia wa Canada aitwe aeleze shughuli anazofanya mume wake ni nini, muda wote awe chini ya ulinzi. Apelekwe Kituo cha Polisi cha Kati hadi kesho,” inasomeka sehemu ya maelekezo ya Kamishna Msumule.
Siku hiyo Mei 29, Kamishna huyo anatoa maagizo kwamba “Huyu aondolewe nchini kwa PI (Prohibited Immigrant) ndani ya siku tano.”
Hata hivyo, pamoja na Kamishna Msumule kuagiza kuondolewa kwa mtuhumiwa kutokana na kutotakiwa nchini kwa kumpiga PI baada ya Khaled kuwekwa chini ya ulinzi katika Kituo cha Polisi cha Kati, Mei 30, alikwenda kituoni hapo kumuwekea dhamana mtuhumiwa huyo na kumtoa nje ya kizuizi.
Juni 3, 2015 Kamishna Msumule alitoa maagizo ya ziada kwa maafisa wake kufuta PI ya Khaled na kuwataka kumpatia kibali cha kuondoka nchini (Order for Departure).
“Baada ya kuwasiliana na afisa wa UAE alinikumbusha kuwa PPT hii ililetwa kwa masuala ya immigration status ndipo mimi nikaizuia hadi sasa na kwa kuwa mhusika Khaled hakufuatilia kujua nini kinaendelea na pia tayari amesha-overstay na hana shughuli muhimu, naagiza badala ya kumpa PI apewe OD 7 days by air kwa kuwa mke wake yuko hapa Dar,” Msumule anasema kwa maandishi.
Juni 2, 2015 ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam ilitoa amri ya kuondoka nchini kwa mtuhumiwa Khaled ambayo ilikuwa inafikia ukomo Juni 9. Juni 7, 2015 Khaled aliondoka nchini kuelekea Lusaka, Zambia kwa usafiri wa ndege.
Kutokana na mkanganyiko huo wa uamuzi, JAMHURI imewasiliana na Kamishna Msumule kupata ufafanuzi kuhusu uamuzi na maagizo yaliyotoka kwenye dawati lake. Aliiomba JAMHURI impatie muda afuatilie suala hilo na kutoa uamuzi.
Hata hivyo, baada ya saa moja na nusu Kamishna Msumule aliwasiliana na JAMHURI na kusema Idara ya Uhamiaji iliamua kumpatia mtuhumiwa amri ya kuondoka nchini Juni 2, 2015 na Juni 7, 2015 aliondoka kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Kamishna huyo anasema PI haiwezi kufutwa na Idara ya Uhamiaji maana haina mamlaka hayo na kueleza kwamba ufutwaji wa amri kama hizo hutolewa na mamlaka za juu.
Anasema amri ya kuondoka nchini si lazima ifutwe maana mhusika anaweza akaondoka na kurudi wakati wowote anaotaka na akafananisha tukio hilo na kadi ya njano katika mpira wa miguu.
Kamishna Msumule alipohojiwa aliko mtuhumiwa Khaled amesema; “Unajua nchi hii mipaka ipo mingi; Namanga, Holili, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na mingine mingi. Anaweza akaingilia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na akakaa Moshi, mpaka afanye makosa akamatwe ndiyo nijue yuko wapi. Lakini kama JAMHURI inajua itwambie tukamkamate.”
Taarifa ambazo JAMHURI imezipata zinaonesha mtuhumiwa Khaled anaishi Oysterbay, jijini Dar es Salaam na hata alipopigiwa simu ilipokelewa na mwanamke anayesadikiwa kuwa mke wa Khaled.
Kuhusu Kamishna huyo kwenda kumtolea mtuhumiwa dhamana katika Kituo cha Polisi cha Kati, Msumule amekiri kumtolea dhamana. Na alipotakiwa kueleza kilichomsukuma kufanya hivyo akasema; “Unajua tunazo sero zetu, ila huwa hatupendi watu kukaa mahabusu maana tunaitia hasara Serikali.”
Kamishna huyo alipoulizwa kwa nini amepingana na uamuzi wake katika sakata hilo, ameng’aka na kusema taarifa hizo anazomdodosa mwandishi ni za siri na kwamba zimefungiwa katika makabati, hivyo ni kosa kupelekwa kwa waandishi wa habari.
“Nani kakupatia mafaili yetu ya siri? Nikuelimishe hii kwa faida yako. Unaingilia taarifa ambazo sizo na ninachojua huyu tulimkamata kwa kukaa muda mrefu nchini bila kibali, hilo la kutoa mafunzo ndiyo nasikia kwako na tambua hapa unaongelea masuala ya siri, hizi taarifa umezipata wapi?” anahoji Kamishna Msumule.
Kamishna huyo ameamua kutumia vitisho kwa JAMHURI kwa kusema iwapo hataambiwa taarifa hizi za siri zimefikaje ofisi za gazeti hili atachukua hatua; “Taarifa hizi za siri umezipata wapi? Bora useme vinginevyo tutakuchukulia hatua. Hatuwezi kukubali taarifa hizi za mafaili za kiofisi zikufikie. Kuna siri za ofisi, tunawataka watu wanaotoa taarifa nje ya ofisi tuwakamate na kuwachukulia hatua.”
JAMHURI ilimtafuta Kaimu Kamishna Mkuu wa Uhamiaji nchini, Lilian Lembeli, na anasema taarifa hizo amezisikia ila hawezi kuzitolea majibu kwa vile hazijafika ofisini kwake.
“Haya ni masuala ya utendaji. Ni lazima kufuatilia ule utendaji ulikwendaje na maamuzi yale yalitolewa vipi, lakini kama unataka kufahamu kuhusu PI inafutwa na Waziri siyo vinginevyo,” anasema Lembeli.
Maswali waliyosema wanabaki nayo wasaidizi wa Kamishna wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam ni pamoja na kwa nini abadili uamuzi wake ndani ya muda mfupi? Je, ni utaratibu Kamishna wa Uhamiaji kwenda kudhamini watuhumiwa Polisi? Nini kilichomsukuma au kumshawishi kumdhamini mtuhumiwa? Aliwahi kufanya hivyo kwa mtuhumiwa mwingine au la?