Kwa mujibu wa madaktari waliopo katika eneo hilo na shirika la afya duniani WHO, zaidi ya watu 50 wamefariki kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na ugonjwa usiojulikana.
Mkurugenzi wa hospitali ya Bikoro, kituo cha ufuatiliaji wa afya, Serge Ngalebato, ameliambia shirika la habari la AP kwamba muda kati ya kuanza kwa dalili na kifo ni saa 48 kwa wagonjwa wengi.
Ngalebato amesema hali hiyo inatia wasiwasi.Mlipuko wa ugonjwa huo usiojulikana ulitokea mnamo Januari 21 na hadi sasa wagonjwa 419 wameripotiwa, ikiwemo vifo vya watu 53.
Kwa mujibu wa ofisi ya WHO barani Afrika, mlipuko wa kwanza katika mji wa Boloko ulitokea baada ya watoto watatu kula popo na kufariki ndani ya saa 48 baada ya kuonyesha dalili za homa na kutokwa na damu.
Mwaka jana, ugonjwa mwengine usiojulikana ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 100 kusini magharibi mwa Kongo japo baadaye iligundulika kuwa ni aina kali ya malaria.
