Tanzania imeihakikishia Uganda kuwa itaendelea kuipa ushirikiano katika kujenga uwezo wa usimamizi wa sekta ya Mawasiliano na TEHAMA, sambamba na kudumisha ushirikiano wa kitaalam katika usimamizi wa sekta hizo.
Akizungumza wakati alipoukaribisha ujumbe wa Tume ya Mawasiliano Uganda (UCC), ukiongozwa na Waziri wa Nchi anaeshughulikia Ulinzi na TEHAMA, Kabbyanga Godfrey uliofika katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ziara ya mafunzo na kubadilishana ujuzi, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Andrew Mathew amebainisha kuwa, Tanzania imefanikiwa kusimamia vilivyo sekta ya Mawasiliano kwa kuweka Sera Madhubuti za usimamizi wa huduma za Mawasiliano, huku akiwahakikishia wageni fursa tele ya kujifunza katika sekta ya Mawasiliano.
“Tanzania imepitisha sera zinazounga mkono ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano – TEHAMA na mfumo wa kisheria na udhibiti unaounga mkono ukuzaji wa uchumi wa kidijiti,” alisisitiza Kundo na kuongeza kuwa “Ninakuhakikishia ujumbe wako kwamba utapata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu ambao utakuwa muhimu katika marekebisho ya Sheria yenu ya Mawasiliano ya 2013,” amebainisha.
Kwa upande wake Waziri Kabbyanga akishukuru baada ya ukaribisho alimweleza Naibu Waziri Kundo, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari na Menejimenti ya TCRA lengo la ziara yao Tanzania kuwa ni kujifunza zaidi namna Tanzania inavyosimamia huduma za Mawasiliano ambao ziara yao mahususi katika ofisi za TCRA ililenga kujifunza namna Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali inavyowezesha usimamizi wa sekta ya Mawasiliano.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili kwenye ofisi za TCRA jijini Dar es Salaam Waziri wa Nchi anaeshughulikia Ulinzi na TEHAMA Mheshimiwa Kabbyanga Godfrey alimweleza mgeni wake Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Kundo Mathew kwamba Uganda imeona vema kuja kujifunza Tanzania kwa kuzingatia ujirani na namna ambavyo Tanzania imefanikiwa katika kusimamia na kudhibiti sekta ya Mawasiliano.
“Tumeambiwa kwamba Tanzania mnazo Sheria Madhubuti za usimamizi wa sekta ya mawasiliano Tumekuja hapa kwa sababu mazingira yetu ni sawa na ya Tanzania hivyo tumeona hapa kwenu tutajifunza na kupata maarifa yenye uhalisia zaidi, tofauti na tungeamua kwenda kujifunza sehemu nyingine,” amesisitiza Kabbyanga.
Ameeleza kwamba pia Uganda inanuia kuboresha huduma za Mawasiliano ya simu kwa raia wake hivyo imeamua kuja Tanzania kujifunza katika eneo linalohusu Mawasiliano ya simu.
Ziara ya Tume ya Mawasiliano Uganda kuzuru Tanzania, na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni mwendelezo wa Mamlaka mbalimbali za Usimamizi wa Mawasiliano za Afrika kufika Tanzania kujifunza na kubadilishana ujuzi wa usimamizi wa huduma za Mawasiliano. Miongoni mwa nchi nyingine zilizozuru TCRA mwaka huu ni pamoja na Malawi, Zimbabwe, Burundi, Rwanda, Uganda, na Msumbiji.