Ni ukweli usiopingika kuwa pamoja na jitihada za serikali katika kuhakikisha inapunguza tatizo la upungufu wa nyumba za walimu, bado kuna changamoto kubwa kwenye sekta hii nyeti (moyo wa taifa) kwa mustakabali wa taifa!

Kwa mujibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), mwaka 2010 zilihitajika nyumba za walimu 165,210 lakini nyumba zilizokuwapo wakati huo ni 46,670, hivyo kuwapo kwa upungufu wa nyumba 118,540.

Kwa kipindi hicho hadi sasa serikali na wadau wamejenga nyumba kadhaa, bila kusahau nguvu za wananchi. Hata hivyo, bado mahitaji ni makubwa, kwa kuwa shule mpya zimejengwa na walimu wengi wameajiriwa.

Licha ya kuwa takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kwa kipindi cha miaka sita serikali imeongeza nyumba 16,613 kutoka mwaka 2010, ikiwa ni ongezeko la nyumba 41,835, hivyo kuwa nyumba 58,448 Februari, 2015.

Upungufu wa nyumba za walimu ni mkubwa na unaleta adha kwa walimu. Hali hii ni mbaya zaidi hasa kwa walimu wa vijijini ambako hakuna hata nyumba za kupanga na kama zipo zenye hadhi ya mtumishi zinakuwa mbali na shule.

Hali hii inasababisha walimu kutembea muda mrefu kwenda kazini, hivyo wakati mwingine humfanya mwalimu achelewe kazini.

Vilevile tatizo hili la uhaba wa nyumba za walimu husababisha mwalimu kuwahi kuondoka katika kituo cha kazi ili awahi kupika na kufanya maandalizi ya masomo ya siku inayofuata.

Wakati mwingine mwalimu akiwa shuleni hufundisha huku akiwaza jinsi gani atakamilisha ratiba ya siku husika.

Kwa upande wa wanafunzi, wanakosa msaada wa ziada pindi wanapohitaji kumuuliza swali mwalimu binafsi baada ya muda wa masomo, kwa kuwa walimu wanakuwa wamekwisha kwenda sehemu hizo za mbali wanakopanga.

Hali hii inawafanya walimu kutovutiwa kufanya kazi vijijini, jambo ambalo linakwamisha utoaji wa elimu bora.

Vilevile upungufu huu wa nyumba za walimu unasababisha gharama kwa mwalimu anapopanga, kwa kuwa hutegemea mshahara; hana posho yoyote kwa mwezi isipokuwa kwa wakuu wa shule na waratibu elimu.

Napaza sauti yangu kushauri serikali kuingia ubia na wawekezaji katika sekta ya ujenzi ili nyumba za walimu zijengwe nchi nzima na serikali iweke kiwango cha kodi ya pango itakayokuwa nafuu kwa walimu, itakayokuwa ikilipwa kwa mwezi kwa walimu watakaopanga kwenye nyumba hizo ili kurudisha gharama za ujenzi. Mfano, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lingejikita katika mradi wa kujenga nyumba za watumishi mahala pa kazi, hasa vijijini.

Mashirika ya mifuko ya hifadhi ya jamii badala ya kujikita kwenye miradi isiyokuwa na tija kwa nchi na wanachama wa mifuko, wangewekeza katika kujenga nyumba za watumishi.

Pia, jamii isaidie kujenga baadhi ya nyumba za walimu kwa kuwa manufaa ya elimu ni kwa wote.

Sekta binafsi ijitose kusaidia kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu kama anavyofanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Ikumbukwe kuwa taaluma zote nchini na duniani zimepatikana kutokana na kazi tukufu ya mwalimu na hii inadhihirisha kuwa mwalimu ni muumbaji wa pili baada ya Mungu!

Hivyo, kila mmoja wetu tujiulize, bila mwalimu ungekuwa ulivyo sasa?

0765757179